Wafanyabiashara madini watakiwa kuuza 20% ya dhahabu BoT

September 28, 2024 1:10 pm · Nuzulack Dausen
Share
Tweet
Copy Link

Ni miongoni mwa hatua za Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan kuimarisha hifadhi ya fedha za kigeni hususan Dola ya Marekani kwa ajili ya matumizi mbalimbali. 


Dar es Salaam. Katika kuimarisha hifadhi ya fedha za kigeni nchini, Tume ya Madini imewataka wachimbaji na wafanyabiashara wakubwa wa dhahabu wanaotaka kuuza bidhaa hiyo nje ya nchi kutenga kiwango kisichopungua asilimia 20 ya madini hayo kwa ajili ya kuiuzia Benki Kuu ya Tanzania (BoT). 

Katika taarifa kwa umma iliyotolewa Ijumaa jioni, tume hiyo imesema utekelezaji wa hatua hiyo utaanza kuanzia Oktoba mosi mwaka huu ikiwa ni utekelezaji wa sheria ya madini baada ya kupitishwa kwa Muswada wa Sheria ya Fedha wa mwaka 2024/25. 

BoT ilianza kununua dhahabu tangu mwaka janakama moja ya hatua za kuimarisha hifadhi za fedha za kigeni na kuongeza upatikanaji wa Dola ya Marekani kwa matumizi mbalimbali ambapo kwa mwaka wa fedha wa 2023/24 ilinununua kilo 418 za dhahabu.

Katika mwaka wa fedha 2024/25 ulioanza Julai 2024, BoT inatarajia kununua tani sita za dhahabu, kiwango ambacho ni kikubwa mara 15 zaidi ya kile kilichonunuliwa mwaka jana. 

Wafanyabiashara hao kwa mujibu wa Kaimu Katibu Mtendaji wa tume hiyo Ramadhan Lwamo watatakiwa kuwasilisha kiasi hicho cha dhahabu katika viwanda vya kusafisha dhahabu (Refineries) vya Eyes of Africa Ltd kilichopo jijini Dodoma na Mwanza Precious Metals Refinery Ltd kinachoendesha shughuli hiyo mkoani Mwanza. 

“Taratibu za malipo zitafanyika kwa mujibu wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT),” imeeleza taarifa hiyo. 

Shilingi ya Tanzania katika miaka ya hivi karibuni imekuwa ikipata shinikizo kutoka kwa sarafu kubwa duniani hususan Dola ya Marekani kutokana na mabadiliko ya kiuchumi katika soko la dunia yakichochewa zaidi na migogoro inayoendelea baina Urusi na Ukraine na Mashariki ya Kati. 

Kwa mujibu wa Ripoti ya mapitio ya uchumi kwa mwezi Agosti 2024 (Monthly Economic Review) ya BoT, hadi Julai mwaka huu Tanzania ilikuwa na hifadhi ya fedha za kigeni Dola za Marekani 5.29 bilioni, kiwango kinachotosha kuingiza bidhaa na huduma kwa miezi 4.3, juu kidogo ya ukomo wa kitaifa wa miezi minne. 

Hata hivyo, kiwango hicho kipo chini kidogo ya ukomo wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wa kuwa na akiba ya fedha za kigeni inayotosha kuingiza bidhaa na huduma kwa miezi isiyopungua 4.5. 

Enable Notifications OK No thanks