Dar es Salaam kinara kwa vifo vya mama wajawazito Tanzania
- Mkoa huo unaongoza kwa vifo 382 licha ya kuwa na vituo vya afya vinavyotoa huduma 1,623.
Dar es Salaam. Kila baada ya dakika mbili, mwanamke mmoja hufariki duniani kutokana na matatizo yanayohusiana na ujauzito au kujifungua.Â
Takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) zinaonyesha kuwa zaidi ya wanawake 260,000 walipoteza maisha mwaka 2023 pekee kutokana na sababu zinazohusiana na uzazi, huku zaidi ya asilimia 90 ya vifo hivyo vikitokea katika nchi za kipato cha chini na cha kati.Â
Tanzania ni miongoni mwa nchi hizo ambazo huripoti vifo vya mama wajawazito wakati wa kujifungua suala linaloacha simanzi kwa wenza, wanafamilia na jamii kwa ujumla.
Kwa mujibu wa ripoti ya matumizi ya mfumo wa kitaifa wa mapitio ya vifo vya uzazi kwa njia ya mtandao katika kuboresha ubora wa huduma wakati wa ujauzito, uchungu wa kujifungua, kujifungua na kipindi cha baada ya kujifungua jumla ya vifo 3,041 vya uzazi vilivyoripotiwa nchini kati ya mwaka 2022 na 2023.
Ripoti hiyo iliyotolewa na Wizara ya Afya Machi 18, 2026 inatolewa wakati ambapo Tanzania ipo kwenye mapambano ya kupunguza idadi ya vifo vya mama na mtoto wakati wa kujifungua.
Kufikia mwaka 2022 Tanzania tayari ilipiga hatua na kupunguza vifo hivyo na kufikia vifo 104 kwa kila vizazi hai 10,000 sula liloifanya Rais Samia Suluhu Hassan kutunukiwa tuzo ya The Global Goalkeeper Award.
Tuzo hiyo ilitolewa Februari, 2025 kwa kutambua mchango wa kiongozi huyo kupunguza vifo vya mama na mtoto kwa asilimia 80.Â
Licha ya hatua ya mafanikio hayo, Tanzania bado inaongeza nguvu kufikia lengo la Umoja wa Mataifa (UN) la kupunguza vifo hivyo hadi chini ya 70 kwa kila vizazi hai 100,000 ifikapo mwaka 2030.
Dar es Salaam Kinara Â
Katika ripoti hiyo Dar es Salaam ni mkoa wa kwanza miongoni mwa mikoa mitano inayoongoza kwa vifo vya akina mama nchini ikiwa na vifo 382 ndani ya kipindi hicho.
Licha ya kuwa kitovu cha biashara na huduma nchini, pamoja na kuwa na hospitali kubwa zinazopokea wagonjwa kutoka maeneo mbalimbali ya Tanzania, mkoa huo umeongoza kwa idadi ya vifo vya uzazi vilivyoripotiwa kuliko mkoa mwingine wowote Â
Hata hivyo, Dar es Salaam inaongoza pia kwa kuwa na vituo vya afya vinavyotoa huduma 1,623 ikifuatiwa na Mwanza (828), Morogoro (822), Dodoma (723) na Tanga (702).
Mkoa wa pili ni Mwanza ikiwa na vifo 309, mkoa huu ni kitovu cha huduma za afya katika Ukanda wa Ziwa ukiwa hospitali kubwa zinazohudumia wagonjwa kutoka mikoa jirani kama Geita, Simiyu, Mara na Kagera.
Morogoro ndio mkoa wa tatu unaongoza kwa vifo 204 licha ya kuongezeka kwa huduma za afya katika miaka ya karibuni, ukubwa wa mkoa na changamoto za kufikia baadhi ya maeneo ya vijijini zinaendelea kuathiri upatikanaji wa huduma za uzazi kwa wakati.Â
Kigoma, iliyorekodi vifo 178 ndio mkoa wa nne, mkoa huu umekuwa ukikabiliwa na changamoto za kijiografia kutokana na umbali wa baadhi ya makazi na vituo vya afya.Â
Mkoa huo pia huhudumia idadi kubwa ya watu kutoka maeneo ya pembezoni mwa Ziwa Tanganyika na maeneo ya mipakani.
Mikoa hiyo mitano pekee ilichangia sehemu kubwa ya vifo vyote vilivyoripotiwa nchini, huku mikoa ya Tanga(59), Ruvuma (49) na Njombe (45) ikiwa na idadi ndogo ya vifo.
Ni zipi sababu za vifo hivyo?
Kulingana na wataalamu wa afya akiwemo Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Wanawake kutoka Hospitali ya Kitonka jijini Dar es Salaam Emmanuel Masali aneleza kuwa sababu kubwa ya vifo kwa wanawake wajawazito ni kuvuja damu nyingi baada ya kujifungua jambo ambalo lina changia asilimia 49 ya vifo kwa wajawazito hao.
Sababu nyingine ni shinikizo la damu la mimba na kifafa cha mimba likichangia asilimia 16, matatizo yanayohusiana na usingizi wa upasuaji asilimia 10 na maambukizi baada ya kujifungua ikiwa asilimia 6.
Vile vile, changamoto katika mfumo wa afya ikiwemo upungufu wa ujuzi wa kitabibu kwa baadhi ya wahudumu wa afya ukichangia asilimia 82 ya vifo, huku mtazamo na mwenendo wa baadhi ya watoa huduma ikiwa asilimia 69 ya vifo hivyo.
Kulingana na WHO, sababu hizo ndizo zinazochangia karibu asilimia 75 ya vifo vyote vya uzazi duniani, huku nyingi zikiwa zinaweza kuzuilika kupitia huduma bora za afya kabla, wakati na baada ya kujifungua.
Je nini kifanyike kuzuia vifo hivyo kwa mama wajawazito? Usikose sehemu ya pili ya makala hii.