Wanawake Tanesco watwishwa zigo kukabiliana na rushwa
- Dk Biteko awataka wanawake hao kutowafumbia macho watu wenye vitendo hivyo.
Arusha. Waziri wa Nishati na Naibu Waziri Mkuu, Dk Dotto Biteko amewataka wanawake wa Shirika la UmemeTanzania (Tanesco) kukemea vitendo vya rushwa vinavyotokea wakati wa kuunganishiwa umeme wa majumbani au sehemu za kazi.
Kwa miaka mingi baadhi ya watumishi Tanesco wamekuwa wakikabiliwa na tuhuma za rushwa ili kutoa huduma za kuunganisha umeme kwa wateja jambo ambalo limekuwa likirudisha nyuma jitihada za Serikali kuongeza watumiaji wa nishati hiyo nchini.
Dk Biteko aliyekuwa akizungumza leo Machi 4, 2025 katika kongamano la kuhamasisha matumizi ya umeme kupikia jijini Dar es Salaam amewataka wanawake hao kutowafumbia macho watu wenye vitendo hivyo.
“Wanawake tuambiane ukweli changamoto ya umeme inapotokea ukiona kuna mtu miongoni mwenu anamtafuta mteja na kumuomba rushwa ili akauganishe umeme ninyi wakinamama muwe wa kwanza kumkemea…
…Ninyi wakina mama msikubali shirika lenu lipakwe matope na watu wachache wenye tamaa tuwakemee kwa nguvu zetu zote na watanzania wapate umeme wa uhakika kwa sababu serikali inawekeza fedha nyingi,” amesema Biteko.
Kwa mujibu wa Biteko, jitihada hizo zitasaidia kuongeza idadi ya Watanzania waliounganishwa na umeme hususani vitongoji 11,532 ambavyo bado havijaunganishwa.
Aidha, jitihada hizo pia zitasaidia kuongeza matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini Tanzania hadi kufikia asilimia 80 kufikia mwaka 2030 kama ilivyoanishwa katika Mkakati wa Nishati Safi ya Kupikia ulizozinduliwa mwaka 2024.
“Mimi naamini tukiamua wakina mama kuwakemea watu wote wanaofanya mambo haya…hatutakubali tena wanawake wengi wapoteze maisha kwa sababu ya kupikia nishati chafu,” amesema Dk Biteko.
Latest



