Corona ilivyochangia kuyumba kwa bei ya dhahabu Tanzania
- Imeshuka kutoka Sh120,000 kwa gramu moja hadi Sh90,000.
- Kufungwa kwa migodi na kuyumba kwa soko kwachangia.
- Utoaji chanjo ya Uviko-19 unaweza kuimarisha biashara ya madini.
Mwanza. Mgodi wa Stamico uliopo kijiji cha Nyarugusu, Wilaya ya Mbogwe mkoani Geita ni miongoni mwa migodi maarufu nchini unaowakutanisha wachimbaji wadogo wadogo wa madini ya dhahabu.
Licha ya kuwa mgodi huo ambao uko kata ya Nyakafuru wilayani hapa kuwa sehemu muhimu ya vijana kujipatia kipato, shughuli zake hazikubaki salama tangu janga la Corona (Uviko-19) lilipoingia Tanzania Machi mwaka jana.
Ugonjwa huo ambao hauna dawa ulivuruga sekta mbalimbali ikiwemo ya madini duniani ikiwemo Tanzania na hivyo kushuhudia kushuka kwa shughuli na masoko ya madini hasa ya dhahabu.
Wachimbaji wadogo wadogo na wafanyabiashara wa dhahabu wa mgodi huo waliathirika kiasi cha baadhi yao kufunga shughuli zao wakisubiri kurejea kwa hali ya kawaida.
Wachimbaji wadogo wadogo katika mgodi huo wa Stamico walioongea na Nukta Habari (www.nukta.co.tz) wanasema hawatasahau walivyopitishwa kwenye ‘tanuru la moto’ kutokana kuyumba kwa biashara ya madini tangu mwaka 2020.
Shughuli za uzalishaji zilidorora, wawekezaji katika baadhi ya maduara (mashimo) yaliyopo mgodini hapo waliondoka na kuyaacha wazi.
Mgodi huo una jumla ya maduara 300 ambayo kabla ya ugonjwa huo yalikuwa yanafanya kazi, lakini sasa ni maduara 50 tu ndiyo wachimbaji wanayotumia kuchimba dhahabu.
Kabla ya kuingia kwa Uviko-19 mgodi huo ulikuwa na wachimbaji zaidi ya 4,000 lakini sasa nusu yao hawapo tena mgodini hapo baada ya shughuli za uchimbaji kupungua.
“Ugonjwa umeathiri shughuli za uchimbaji, maduara hayana wawekezaji na hata wafanyakazi walikimbia wakiogopa kuambukizwa ugonjwa huo na baadhi ya wawekezaji waliogopa kuwa bei ya dhahabu huenda ikaporomoka,” anasema Venance Kalamu, mwekezaji wa duara mojawapo lililopo mgodini hapo.
Wachimbaji wadogo wa dhahabu katika mgodi wa Chitongo wilayani Misungwi wakiendelea na shughuli ya kupiga rora ili kuvuta mfuko wa mchanga wa dhahabu ambao unachimbwa ndani ya shimo. Picha | Mariam John.
Kalamu anasema kabla ya ugonjwa huo, wafanyakazi ndani ya duara moja walikuwa wanaingia zaidi ya 20 kwa kupokezana, lakini sasa nguvu kazi imepungua ambapo duara moja linaweza kuwa na wafanyakazi sita ambao wanafanya kazi muda mrefu.
Kutokana na nguvu kazi kupungua imesababisha pia uzalishaji mchanga wa dhahabu kupungua kutoka mifuko 100 iliyokuwa inazalishwa ndani ya siku tatu ambapo kwa sasa mifuko hiyo inazalishwa kwa muda wa wiki mbili na kuendelea.
‘Migodi mingine haijabaki salama’
Kilio cha wachimbaji wa madini wa Nyarugusu pia kimewapata wachimbaji wadogo wadogo na wawakezaji katika mgodi wa Chitongo-Ishokela hela wilayani Misungwi, Mkoa wa Mwanza.
Huko nako baadhi ya wawekezaji walikimbia baada ya nguvukazi kupungua na hivyo kuhofia kupata hasara.
Mpaka sasa, wachimbaji hawana tumaini kama wawekezaji hao watarudi tena kuendeleza shughuli zao kutokana na ugonjwa huo kutoonyesha dalili za kutokomezwa katika siku za hivi karibuni licha ya juhudi za utoaji chanjo.
Kabla ya Uviko-19, mgodi huo uliopo kijiji cha Buhunda ulikuwa na zaidi ya wachimbaji 300 lakini sasa wamebaki nusu ya wachimbaji waliokuwepo awali wakihofia madhara ya ugonjwa huo.
Awali kulikuwa maduara 16 yaliyokuwa yanafanya kazi lakini sasa ni maduara nane tu ndiyo yanaendelea na uzalishaji.
