Sababu BoT kuondoa kwenye mzunguko noti za zamani

October 31, 2024 2:58 pm · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Yasema ni zoezi la kawaida na la kisheria.
  • Yakana madai kuhususisha zoezi hilo na kushuka kwa thamani ya shilingi.
  • Zoezi hilo kuanza Januari 6, 2025.   

Dar es Salaam. Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imesema zoezi la kuondoa noti za zamani kwenye mzunguko wa sarafu linalotarajia kuanza Januari 2025 ni la kawaida na halina uhusiano wowote wa kushuka kwa thamani ya shilingi ya Tanzania.

Oktoba 11, 2024 kupitia tangazo la Serikali namba 858, BoT ilitangaza zoezi la kuondoa kwenye mzunguko noti za zamani za Shilingi 20, 200, 1,000, 5,000 na 10,000 kwa matoleo ya mwaka 1985 hadi 2003. Pia imetangaza kuondoa noti ya Shilingi 500 iliyotolewa mwaka 2010. 

Baada ya tangazo hilo, kumekuwepo na mijadala mbalimbali ndani na nje ya mitandao ya kijamii kuhusu zoezi hilo litakaloanza Januari 6 hadi Aprili 5, 2024.

Baadhi ya watu wamekuwa wakidai kuwa sababu kuu ni kushuka kwa thamani ya sarafu ya shilingi ya Tanzania dhidi ya fedha za kigeni ikiwemo dola ya Marekani. 

Kaimu Mkurugenzi Usimamizi wa Sarafu wa BoT, Ilulu Ilulu amesema madai hayo hayana ukweli wowote kwa sababu shilingi ya Tanzania bado iko imara na ubora wake uko katika kiwango kizuri. 

“Kwa wanaopitia takwimu, kiwango na thamani ya pesa yetu iko pale pale isipokuwa tunachotekeleza ni kuondoa huo utata. Watu wanajiona wanazo hizo noti amekaa nazo lakini hawezi kwenda kununulia,” amesema Ilulu. 

Ilulu amesisitiza kuwa zoezi la kuondoa noti za zamani kwenye mzunguko wa sarafu siyo njia ya kukabiliana na kile ambacho watu wanadai kuwa thamani ya shilingi ya Tanzania imeshuka. 

“Zoezi la namna hii siyo geni nchini kwani mara kadhaa Benki Kuu imetekeleza zoezi la aina hii,” amesema Ilulu mbele ya waandishi wa habari jijini Dar es Salaam na kuongeza huu ni wakati sahihi kuondoa noti hizo ambapo baadhi ya wananchi wamekuwa wakiomba kubadilishiwa. 

Kifungu cha 28 (2) cha Sheria ya Benki Kuu ya Tanzania kinaeleza kuwa benki hiyo imepewa mamlaka kusitisha uhalali wa fedha itakazozianisha kadri itakavyoona inafaa kwa kuchapisha tangazo katika Gazeti la Serikali. 

BoT imeeleza kuwa baada ya Aprili 5, 2024, noti zilizoanishwa hapo juu zitakoma kuwa halali kwa malipo ndani na nje ya Tanzania na zile zitakazokusanywa zitateketezwa. 

Zoezi hilo la kubadilisha noti hizo za zamani litahusisha ukusanyaji wa noti husika kutoka kwa wananchi kupitia ofisi za BoT zilizopo nchini na benki zote za biashara ambapo wananchi watatakiwa kuziwasilisha huko na kupatiwa malipo yenye thamani sawa sawa na kiasi watakachowasilisha. 

Ili kuhakikisha zoezi hilo linafanikiwa, BoT itatoa elimu kwa wananchi kwa njia mbalimbali ikiwemo vyombo vya habari. 

Hii itakuwa mara ya tano kwa BoT kuondoa noti za zamani katika mzunguko wa sarafu. Mara ya kwanza zoezi hilo lilifanyika mwaka 1977 kwa noti ya Shilingi 100 iliyochapishwa kuanzia 1966 hadi 1977. 

Pia iliendesha zoezi hilo tena mwaka 1979 kwa kuondoa uhalali wa noti ya Shilingi 10 na Shilingi 20 zilizochapishwa kati ya mwaka 1966. Mwaka 1980, BoT iliondoa katika mzunguko noti ya Shilingi 5 na Shilingi 20 zilizochapishwa kati ya 1966 hadi 1979.

Zoezi la nne lilifanyika mwaka 1995 ambapo noti ya Shilingi 50 na Shilingi 100 zilizochapishwa kati ya mwaka 1979 hadi 1995 ziliondolewa katika mzunguko.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks