Biteko: Tanesco itoe elimu unafuu wa kupika kwa umeme

March 4, 2025 6:41 pm · Fatuma Hussein
Share
Tweet
Copy Link
  • Asema kuna dhana potofu kwa Watanzania kuhusu gharama za umeme kupikia. 

Dar es Salaam. Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dotto Biteko amelitaka Shirika la Umeme Nchini (Tanesco) kuongeza juhudi za kuelimisha umma wa Watanzania kuhusu unafuu wa kupika kwa kutumia nishati ya umeme ili kuokoa fedha, muda, kutunza mazingira na kuepukana na athari za kiafya zitokanazo na nishati chafu.

Kwa mujibu wa Biteko baadhi ya Watanzania wanaamini matumizi ya nishati ya umeme kupikia huwa na gharama kubwa jambo linalosababisha wasalie kutumia nishati chafu ikiwemo kuni na mkaa.

Biteko aliyekuwa akizungumza leo Machi 4, 2025 katika kongamano la kuhamasisha matumizi ya umeme kupikia amesema maendeleo ya teknolojia yamerahisisha upatikanaji wa majiko yanayopika kwa kutumia nishati kidogo ya umeme.

“Tumeambiwa unit moja unaweza ukapika kwa saa moja, ambayo thamani yake haizidi Sh350, maana yake ukitumia mkaa unatumia gharama kubwa zaidi kuliko ambavyo ungetumia umeme. Tuendelee kutoa elimu kwa watu wote kuwa nishati ya umeme inafaa kwa kupikia,” amesema Biteko jijini Dar es Salaam.

Matumizi ya nishati safi ya kupikia ni agenda mahususi ambayo imechukua nafasi kubwa katika Sera, Mipango na Mikakati ya Serikali mbalimbali duniani ikiwemo Tanzania.

Umuhimu wa agenda hiyo unasukumwa na ongezeko la uharibifu wa mazingira na mabadiliko ya tabianchi pamoja na athari za kiafya zinazotokana na matumizi ya nishati chafu ya kupikia. 

Lengo Namba 7 la Malengo Endelevu ya Umoja wa Mataifa limejikita katika kuhakikisha upatikanaji wa nishati nafuu, inayopatikana kwa urahisi, endelevu na ya kisasa kwa wote.

Hata hivyo, bado kumekuwa na changamoto ya upatikanaji wa nishati nafuu, endelevu na za uhakika kwa ajili ya matumizi mbalimbali hususan ya kupikia hasa kwa nchi zilizopo Kusini mwa Jangwa la Sahara ikiwemo Tanzania

Hali hiyo inasababisha wananchi wengi na baadhi ya taasisi kuendelea kutumia nishati chafu ya kupikia, jambo linaloendelea kuchochea ongezeko la athari za kimazingira, kiafya, kiuchumi na kijamii.

Serikali ya Tanzania imeandaa Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia ambao unatoa mwelekeo wa nchi wa kuhamia katika matumizi ya nishati hiyo ukiwa na lengo la kuhakikisha asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia ikapo mwaka 2034.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks