Corona ilivyokatisha ndoto za wafanyabiashara wa maua Iringa

August 26, 2021 12:43 pm · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Baadhi yao wafunga mashamba, biashara na kupoteza ajira.
  • Hiyo inatokona na kushuka kwa soko la bidhaa hiyo.
  • Washauriwa kuanza upya na kuangazi masoko ya ndani na mtandaoni. 

Iringa. Alikuwa na ndoto ya kuwa mkulima na mfanyabiashara mkubwa wa maua aliyefanikiwa na kutoa fursa kwa Watanzania wasio na ajira kujipatia kipato. 

Hata hivyo, kila kitu kimebadilika wakati hata ndoto yake haijatimia.

Shamba lake la maua lililopo Wilaya ya Kilolo mkoani hapa limefungwa tangu mwaka jana baada ya kuanguka kwa soko la maua duniani.

Anguko hilo limetokana na athari za janga la ugonjwa wa Corona (Uviko-19) uliosababisha mahitaji ya maua kushuka ulimwenguni.

Nchi mbalimbali zilifunga mipaka yake na safari za anga hivyo kutatiza shughuli za usafirishaji bidhaa ikiwemo maua.

“Shamba limefungwa kwa sasa hamna shughuli inayoendelea, soko hamna nilikuwa nasafirisha nje ya nchi, Corona imeharibu kila kitu,” Reminus Sanga ambaye aliajiri vijana wasiopungua 10. 

Maua hayo waridi ambayo hupandwa kwenye makasha ya plastiki na mbao, Sanga alikuwa akisafirisha kwenda Arusha kwa ajili ya masoko ya nje ikiwemo Kenya na nchi za Ulaya.

Janga hilo pia liliharibu soko la ndani.  Sanga alikuwa ana wateja wake kutokana na shughuli mbalimbali za sherehe zikiwemo harusi kusitishwa na Serikali Machi 2020 baada ya ugonjwa wa Uviko-19 kuingia bado hali haikurudi kama awali.

“Ilikuwa wakati mgumu sana, biashara hiyo nilikuwa naitegemea sana na nilikuwa na malengo kuwa mfanyabiashara mkubwa wa maua nyanda za juu kusini,” anasema Sanga.

Maua ya asili (fresh flowers) yamekuwa yakitumika katika shughuli mbalimbali ikiwemo sherehe, misiba na kupeana zawadi kwa sababu watumiaji wanaamini yanabeba ujumbe wenye hisia.

Pia yanatumika kutengenezea marashi ya aina mbalimbali zikiwemo pafyumu.

Maua aliyokuwa analima Reminus Sanga wilayani Kilolo yakiwa yamewekwa kwenye ndoa katika maonyesho ya Nane Nane mwaka 2017. Picha| Reminus Sanga.

Anguko la biashara ya maua siyo tu limesababisha Sanga na wafanyakazi wake kukosa ajira, pia limeawaathiri wafanyabiashara wadogo mkoani hapa waliokuwa wakinunua na kuuza maua hayo kwa wateja wao kutoka kwake.

Miongoni mwa wafanyabiashara hao wa Iringa ni Veronica John aliyekuwa akinunua maua hayo na kuwauzia wateja wake kwa ajili ya harusi, sherehe za kuzaliwa na kupeana zawadi kwa wapendanao.

“Ilikuwa biashara inayoniweka mjini maana nilikuwa sikosi fedha ya kujikimu lakini sasa maisha yangu yanayumba,” anasema Veronica ambaye alikuwa akipata faida ya kati ya Sh5,000 hadi Sh10,000 kwa siku kutokana kuuza maua hayo. 

Kwa mujibu wa Kitabu Cha Hali ya Uchumi wa Taifa kwa mwaka 2020 kilichotolewa hivi karibuni na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), uzalishaji wa maua nchini Tanzania umeshuka zaidi ya mara saba hadi tani 1,710 mwaka 2020 kutoka tani 13,240 mwaka juzi.

Hilo ni sawa na angulo la asilimia 87.1 ndani ya kipindi cha mwaka mmoja.

“Upungufu huo ulitokana na kushuka kwa uhitaji wa maua kwenye soko la dunia kulikosababishwa na athari za UVIKO-19,” imeeleza sehemu ya kitabu hicho.

Kufungwa kwa shamba la Sanga kumesababisha wapambaji katika mkoa huu kuagiza maua kutokea Arusha jambo linaloongeza gharama ya biashara kutokana na bei kubwa inayojumuisha usafiri. 

Mjasiriamali Mercy Mshana anayefanya shughuli za kupamba kumbi za sherehe mkoani hapa anasema kwa sasa ameamua kutumia maua ya bandia/plastiki (artificial flowers) kutokana na kuadimika kwa maua asilia.

“Mimi hua nalazimika kuagiza maua (asilia) kutoka Arusha kwa sababu huko wako baadhi ya wakulima wanaendelea kulima,” anasema Mshana.

Shamba la maua la mkulima huyo lilikuwa miongoni mwa mashamba machache yanayomilikiwa na vijana wajasiriamali nyanda za juu kusini ukiachana mashamba makubwa yanayopatikana katika Hifadhi ya Taifa ya Kitulo (Nyumba ya Mungu) ambayo yanatumika kwa shughuli za utalii.

Ili kupunguza makali ya maisha, Sanga amehamia Arusha kwa ajili ya shughuli zingine za kilimo, licha ya kuwa hutembelea Iringa mara moja moja.

Kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Kazi Duniani (ILO) kuhusu ajira iliyotolewa Aprili mwaka huu , watu milioni 114 walipoteza ajira zao mwaka 2020 kutokana na shughuli zao kuathiriwa na janga la Uviko-19.

Hata hivyo, ILO inaeleza kuwa kuna matumaini ya soko la ajira kutengemaa tena mwaka huu kutokana hatua mbalimbali zinazochukuliwa kutokomeza ugonjwa huo ikiwemo utoaji wa chanjo na programu zilizobuniwa duniani za kuwawezesha kifedha watu wa makundi mbalimbali wakiwemo vijana.

Licha Sanga bado ana matumaini makubwa ya kufungua upya shamba lake la maua endapo upepo wa Uviko-19 utakapotulia.

Licha ya biashara ya maua asilia kuathiriwa na Uviko-19 mwaka jana, biashara hiyo imeanza kurejea taratibu, jambo linatoa matumaini kwa wakulima kuanza kupata soko la ndani la kimataifa. Picha| Mtandao.

Suluhu kwa wakulima, wafanyabiashara

Licha ya kuwa shughuli za usafirishaji bidhaa zimeanza kurejea duniani, wafanyabiashara wa maua wametakiwa kuangazia matumizi ya mifumo ya biashara mtandaoni (e-commerce) ili kuyafikia masoko yao.

Benki ya Dunia katika andiko lake la jinsi wakulima wavyoweza kujikwamua wakati wa Uviko-19 la May 2021, imeeleza kuwa Serikali na taasisi binafsi zikiwemo benki zitengeneze mfumo utakaorahisisha mnyororo wa thamani wa mazao ikiwemo biashara ya maua.

“Sera zitengenezwe kuvutia na kuwafunza wabunifu wa teknolojia na masoko kufanya kazi na vyama vya wakulima. 

Hawa watu wanaweza kuleta mabadiliko kwa wazalishaji na kuimarisha mnyororo wa thamani wa mazao,” inaeleza sehemu ya andiko hilo la Benki ya Dunia.

Makala hii imeandaliwa kwa ushirika na Shirika la maendeleo ya habari la International Media Support (IMS) na Umoja wa Ulaya (EU). 

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW