Noti mpya kuanza kutumika Februari Mosi, 2025
- Ni zenye saini ya Mwigulu Nchemba na Tutuba.
- Zitaingizwa kwenye mzunguko na kutumika pamoja na noti zilizopo hivi sasa.
Dar es Salaam. Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Emanuel Tutuba amesema noti mpya za Tanzania zenye saini yake na Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba zitaingia kwenye mzunguko kuanzia Februari Mosi mwaka huu.
Noti hizo zitakazoingizwa sokoni ni zile za toleo la mwaka 2010 zikiwa mbadala wa zile zinazotumika hivi sasa zenye saini ya aliyekuwa Waziri wa Fedha Dk Philip Isdor Mpango ambaye sasa ni Makamu wa Rais wa Tanzania na Profesa Florens Luoga, Gavana mstaafu wa BoT.
Gavana Tutuba aliyekuwa akizungumza wakati akimkabidhi Dk Nchemba, noti kifani za Sh10,000, 5,000, 2,000 na Sh 1,000 katika ofisi ndogo za Wizara ya Fedha, Jijini Dar es Salaam leo Januari 22,2025 amesema noti zitatumika pamoja na zile za awali.
“Noti hizo zitatumika sambamba na noti zilizopo hivi sasa, zinamwonekano wa noti zinazotumika hivi sasa zilizotolewa Mwaka 2010, ikiwemo alama za usalama, ukubwa, rangi na mambo mengine isipokuwa ina marekebisho kwenye saini ya Waziri wa Fedha, na Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania,” amesema Tutuba.

Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba (kushoto), akipokea noti mpya kifani kutoka kwa Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Emmanuel Tutuba, katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Fedha, Jijini Dar es Salaam.
Akizungumza baada ya kupokea sampuli za Noti hizo mpya Dk Nchemba, amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuruhusu jambo hilo kufanyika na kumpongeza Tutuba, kwa kusimamia mchakato wa uchapaji wa noti hizo kwa weledi na uadilifu mkubwa.
“Mpaka kufikia hatua hii ni heshima kubwa kwa Taifa letu na inaendeleza heshima ya wataalamu wetu mnavyoweza kusimamia kwa umakini mambo yenye maslahi mapana kwa nchi yetu,” Ameema Dkt. Nchemba.
Latest



