Si kweli: Rais Ibrahim Traore anajenga nyumba za bure Burknafaso

May 9, 2025 1:28 pm · Kelvin Makwinya
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni  miradi ya ujenzi wa makazi ya kisasa inayoendelea nchini Algeria, hasa katika miji mipya ya Boughezoul na Sidi Abdallah.

Dar es Salaam. Katika siku za hivi karibuni kuna taarifa zinasamba kwenye mitandao ya kijamii zikidai kuwa Rais wa Burkina Faso, Ibrahim Traoré, amejenga nyumba za bure kwa ajili ya wananchi wake kama sehemu ya juhudi za kuleta maendeleo nchini humo, taarifa hizo si za kweli.

Video na picha kuhusu taarifa hizo zimekuwa zikisambaa kwa kasi kwenye mitandao ya kijamii kama Facebook na X (zamani Twitter), zikiibua hisia na mjadala mkubwa miongoni mwa watumiaji.

Hata hivyo, uchunguzi uliofanywa na Nukta Fakti umebaini kuwa madai hayo si ya kweli. Video hizo hazihusiani na Burkina Faso bali zinahusu miradi ya ujenzi wa makazi ya kisasa inayoendelea nchini Algeria, hasa katika miji mipya ya Boughezoul na Sidi Abdallah.

Uchambuzi wa picha na video hizo umebaini kuwa ni vipande kutoka kwenye makala zilizotolewa na mashirika ya habari ya kimataifa kama Africa News na Euronews, zilizochapishwa Disemba 5, 2022.

Kwa mujibu wa ripoti ya Cyril Fourneris wa Africa News, mji wa Boughezoul  uliopo takribani kilomita 170 kusini mwa mji mkuu wa Algiers  unajengwa kwa lengo la kuhifadhi zaidi ya wakazi 400,000, ukiwa na jumla ya hekta 20,000 zilizogawanywa kwa matumizi ya makazi, biashara, na kilimo. 

Mradi huo ni sehemu ya mkakati wa Serikali ya Algeria kupunguza makazi duni, kukuza usawa wa maendeleo na kuwapatia wananchi mazingira bora ya kuishi.

Mji mwingine wa Sidi Abdallah, ulioko ndani ya Algiers, unajengwa kwa misingi ya maendeleo endelevu na matumizi ya teknolojia ya kisasa. 

Serikali ya Algeria imeweka kipaumbele kwenye utoaji wa makazi nafuu, mikopo isiyo na riba, na kupunguza msongamano wa watu mijini.

Video hizo hazihusiani na Burkina Faso bali zinahusu miradi ya ujenzi wa makazi ya kisasa inayoendelea nchini Algeria, hasa katika miji mipya ya Boughezoul na Sidi Abdallah.

Zaidi ya hapo, taarifa rasmi iliyochapishwa kwenye tovuti ya kampuni ya ujenzi ya POWERCHINA tarehe 15 Januari 2025, imethibitisha kuwa mradi mwingine wa ujenzi wa nyumba 1,476 unatekelezwa katika mkoa wa Guelma, kaskazini-mashariki mwa Algeria. 

Mradi huo, unaokaliwa na watu wa kipato cha chini, unajengwa katika eneo lenye ukubwa wa mita za mraba 102,900, na eneo la ujenzi la takriban 155,900 sqm, na tayari umekamilika na kupokelewa vyema na jamii.

Hadi sasa, hakuna ushahidi wowote rasmi kutoka kwa Serikali ya Burkina Faso, vyombo vya habari vya taifa hilo, au taasisi huru yoyote inayothibitisha kuwepo kwa mradi kama huo nchini humo au kuhusika kwa Rais Ibrahim Traoré katika ujenzi wa makazi hayo.

Kwa msingi huo, madai yanayosambazwa mitandaoni kwamba Rais wa Burkina Faso anajenga nyumba za bure kwa wananchi wake si ya kweli, bali ni upotoshaji unaotokana na kuchukua video za miradi ya Algeria na kuzihusisha kimakosa na Burkina Faso.

Nukta Fakti inawahimiza wananchi kuwa makini na kuchunguza ukweli wa taarifa kabla ya kuzisambaza mitandaoni, uhakiki wa taarifa ni muhimu zaidi kuliko kitu chochote.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks