Dk Mpango ataja mambo yatakayokuza biashara ya kaboni Tanzania

March 6, 2025 4:08 pm · Lucy Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni pamoja na kukuza uelewa juu ya biashara hiyo na uwazi wa mikataba ya biashara.
  • Miradi 72 ya biashara ya kaboni imesajiliwa kufikia Februari 2025.

Arusha. Makamu wa Rais Dk Philip Isdory Mapango ameainisha mambo muhimu yanayotakiwa kutupiwa macho ili kuchochea ukuaji wa biashara ya kaboni nchini Tanzania ikiwemo kukuza uelewa kuhusu biashara hiyo kwa wadau na wananchi.

Biashara ya kaboni ni mfumo katika soko la dunia ambao unakusudia kupunguza gesi joto ambazo zinachangia kuongezeka kwa joto la dunia hasa ikiwemo hewa ukaa (carbondioxide) ambayo inatokana na shughuli za viwanda na uchomaji wa uoto na ukataji wa miti.

Dk Mpango aliyekuwa akizungumza katika mkutano wa taasisi na mashirika ya umma kuhusu mabadiliko ya tabianchi na biashara ya kaboni  jijini Dar es Salaam leo Machi 6, 2025 amesisitiza kuwa bado watu wengi hawana uelewa juu ya biashara hiyo.

“Biashara ya kaboni bado haiweleweki kwa walio wengi na  hivyo kushindwa kutumia fursa hiyo kwa walio wengi ni matumaini yangu kuwa wataalamu waliopo kutoka wizara, taasisi na makampuni ambayo tayari wanatekeleza miradi ya aina hiyo watatusaidia kutupa uzoefu ili tuifahamu vyema iashara hiyo,” amesema Dk Mpango.

Tanzania ni miongoni mwa nchi wanachama wa Mkataba wa Mabadiliko ya Tabianchi, Itifaki ya Kyoto na Makubaliano ya Paris inayoiwezesha kufanya biashara hiyo na mataifa mengine duniani.

Licha ya rasilimali lukuki zinazoweza kuzalisha kaboni nchini Tanzania Dk Mpango amewaambia wahudhuriaji wa mkutano huo kuwa mpaka kufikia mwishoni mwa mwezi Februari Kituo cha Taifa cha Ufuatiliaji wa Kaboni (NCMC) kimesajili miradi 72 ya biashara hiyo.

Uchache wa miradi hiyo huenda pia unasababishwa na  changamoto ya uwazi wa mikataba katika uendeshaji wa biashara hiyo jambo linaloifanya kutokukua kwa viwango vinavyohitajika.

Baadhi ya wahudhuriaji wa mkutano wa taasisi na mashirika ya umma kuhusu mabadiliko ya tabianchi na biashara ya kabon unaofanyika katika Ukumbi wa APC – Mbweni Jijini Dar es Salaam.

Uwazi wa mikataba hiyo utairahishsia Serikali kujua ni jinsi gani wanaweza kuisaidia sekta hiyo kukua pamoja na kuounguza vipengele ambavyo huenda vinawakandamiza wazalishaji wa kaboni nchini.

Pamoja na hayo Dk Mpango amebainisha mambo mengine muhimu yatakayokuza biashara hiyo ambayo ni kujifunza kutoka kwa nchi nyingine, kugeukia matumizi ya nishati safi ya kupikia pamoja na kutumia vyombo vya usafiri vinavyotumia gesi na umeme.

Kwa upande wake Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Muungano na Mazingira Hamadi Masauni amesema kuwa Serikali ipo tayari kuongeza jitihada ili kufikia malengo ya Taifa katika biashara ya kaboni kwa kutumia mbinu mbalimbali kushirikisha wadau kama ilivyofanyika katika mkutano huo.

“Kuna maswali ya kujiuliza je tuelewa kutosha juu ya biashara hii, je tuna weredi wa kutosha? Naamini Kikao hiki kitatusaidia kupata majawabu ya maswali hayo,; amesema Masauni.

Pamoja na hayo Masauni amesema kuwa biashara hiyo inatakiwa kuangaliwa zaidi kutokana na mchango wake katika pato la Taifa na kukuza uchumi wa Tanzania.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks