Mambo ya kuzingatia unapojiandaa kustaafu
- Ni pamoja na kudhibiti mapato, matumizi na kuanaa mapema uwekezaji.
- Washauri wa masuala ya kifedha waonya wastaafu kufanya biashara wasizokuwa na uzoefu nazo.
Arusha. Kustaafu ni moja ya hatua muhimu katika maisha ya kila mfanyakazi, ikimaanisha mwisho wa safari ya ajira rasmi na mwanzo wa sura mpya ya maisha.
Hatua hii ni matokeo ya miaka mingi ya kujituma, ubunifu na kufanya kazi bila kuchoka kwa miaka 55 au 60 hadi kufikia kustaafu kwa mujibu wa Ibara ya 25 ya Sheria ya Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma ya Mwaka 2018.
Umri huo wa kustaafu unaweza kuwa wa hiari mfanyakazi anapofikisha miaka 55 au wa lazima ikiwa mfanyakazi atafikisha umri wa miaka 60 akiwa kazini lengo likiwa kupumzika huku akiwaachia kijiti vijana wenye uwezo wa kufanyakazi hiyo kwa ufanisi zaidi.
Pamoja na umuhimu wa kupumzika, idara ya kazi ya nchini Marekani inasema kuwa ili mtu aweze kufurahia maisha baada ya kustaafu anahitaji asilimia 70 mpaka 90 ya fedha aliyokuwa akiingiza wakati akiwa anafanya kazi.
“Usalama wa kifedha baada ya kustaafu hautokei tu kwa bahati. Unahitaji mipango, dhamira, na bila shaka, fedha…Siri ya kustaafu kwa uhakika ni kupanga mapema, imesema tovuti ya idara hiyo.
Ili kujiandaa vyema na hatua ya kustaafu Nukta Habari imezungumza na washauri binafsi wa masuala ya kifedha ambao wameanisha mambo matatu muhimu ya kuzingatia wakati unajiandaa.
- Kudhibiti mapato na matumizi
Miongoni mwa mambo muhimu ya kuzingatia kwa mfanyakazi yoyote anayejipanga kustaafu ni kudhibiti mapato anayoyaingiza kwa siku, wiki au mwezi na kujua namna ya kuyatumia kikamilifu kwa ajili ya sasa na baadae.
Ndahani Mwenda, Mshauri wa Masuala ya kifedha kutoka jijini Dar es Salaama ameiambia Nukta Habari kuwa ili kuweza kudhibiti mapato na matumizi mfanyakazi lazima ajifunze kutumia kanuni ya 50, 30, 20 ambayo ni maarufu na imewasaidia wengi kudhibiti fedha.
Kwa mujibu wa kanuni hii, unapaswa kugawanya mapato yako katika sehemu tatu: asilimia 50 kwa mahitaji ya msingi (kama vile kodi ya nyumba, usafiri, ada, chakula, na umeme), asilimia 30 kwa matumizi ya kawaida (kama vile burudani na mavazi), na asilimia 20 kwa ajili ya kuweka akiba na kuwekeza.
“Kustaafu ni suala la lazima, hakuna atakayefaya kazi milele, ukiweza kuwa mtii kwenye kanuni hii lazima uone matokeo na hata ukistaafu kesho unaweza kuona matunda ya kazi uliyokuwa unaifanya,” amesema Ndahani.
- Kuanza mapema uwekezaji
Mbali na kutegemea mifuko ya hifadhi ya jamii ambayo inalenga kutoa mafao kwa wanachama wake baada ya kustaafu, kuugua, au kufariki Ndahani anashauri mfanyakazi kutafuta aina nyingine za uwekezaji wenye tija.
Miongoni mwa uwekezaji anaoweza kufanya mfanyakazi ni uwekezaji katika hisa kupitia Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), ambapo wawekezaji hununua na kuuza hisa kwa faida au kupata gawio.
Pia mfanyakazi anaweza kuwekeza katika mifuko ya ikiwemo Unit Trust of Tanzania (UTT AMIS), unaosimamiwa na Benki Kuu ya Tanzania,
Naye Pearly Meena, mshauri mwingine wa masuala ya fedha jijin Dar es Salaam anasema umri sahihi kwa mfanyakazi kuwekeza ni mara baada ya kupata kazi.
“vijana, hawataki kujifunza uwekezaji kwasababu wengi ni wavivu ila ilitakiwa akiingia tu kazini na kuanza kulipwa basi aanze kuwekeza ili aweze kuwa na akiba itakayomtosha wakati akistaafu,: anasema Meena.
- Kuwa na elimu sahihi ya fedha
Licha ya kuwa kundi kubwa la wafanyakazi wanaostaafu kila mwaka Ndahani anasema kuwa ni asilimia chache kati yao ndiyo wenye elimu sahihi ya masuala ya fedha hali inayofanya baadhi yao kutumia vibaya fedha ya kiinua mgongo na kujikuta wakisota kwenye umaskini.
Mtaalamu huyo wa masuala ya fedha anasema kuwa muda sahihi wa kutafuta elimu sahihi ya uwekezaji ni wakati wa ujana au ukichelewa basi iwe kabla hujapokea hela ya kiinua mgongo
“Tatizo la wastaafu wengi akioata tu pesa anaita kikao cha mke na watoto ambao wengi wao hawana elimu ya fedha au uwekezaji matokeo yake wanaishi tu kurudi kwenye umaskini,” amesema Ndahani.
Aidha, Ndahani amewataka wastaafu kujiepusha kufanya biashara ambazohawana ujuzi nazo au kuwekeza bila kuwa na taarifa sahihi ili kuepuka kupoteza fedha za kiinua mgomgo au mafao na baadae kuruddi kuwa tegemezi.
Latest



