CCM yatoa ratiba mpya ya uteuzi wa watia nia wa ubunge, uwakilishi na udiwani
- Majina ya wagombea kujulikana rasmi Agosti 22.
Dar es Salaam. Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimetoa ratiba mpya ya vikao vya uteuzi wa watia nia wa nafasi za ubunge, uwakilishi na udiwani ili kufanikisha mchakato wa kuwapata wagombea.
Hii ni baada ya mabadiliko ya ratiba yaliotangazwa Julai 19, 2025 kupitia kwa Katibu wa Halmashauri Kuu, Itikadi Uenezi na Mafunzo ACP Amos Makalla, ambapo alieleza sababu ya mababadiliko ni kuwepo kwa idadi kubwa ya majina ya watiania.
Kwa mujibu wa ratiba hiyo iliyotangazwa Julai 22, mchakato wa uteuzi utaanza Julai 27 kwa kikao cha Kamati ya Usalama na Maadili ya Taifa, kitakachofuatiwa na kikao cha Kamati Kuu ya CCM Julai 28, ambacho kitaamua majina ya watia nia wa ubunge na uwakilishi wasiozidi watatu kwa kila jimbo.
Julai 30, mikutano ya UWT mikoa itafanyika kwa ajili ya kupiga kura ya maoni kwa wagombea wa ubunge wa viti maalum, huku Agosti 1 kukiwa na mkutano wa UVCCM Taifa kwa kura za viti maalum vya vijana kwa Tanzania Bara na Zanzibar.
Mkutano Mkuu Maalum wa UWT Taifa utafanyika Agosti 2 kupitisha kura za wagombea wa viti maalum wa makundi.
Kati ya Julai 30 hadi Agosti 3, wagombea watajitambulisha katika Kata/Wadi na Majimbo yao.
Agosti 4 kutafanyika mikutano ya kupiga kura za maoni kwa wagombea wa ubunge, uwakilishi na udiwani.
Mikutano ya kamati mbalimbali za siasa kuanzia kata hadi mkoa itafanyika kati ya Agosti 5 hadi Agosti 11, kwa ajili ya kuchuja na kupendekeza majina ya wagombea kwa ngazi za juu.
Agosti 13, Halmashauri Kuu za CCM za mikoa zitafanya uteuzi wa mwisho wa wagombea udiwani mmoja kwa kila Kata/Wadi, na Agosti 15, Kamati ya Utekelezaji ya UWT Taifa itajadili wagombea wa viti maalum kwa makundi mbalimbali.
Maandalizi ya vikao vya uteuzi wa mwisho yataendelea Agosti 16 hadi 20 kupitia vikao vya sekretarieti na kamati maalum, kabla ya kufikia kilele cha uteuzi Agosti 22 ambapo Halmashauri Kuu ya CCM Taifa itafanya uteuzi wa mwisho wa majina ya wagombea wa ubunge na uwakilishi wa majimbo pamoja na viti maalum.
Latest



