Dk Bashiru aondolewa nafasi Katibu Mkuu Kiongozi, ateuliwa ubunge
- Ameondolewa katika nafsi hiyo na kuteuliwa kuwa Mbunge wa Bunge la Tanzania.
- Nafasi yake imechukuliwa na Balozi Hussein Kattanga ambaye kabla ya uteuzi huo alikuwa Balozi wa Tanzania nchini Japan.
- Dk Bashiru amedumu katika nafasi hiyo kwa wiki zisizozidi tano.
Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amemuondoa Dk Bashiru Ally katika nafasi ya Katibu Mkuu Kiongozi ambayo ameishikilia kwa wiki zisizozidi tano tangu ateuliwe na Hayati Rais John Magufuli mapema mwaka huu.Â
Nafasi yake imechukuliwa na Balozi Hussein Kattanga ambaye kabla ya uteuzi huo alikuwa Balozi wa Tanzania nchini Japan.
Dk Bashiru aliteuliwa na Hayati Rais Magufuli kuwa kuwa Katibu Mkuu Kiongozi na Balozi Februari 26, 2021 akichukua nafasi iliyoachwa na Balozi John Kijazi aliyefariki Februari 17 wakati akipatiwa matibabu katika hospitali ya Benjamin Mkapa jijini Dodoma.
Samia aliyekuwa akizungumza leo Machi 31, 2021 baada ya kumuapisha Makamu wa Rais Dk Philip Mpango Ikulu, Chamwino mkoani Dodoma baada ya kumuondoa katika nafsi hiyo Balozi Bashiru  ambaye pia alikuwa Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) amemteua kuwa Mbunge wa Bunge la Tanzania.
Soma zaidi:Â
Dk Bashiru ambaye aliwahi kuwa Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) aliteuliwa na Dk Magufuli kushika nafasi ya ukatibu mkuu wa CCM Mei 2018 akichukua nafasi ya Abdurahman Kinana.
Kwa mabadiliko hayo, Dk Bashiru anakuwa Katibu Mkuu Kiongozi wa kwanza ambaye amedumu katika nafasi hiyo kwa muda mfupi kuliko wenzake waliomtangulia.
Utezi wa Kattanga unamfanya kuwa Katibu Mkuu Kiongozi wa 11 wa Tanzania, tangu nchi ilipopata uhuru mwaka 1961.
Balozi Kattanga ni nani?
Balozi Kattanga amewahi kushika nyadhifa mbalimbali serikalini ikiwemo Katibu Mkuu Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais Tamisemi kuanzia mwaka 2011 hadi 2012 na baadaye Mtendaji Mkuu wa Mahakama Tanzania kuanzia mwaka 2012 hadi 2019.
Habari hii imeandikwa na Daniel Mwingira na Daniel Samson.
Latest