“Tunazalisha mifuko 50 (ya udongo wa dhahabu) kwa mwezi na hii ni kutokana na nguvu kazi kupungua kutokana na janga hili la Corona,” anasema Shikombe Shikao, mwekezaji katika mgodi wa Chitongo.
Shikao anasema hali hiyo imechangia uchumi wao kushuka kutokana na uzalishaji hafifu uliosababishwa na janga hilo la Uviko-19.
Bei ya dhahabu yashuka
Kutokana kupungua kwa shughuli za uchimbaji kulikosababishwa na kufungwa kwa mipaka, kuliathiri hata bei ya madini yakiwemo dhahabu.
Bei hizo za dhahabu zimeshuka katika migodi yote miwili ambayo Nukta Habari (www.nukta.co.tz) ilitembelea ambapo kwa sasa gramu moja ya madini hayo inauzwa kwa Sh90,000 kutoka Sh120,000 iliyokuwa inatumika awali.
Hiyo ni sawa kusema wachimbaji wanapoteza Sh30,000 kwa kila gramu moja ya dhahabu wanayouza ikilinganishwa na bei ya awali.
“Bei hii ni kutokana na mipaka mingi kufungwa hivyo wazalishaji wakazalisha dhahabu kwa wingi lakini haikuweza kutoka nchini kwenda nchini China ambako ndiyo wanunuzi wakubwa wa dhahabu ya hapa nchini,” anasema Thobias Moris, Mkurugenzi wa mgodi wa Chitongo.
Shughuli kusafisha vipande vya dhahabu ikiendelea baada kuchimbwa ndani ya shimo katika mgodi wa Stamico mkoani Geita. Picha| Mariam John.
Ugonjwa huo pia umegusa maisha ya wafanyabiashara ambao walikuwa wananunua madini na kuyauza nje ya nchi ambapo nao wanalalamika kuwa bei imeshuka.
Mwenyekiti wa wafanyabaishara katika soko la dhahabu la Geita, Stumaini Ngarama anasema baada ya ugonjwa huo kuingia nchini shughuli za ununuzi na uuzaji wa dhahabu nje ya nchi zilisimama na kusababisha hasara kwa wafanyabiashara.
Anasema kipindi hicho mipaka kwenye nchi zinazonunua dhahabu ilikuwa imefungwa na wafanyabaishara hawakuruhusiwa kupeleka mizigo.
“Athari zilizonekana, mzunguko wa fedha kwenye sekta hii ulikuwa mdogo kwa kuwa hakukuwa na mzigo uliotoka kwenda nchini Dubai kwa ajili ya kuuza,” anasema Ngarama na kubainisha walioathirika zaidi ni wale ambao walinunua mzigo mkubwa wa dhahabu.
Kitabu cha Hali ya Uchumi wa Taifa kwa mwaka 2020, kinaeleza kuwa wawekezaji wengi walinunua madini hayo na kuyahifadhi kama akiba benki ili kunusuru thamani ya fedha zao kutoka katika masoko ya fedha na mitaji ambayo mengi yaliporomoka katika kipindi cha mlipuko wa Uviko-19.

Matumaini yaanza kuonekana
Licha ya maumivu ya zaidi ya mwaka mmoja waliyopata wachimbaji na wawekezaji katika mgodi huo, shughuli za uchimbaji katika migodi hiyo zimeanza kuimarika, jambo linalowapa matumaini kuwa wataanza kufaidika tena na shughuli hizo.
Hiyo inatokana na hatua mbalimbali zilizochukuliwa za kupambana na ugonjwa wa Uviko-19 ikiwemo kuanza kutolewa kwa chanjo na kufunguliwa kwa mipaka ya nchi mbalimbali na kuruhusu usafirishaji wa watu na bidhaa.
Mwenyekiti wa wafanyabaishara katika soko la dhahabu la Geita, Stumaini Ngarama anasema angalau kwa sasa kuna ustahimilivu wa masoko ya dhahabu baada ya chanjo kuanza kutolewa na hivyo wafanyabiashara kuanza kusafiri ili kuuza madini nje ya nchi.
Ngarama anasema hatua hizo zitasaidia wawekezaji kurudi migodini na hivyo kuongeza uzalishaji na bei ya dhahabu.
Waziri wa Madini, Doto Biteko katika hutuba ya bajeti ya wizara yake kwa mwaka 2021/22 alisema wataendelea kuboresha maslahi ya wachimbaji wadogo wa madini ili kukabiliana na changamoto mbalimbali ikiwemo Uviko-19.
Alisema hatua ambazo Serikali inachukua ni kuhakikisha bei ya madini yakiwemo dhahabu inaimarika kupitia uuzaji katika vituo vya madini vilivyopo maeneo mbalimbali nchini.
Makala hii imefadhiliwa na Shirika la maendeleo ya habari la International Media Support (IMS) na Umoja wa Ulaya (EU).
Latest