CCM kutumia ‘QR code’ kukabiliana na taarifa za uongo
- Lengo ni kuwezesha wananchi kuhakiki taarifa rasmi moja kwa moja kutoka kwenye vyanzo vya chama
Dar es Salaam. Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimesema kimeanza rasmi kutumia msimbo ‘QR code’ katika taarifa zake kwa umma, hatua inayolenga kukabiliana na ongezeko la taarifa potofu.
Msimbo ni alama, mchoro, tarakimu au herufi, inayoandikwa na kutumiwa kuwakilisha dhana au jambo fulani.
Kwa mujibu wa taarifa ya Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa anayeshughulikia Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Amos Makalla iliyotolewa leo Julai 21, imebainisha kuwa teknolojia hiyo itarahisisha uthibitishaji wa taarifa kwa wananchi, na kusaidia kudhibiti upotoshaji unaolenga kudhoofisha hadhi ya chama hicho.
“Uhakiki unaweza kufanyika kwa ‘ku-scan’ nembo ya QR Code. Mara moja, msomaji ataelekezwa kwenye taarifa rasmi iliyochapishwa na CCM kupitia tovuti au mitandao yake ya kijamii,” imesema taarifa ya Makalla.
Makalla amefafanua kuwa taarifa yoyote ya uongo, iliyotungwa na watu wenye nia ovu, haitakuwa na QR code itakayompeleka msomaji kwenye chanzo halisi, hivyo kumuwezesha kujua taarifa halali na zile zilizopotoshwa.
Mfano wa taarifa ya kupotosha
Makalla ametoa mfano wa tukio la hivi karibuni lililotokea Julai 20, 2025, ambapo ilienea taarifa iliyodai kuwa CCM imetoa rambirambi kwa ajali iliyotokea Iwambi, Mbeya.
Hata hivyo, kwa kufanya ‘scan’ ya QR code iliyowekwa kwenye taarifa halali ya chama, msomaji alikumbana na kichwa cha habari kilichoandikwa: “CCM YATOA RAMBIRAMBI KWA AJALI GARI IWAMBI, MBEYA,” jambo linalodhihirisha kuwa taarifa hiyo ya awali haikuwa sahihi.
Kwa mujibu wa Makalla, hatua hiyo ni sehemu ya jitihada za chama kulinda uaminifu wa wananchi dhidi ya wimbi la habari potofu linaloshuhudiwa mitandaoni kwa siku za hivi karibuni kuelekea uchaguzi mkuu wa madiwani, wabunge na Rais.
Hata hivyo, wadau mbalimbali ikiwemo Nuktta Fakti wamekuwa wakitoa elimu kwa umma juu ya namna ya kubaini na mbinuza kukabiliana na habari hizo.
CCM imewahimiza Watanzania na wapenzi wa chama hicho kuwa makini na taarifa wanazozipokea, na kutumia QR code zilizowekwa ili kuhakiki uhalali wake kabla ya kuzisambaza.
Latest



