BoT kuondoa noti za zamani kwenye mzunguko Tanzania

October 26, 2024 6:09 pm · Lucy Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni pamoja na noti za Sh20, 200, 500, 1000, 2000, 5000) na 10000 kwa matoleo ya mwaka 1985 hadi mwaka 2003.
  • Matumizi ya noti hizo yatasitishwa Aprili 6, 2024.

Arusha. Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imesema itaziondoa kwenye mzunguko baadhi noti za zamani za Tanzania na kusitisha matumizi yake ifikapo Aprili 6, 2024.

Taarifa ya Gavana wa BOT, Emmanuel Tutuba iliyotolewa leo Oktoba 26, 2024 inafafanua kuwa matoleo ya fedha hizo yatakayoondolewa katika mzunguko ni pamoja na ya mwaka 1985 hadi mwaka 2003 pamoja na baadhi ya 2010.

“…Noti za zamani za shilingi ishirini (20), mia mbili (200), mia tano (500), elfu moja (1000), elfu mbili (2000), elfu tano (5000) na elfu kumi (10000) kwa matoleo ya mwaka 1985 hadi mwaka 2003…

… na noti ya shilingi mia tano (500) iliyotolewa mwaka 2010 zenye sifa zilizoainishwa kwenye Tangazo la Serikali Na. 858 la tarehe 11 Oktoba 2024,” imebainisha taarifa ya Tutuba.

BoT imebainisha kuwa zoezi la hilo  litaanza Januari 6, 2025 hadi Aprili 5, 2025 kupitia ofisi zote za Benki Kuu na benki zote za biashara kwa kupatiwa malipo yenye thamani sawasawa na kiasi kitakachowasilishwa. 

Aidha, matumizi ya noti hizo yatafikia ukomo wa kuwa fedha halali za Tanzania kuanzia tarehe 06 Aprili, 2025 na  baada ya tarehe hiyo, mtu yeyote au taasisi yoyote inayomiliki fedha hizo haitaruhusiwa kuzitumia katika kufanya malipo popote duniani na benki zote hazitaruhusiwa kulipa wala kupokea amana au maombi ya kubadilisha noti zilizoondolewa kwenye mzunguko.

BoT imetoa  rai kwa wananchi wote wenye akiba ya noti hizo za zamani, kuzibadilisha au kuziweka amana kwenye benki yoyote ndani ya kipindi kilichotolewa. 

Kwa taarifa au msaada zaidi BoT imewataka wananchi kuwasiliana na Kurugenzi ya Usimamizi wa Sarafu kupitia sanduku la posta 2939 Dar es Salaam   kwa Barua Pepe info@bot.go.tz  au namba ya simu 0745802007.

Enable Notifications OK No thanks