Sababu uzalishaji wa almasi kushuka Tanzania

January 19, 2022 7:31 am · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link
  • Uzalishaji wa madini hayo umekuwa ukishuka mfululizo tangu 2018.
  • Wadau wamesema hali hiyo imechangiwa na ugonjwa wa Corona.
  • Matumaini yapo mwaka huu baada ya vikwazo vya safari kuondolewa.

Dar es Salaam. Mchango wa sekta ya madini nchini upo wazi. Sekta hiyo imeendelea kuchangia pato la Taifa kwa uchimbaji na biashara ya madini ikiwemo almasi, dhahabu na tanzanite.

Mbali na pato la Taifa, sekta hiyo pia ina mchango mwingine katika kuwapatia Watanzania ajira zikiwemo za migodi mikubwa, ofisini na ajira binafsi kwa wachimbaji wadogo wadogo.

Taarifa ya uchumi wa Taifa iliyotolewa na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba inaeleza kuwa, sekta ya madini na mawe itachangia Pato la Taifa (GDP) kwa takriban asilimia 4.8 kwa mwaka 2021/22.

Licha ya mchango wa sekta hiyo, katika kipindi cha miaka mitano iliyopita baadhi ya madini uzalishaji wake yakiwemo madini ya almasi umekuwa ukishuka mfululizo. 

Kwa mujibu wa Ripoti ya Dondoo za bidhaa za ndani ya nchi za robo ya tatu ya mwaka 2021(Highlights on the Third Quarter GDP (July – September 2021) iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), uzalishaji wa madini ya almasi nchini umekuwa ukiporomoka mfululizo kwa miaka minne iliyopita tangu mwaka 2018.

Mwaka 2017 uzalishaji ulikuwa wakia 88,943 ukashuka hadi wakia 80,509 mwaka 2018 kabla hujashuka zaidi mwaka ulofuata hadi wakia 56,682 mwaka 2019 ikiwa ni mdondoko wa asilimia 29.5.

Uzalishaji wa almasi uliendelea kushuka hata mwaka 2020 hadi wakia 35,243 Na ukashuka zaidi hadi wakia 19,418  mwaka jana.

Ikilinganishwa na madini mengine yanayozalishwa nchini ikiwemo dhahabu, chokaa, chumvi na makaa ya mawe, ni almasi pekee ambayo uzalishaji wake umeshuka mfululizo.

Mathalan,  dhahabu, uzalishaji wake umekuwa ukipanda kuanzia mwaka 2018 ambapo uzalishaji ulikuwa kilogramu (kg) 10,144 na kupanda hadi kg 14,915 mwaka jana.

Mhandisi wa Migodi ambaye alikuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Madini la Taifa (Stamico), Mhandisi Edwin Ngonyani ameiambia Nukta Habari (www.nukta.co.tz)  kuwa tofauti na dhahabu, madini ya vito kama almasi na tanzanite ni madini ya anasa na mapambo.

Watu huyanunua kwa ajili ya kujipamba kwa vitu kama saa, hereni, mikufu na urembo mwingine.

Corona yachangia kushusha uzalishaji wa almasi

Kushuka kwa uzalishaji kwa uzalishaji wa madini hayo kumechangiwa na mlipuko wa janga la Corona (Uviko-19) ambalo lilisababisha zuio la safari za watalii ambao ndiyo wateja wa madini hayo.

“Vito huchukuliwa kama anasa hivyo kipindi cha corona watu walikuwa wanatumia fedha zao kwenye vitu muhimu tu. Hiyo imesababisha soko la vito kukosekana na hata bei yake kushuka,” amesema Mhandisi Ngonyani.


Soma zaidi


Tumaini lipo

Kwa sasa, safari za kimataifa zimerejea japo kwa masharti kadhaa, hivyo utalii nao umeanza kurudi mahala pake. Jambo hilo huenda likawa matumaini kwa wafanyabiashara na wachimbaji  kuongeza uzalishaji wa madini hayo ili kujipatia kipato.

Afisa Mawasiliano na Uchechemuzi kutoka Shirika la Hakirasilimali, Lucy Shao amesema kuwa kuongezeka kwa uzalishaji wa madini mengine ikiwemo dhahabu ni kwa sababu ya thamani na matumizi yake.

Shao amesema, baadhi ya watu hutumia dhahabu kama njia ya uhifadhi wa mali zao katika kipindi cha majanga ikiwemo Corona.

Amesema hata nchi nyingine ikiwemo Marekani, katika kipindi cha majanga ya kitaifa, matajiri hununua dhahabu na kisha kuzihifadhi na baadaye kuziuza pale hali inapokuwa shwari.

Hilo huenda ni sababu ya uzalishaji wa dhahabu kuendelea kukua licha ya ugonjwa wa Corona ambao ulishusha uzalishaji wa madini mengine kama almasi.

“Kwa sasa watalii wameanza kuja nchini na safari za kimataifa zinafanyika hivyo tumaini la soko kwa madini hayo lipo,” amesema Shao.

Follow us on TikTok

Nukta Habari

FOLLOW NOW
Subscribe to our channel

Nukta TV

SUBSCRIBE NOW
Rais Samia azindua minara 758, aacha maagizo mazito juu ya mkongo wa taifa

Rais Samia azindua minara 758, aacha maagizo mazito juu ya mkongo wa taifa

Nukta TV

JAJI MKUU: Njia za asili ni mojawapo ya njia halali za utatuzi wa migogoro

JAJI MKUU: Njia za asili ni mojawapo ya njia halali za utatuzi wa migogoro

Nukta TV

Hesabu ya bosi, bei ya mafuta pasua kichwa madereva wa daladala

Hesabu ya bosi, bei ya mafuta pasua kichwa madereva wa daladala

Nukta TV