Afrika inavyoweza kuongeza upatikanaji wa umeme

January 27, 2025 8:37 pm · Lucy Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni pamoja na kuangazia vipaumbele vya kisera katika masuala ya nishati vilivyoweka na nchi za Afrika.
  • Wadau washauri ‘Misheni 300’ iangazie nishati safi ya kupikia.

Arusha. Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dotto Biteko amefungua mkutano wa nishati wa wakuu wa nchi za afrika utakaofanyika kwa siku mbili jijini Dar es Salaam huku akiwataka viongozi hao kujadili mbinu zitakaoongeza upatikanaji wa umeme Afrika.

Mkutano huo uliobeba ajenda ya ‘misheni 300’ unaofanyika Januari 27 na 28 katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa JNICC ni miongoni mwa mikutano mikubwa zaidi kuwahi kufanyika barani Afrika ukilenga kuongeza upatikanaji wa nishati kwa Waafrika milioni 300.

Dk Biteko aliyekuwa akizungumza katika mkutano huo leo Januari 27, 2025 amesema ili kufanikisha lengo hilo wakuu hao wanatakiwa kuwekeza nguvu za pamoja ili kufanikisha upatikanaji wa umeme kwa Waafrika milioni 300 kati ya milioni 600 waliosiokuwa na nishati hiyo.

“Kutokana na changamoto hii mkutano huu umeitishwa ukiwa na lengo kubwa lakini linalowezekana la kuongeza upatikanaji wa umeme kwa watu wasiopungua milioni 300 barani Afrika ndani ya miaka mitano ijayo,” amesema Dk Biteko.

Kwa mujibu wa Dk Biteko mkutano huo utaangazia vipaumbele vya kisera katika masuala ya nishati vilivyoweka na nchi za Afrika, kutafuta suluhu na kuweka mikakati ya utekelezaji wa mpango wa misheni 300 katika miaka mitano ijayo.

Aidha, Dk Biteko amewashukuru waandaaji wenza wa mkutano huu, ambao ni Benki ya Dunia (WB), Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Taasisi ya Rockefeller, Nishati Endelevu kwa Wote, na Muungano wa Kimataifa wa Nishati kwa Watu na Sayari kwa kufanikisha mkutano huo.

‘Misheni 300’ iangazie nishati safi ya kupikia

Wakati mawaziri hao wakijadili jinsi ya kufikisha umeme kwa Waafrika 300 ambao hawajafikiwa na nishati hiyo baadhi ya wadau wameshauri kuingizwa kwa ajenda ya nishati safi ya kupikia ambayo pia ni janga kwa nchi za Afrika.

Dk Richard Muyungi, Mjumbe Maalum wa Rais aliyekuwa miongoni mwa wazungumzaji amesema kuwa bado kuna idadi kubwa ya Waafrika wanatumia nishati zisizo salama kupikia jambo linalowasababishia kupoteza maisha hivyo mkutano huo utafute suluhu ya tatizo hilo.

Ametolea mfano baadhi ya mikakati ambayo Tanzania imeichukua kupambana na tatizo la matumizi ya nishati zisizo salama ambayo ni pamoja na uhamasishaji kutoka kwa viongozi wa juu.

“ili kubadilisha mifumo katika ngazi ya kitaifa kuhusu nishati safi ya kupikia , kitu cha kwanza unachohitaji ni uhamamsishaji kutoka kwa viongozi wa juu kabisa. Na hili tumeshuhudia kutoka kwa Mheshimiwa Rais akisimamia uzinduzi wa mkakati wa nishati safi ya kupikia” amesema Dk Mayungi.

Mbali na mkakati huo ametaja masuala ya utoaji wa elimu, ushirikishwaji wa wadau wa sekta binafsi na mashirika ya kimataifa kama mbinu zinazotumiwa na Tanzania kuchochea matumizi ya nishati safi.

Naye Richard Kimani, Mkurugenzi wa Mtendaji wa M- Gas amewataka viongozi hao kutaza ma kwa upya suala la gharama ya nishati safi ya kupikia na kubuni teknolijia itakayowawezesha Waafrika kuipata kwa gharama nafuu.

Mkutano huo wa nishati wa wakuu wa nchi wa Afrika utaendelea tena siku ya Kesho ukitarajiwa kuhudhuriwa na marais 25 akiwemo Rasi wa Tanzania Samia Suluhu Hassan.

Enable Notifications OK No thanks