Dk Mpango aitaka Takukuru kujiandaa kudhibiti rushwa uchaguzi mkuu wa 2025

December 16, 2024 5:56 pm · Lucy Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Asema viongozi wanaochaguliwa kwa njia ya rushwa hawawezi kutatua kero za wananchi.
  • Aipongeza kwa kuokoa Sh18 bilioni ndani ya mwaka mmoja.

Arusha.  Makamu wa Rais wa Tanzania Dk Philip Mpango ameitaka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kujiandaa kudhibiti rushwa wakati wa uchaguzi mkuu utakaofanyika mwaka 2025.

Uchaguzi huo wa Rais, wabunge na madiwani utakaofanyika nchini mwakani ni miongoni mwa matukio yanayodaiwa kuwa na vitendo vingi vya rushwa kutoka kwa wagombea wanaowashawishi wananchi kuwapigia kura katika nafasi mbalimbali wanazozigombea.

Dk Mpango aliyekuwa akizungumza katika mkutano wa mwaka wa viongozi wa Takukuru leo Disemba 16, 2024 amewakumbusha viongozi hao kuanza jitihada za mapema za kuzuia rushwa katika uchaguzi mkuu kama ilivyofanyika katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa.

“Nipende kusisitiza tunapoelekea katika uchaguzi mkuu mwakani nawakumbiusha viongozi na watumishi wa Takukuru kujidhatiti kupambana na vitendo vya rushwa ambavyo vina madhara makubwa kwa maendeleo ya Taifa…

…Kama mnavyofahamu viongozi wanaochaguliwa kwa njia ya rushwa si kwamba hawewezi kukemea vitendo vya rushwa lakini pia hawawezi kutatua kero za wananchi na kusimamia vyema miradi ya maendeleo,” amesema Dk Mpango.

Kwa mujibu wa Dk Mpango mkutano huo uliokutanisha viongozi wa Takukuru 204 kutoka maeneo mbalimbali nchini ni fursa ya kuthamini masuala muhimu ikiwemo sheria, kanuni na taratibu zinazotumika kukamata na kuhukumu watuhumiwa wa rushwa nchini.

Pia amewataka kuzitumia siku nne za mkutano huo kujadili njia za  mapendekezo yaliyotolewa na tume ya haki jinai kwa kuwa taasisi yao ni miongoni miongoni mwa taasisi za haki jinai ambazo zimekuwa zililalamikiwa sana na wananchi.

Itakumbukwa kuwa Rais Samia Suluhu Hassan January 31, 2023 aliunda tume ya kuangalia jinsi ya kuboresha taasisi za haki jinai nchini ikiwa na lengo la kubaini changamoto na kutoa mapendekezo ya jinsi ya kuzitatua.

 Julai 15, 2023 tume hiyo iliyokuwa na wajumbe tisa ilikabidhi ripoti yake kwa Rais Samia aliyesisisitiza utekelezaji wa mapendekezo yaliyotolewa.

Baadhi ya vongozi wa Takukuru katika mkutano mkuu wa mwaka unaofanyika kwa siku nne jijini Arusha. Picha|Takukuru.

Takukuru yaokoa Sh18 bilioni ndani ya mwaka mmoja

Crispin Chalamila, Mkurugenzi Mtendaji wa Takukuru aliyekuwa akizungumza katika mkutano huo amesema taasisi hiyo imeokoa kiasi cha Sh18 bilioni kupitia oparesheni mbalimbali za uchunguzi zilizofanyika kipindi cha Januari hadi Disemba mwaka huu.

“Fedha hizo zimerudishwa serikalini na nyingine zinatumika katika utekelelzaji wa miradi ya maendeleo kama inavyokusudiwa  na hivyo kuchangia katika ustawi wa wananchi,”amesema Chalamila.

Aidha, Chalamila amesema kwa kipindi hicho pia walishinda asilimia 75.9 ya mashtaka ya rushwa yaliyofikishwa mahakamani likiwa ni ongezeko la asilimia 6.2 kutoka asilimia 69.7 waliyoshinda mwaka jana ambapo watuhumiwa walihukumiwa kwa mujibu wa sheria.

Licha ya mafanikio hayo, George Mkuchika Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Ikulu (Kazi Maalum) amewataka kutobweteka na kuendeleza mapambano hayo dhidi ya rushwa hususani katika uchaguzi ujao.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks