Zaidi ya chanjo 900,000 kupambana na polio Mwanza
- Watoto zaidi ya 846,733 watapata chanjo ya polio mkoani humo.
- Chanjo 973,740 zimeandaliwa katika mkoa huo.
Mwanza. Zaidi ya Watoto 846,733 wenye umri kati ya miaka 0 hadi mitano wanatarajiwa kupatiwa chanjo ya ugonjwa wa kupooza (polio) mkoani Mwanza ili kuwalinda dhidi ya ugonjwa huo ambao umeripotiwa kusambaa katika nchi jirani za Afrika Mashariki.
Ili kupambana na ugonjwa huo, chanjo 973,740 zimeandaliwa katika mkoa huo.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Robert Gabriel amewataka wananchi kuwa mabalozi wazuri wa kuhamasisha zoezi hilo ili watoto wote wapate chanjo hiyo.
Chanjo hiyo itafanyika kwa siku nne ambapo itatolewa kwenye maeneo tofauti ikiwemo nyumba kwa nyumba, vituo vya afya, sokoni, stendi za mabasi na kwenye maeneo ya mikusanyiko huku kauli mbiu katika kampeni hiyo ya polio ni ‘kila tone la polio litaiweka Tanzania salama dhidi ya ugonjwa wa kupooza’
Ugonjwa wa polio huaathiri mfumo wa neva na huweza kusababisha udhaifu wa misuli au kupooza, ambayyo ni kushindwa kusogeza misuli. Ugonjwa huu ni adimu, kwa kuwa chanjo imepunguza uwepo wa virusi hivi katika nchi nyingi.
Polio hutokea zaidi kwa watoto wenye umri chini ya miaka 5. Watu ambao bado hawajapata chanjo wapo kwenye hatari ya kuambukizwa.
Akizungumza kwenye uzinduzi wa kutoa chanjo hiyo leo Mei 18 uliofanyika katika Zahanati ya Mkolani jijini Mwanza, Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Amina Makilagi amekemea upotoshaji unaotolewa na baadhi ya wananchi kuhusu chanjo hiyo.
Amesema ipo imani potofu inayoenezwa na baadhi ya watu kuwa chanjo hiyo siyo nzuri inasababisha madhara kwa watoto kuwa siyo sahihi kwa kuwa chanjo hiyo si mara ya kwanza kutolewa Tanzania.
Soma zaidi
Amesema tafiti za kitaalamu zinabainisha kuwa ugonjwa huo unaweza kumpata mtu yeyote hasa watoto kwa kuwa virusi vya polio humwingilia mtu mwilini kupitia chakula au maji au vitu mbalimbali vinavyoweza kuingia mwilini ambavyo vimechafuliwa na virusi hao.
“Nitoe rai kwa wananchi kutosikiliza maneno ya watu wanaopotosha kuhusiana na suala hili la chanjo kutowasikiliza kwa kuwa chanjo hii si ya kwanza kutolewa hapa nchini na kwamba miaka ya nyuma iliwahi kutolewa baada ya kuzuka kwa ugonjwa huo,” amesema Makilagi.
Amesema lengo la kutoa chanjo hiyo ni kuwakinga watoto wote wasiambukizwe na ugonjwa huo ulioibuka katika nchi ya jirani na kwamba kampeni hiyo itafanyika kwa siku nne, na itapatikana maeneo tofauti.
Dalili za polio huweza kujumuisha homa, koo kuuma, maumivu ya kichwa na misuli kuuma. Baadhi ya watu hupata udhaifu wa misuli. Matokeo baada ya maambikizi ya polio hutegemea dalili ni kali kiasi gani. Inaweza kusababisha ulemavu wa kudumu na kifo.
Awali Mganga Mkuu wa Jiji la Mwanza, Sebastian Pima amesema wameshatoa maelekezo kwa viongozi wa serikali za mtaa na watendaji ili kuwaandaa wananchi wajitokeze kwenda kupatiwa chanjo lakini pia watalaam wa afya wapo tayari kupita nyumba kwa nyumba kwa ajili ya kufanikisha zoezi hilo.
Amesema hawatarajii madhara yoyote kutokea kwa watoto kwakuwa chanjo hiyo ni salama.
“Kwa mara ya kwanza tumepata matokeo mazuri ya wazazi kujitokeza kupata chanjo ya polio, watu wamejitokeza kwa wingi na kwamba niendelee kuwaomba wananchi waendelee kutoa ushirikiano na kujitokeza ili zoezi hili liweze kufanikiwa,” amesema Pima.
Baadhi ya wananchi waliozungumza na Nukta Habari wamesema wapo baadhi ya watu wanagoma kuwapeleka watoto wao kupata chanjo hiyo wakiamini kuwa inaweza kuleta madhara
Zuena Zuberi ni mmoja wa wazazi ambaye mtoto wake amefanikiwa kupatiwa chanjo anasema kampeni ya nyumba kwa nyumba itasaidia zoezi hilo kwakuwa kabla ya kutoa chanjo watalazimika kutoa elimu.
“Mimi nadhani kampeni ya nyumba kwa nyumba itakuwa na matokeo chanya kwakuwa wananchi watapatiwa elimu kwanza kabla ya Watoto wao kuchanjwa hali itakayosaidia kuondoa hizo dhana potofu,” amesema Zuena.
Kwa mujibu wa Wizara ya Afya, watoto milioni 10.3 wanatarajiwa kufikiwa Tanzania Bara na Zanzibar kwa awamu hii ya pili ambapo awamu ya kwanza iliyofanyika katika mikoa ya Njombe,Mbeya, Ruvuma na Songwe waliwafikia watoto 1,138,949 kati ya 983,542 waliokusudiwa.
“Hatutakubali kuona watu wachache kwa maslahi yao wakiiweka Tanzania hatarini kwa ugonjwa wa Polio,Vyombo vya usalama wachukulieni hatua wale wote wanaosambaza taarifa za uzushi na kupotosha jamii kuhusu chanjo,chanjo hizi ni salama,” amesema Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu katika uzinduzi wa kampeni ya kutoa chanjo ya matone ya Polio kwenye viwanja vya Chinangali jijini Dodoma.
Latest
