BoT kununua dhahabu kwa bei ya soko la dunia

October 2, 2024 1:12 pm · Nuzulack Dausen
Share
Tweet
Copy Link
  • Wachimbaji wakubwa na wafanyabiashara wa dhahabu watakaoiuzia benki hiyo madini watapata punguzo la ada litakalopunguza maumivu ya ufanyaji biashara.

Dar es Salaam. Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imesema itanunua dhahabu kutoka kwa wachimbaji wakubwa na wauzaji wa dhahabu nchini kwa bei shindani za soko la dunia na kutoa motisha zitakazosaidia kupunguza maumivu kwa wauzaji hao. 

Katika taarifa iliyotolewa jioni ya Oktoba 1 mwaka huu, BoT imeeleza kuwa mauzo yote ya madini yatakayofanyika baina yake na wauzaji yatatumia bei ya dhahabu duniani ambayo hutolewa kila siku na Tume ya Madini. 

Maelezo hayo ya benki hiyo yanakuja ikiwa ni siku nne tangu Tume ya Madini itangaze kuwa wachimbaji wakubwa na wauzaji wa dhahabu wanaotaka kuuza nje ya nchi  wanatakiwa kutenga asilimia 20 ya madini hayo kwa ajili ya kuiuzia BoT. 

Uamuzi huo ulifanywa na Serikali baada ya kufanyika maboresho katika Sheria ya Madini kufuatia kutungwa kwa Sheria ya Fedha ya mwaka 2024/25. 

Kwa sasa BoT  inaendelea na mpango wake wa kununua dhahabu nchini unaolenga kuongeza hifadhi za fedha za kigeni hususan Dola ya Marekani hasa katika kipindi ambacho Shilingi imekuwa ikipata mashinikizo makubwa kutoka kwa sarafu kubwa duniani. 

Katika mwaka wa fedha wa 2024/25, BoT imepanga kununua tani sita, ikiwa ni mara 15 zaidi ya kilo 418 zilizonunuliwa katika mwaka wa fedha uliopita. 

Benki hiyo imesema itafanya malipo yote ndani ya Saa 24 baada ya kupata ripoti ya uchenjuaji wa dhahabu na kwamba itagharamia gharama zote za kuchenjua madini hayo. 

Miongoni mwa motisha zitakazotolewa na benki hiyo kwa watakaoiuzia asilimia 20 ya dhahabu zao ni punguzo la mrabaha hadi asilimia nne kutoka asilimia sita, kutotozwa ada ya ukaguzi badala ya asilimia moja na kutozwa kodi ya ongezeko la thamani (VAT) kwa asilimia sifuri, fursa inayompa muuzaji kudai rejesho la kodi hiyo maarufu  kwa kimombo kama “input tax’. 

“Chini ya mpango huu, wamiliki wa leseni ya uchimbaji madini, wafanyabiashara wakubwa wa madini na viwanda vya kuchenjulia dhahabu wanaweza kuiuzia benki kuu kiasi chochote cha dhahabu,” imesema taarifa hiyo ya BoT. 

Kutolewa kwa maelezo hayo ya viwango vya ununuzi kutoka BoT angalau kutapunguza hofu miongoni mwa wafanyabiashara na wadau wa madini ambao walikuwa wanahofia huenda benki hiyo ingekuja na bei zake ambazo zisingekuwa rafiki kwa wachimbaji na wauzaji. 

Enable Notifications OK No thanks