CCM yaahidi uwanja wa ndege, kongani ya viwanda Singida
Samia asema uwanja wa ndege utafungua fursa za kibiashara na ajira.
Dar es Salaam. Mgombea urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan, ameahidi ujenzi wa viwanda pamoja na uwanja wa ndege mkoani Singida endapo chama chake kitapata ridhaa ya kuendelea kuongoza nchi kwa miaka mitano ijayo.
Akihutubia wananchi wa Singida Mjini leo Septemba 9,2025, Samia amesema hatua hiyo inalenga kufungua fursa mpya za kiuchumi na kibiashara kwa Wananchi wa mkoa huo, sambamba na kuongeza ajira kupitia uwekezaji wa viwanda.
“Mkoa wa Singida mwaka 2020 ulikuwa na kiwanda kimoja kikubwa pekee, hadi sasa tumefikia viwanda tisa, kati ya hivyo sita vipo Singida Manispaa.
Tunapokwenda mbele, tumejipanga kuendeleza kongani za viwanda katika wilaya mbalimbali ili kuongeza thamani ya mazao yanayolimwa na kuvunwa Singida, na hivyo kutengeneza ajira kwa vijana wetu,” amesema Samia.
Huenda ahadi hizo zikakuza pato la mkoa huo ambao Kitabu cha Takwimu za Msingi za Tanzania kwa mwaka 2024 (Tanzania in Figures ) kinautaja kuwa miongoni mwa mikoa maskini ikiwa na pato la Sh1.7 milioni kwa mwaka.
Aidha, Samia amesisitiza kuwa kukamilika kwa mradi wa reli ya kisasa (SGR) na uwepo wa uwanja wa ndege wa kimataifa wa Msalato mkoani Dodoma kunatoa fursa kubwa za kibiashara, na kuongeza kuwa Singida nayo inapaswa kuwa sehemu ya maendeleo hayo.
Samia amewaomba wananchi wa Singida kutumia vyema fursa zinazojitokeza ili kuinua hali zao kiuchumi huku Serikali ikiendelea kuweka mazingira bora ya uwekezaji.
Katika hotuba yake, amesisitiza kuwa mafanikio yaliyopatikana chini ya Serikali ya CCM ni matokeo ya usimamizi wa chama hicho pamoja na watumishi wa umma wanaotekeleza miradi ya maendeleo kwa wananchi.
“Serikali ya CCM imekuwa ikikagua miradi inayotekelezwa. Pale ambapo haturidhiki, tunasema wazi. Hii ni kwa sababu chama kipo karibu na wananchi na kinasimamia ipasavyo Serikali yake,” ameongeza mgombea huyo.
Akihitimisha hutuba yake Samia amewataka wananchi wa Singida kuendelea kuiamini CCM ili kutekeleza miradi iliyopangwa kwenye ilani ya uchaguzi wa chama hicho kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.
Latest



