Tumbaku: ‘Rafiki wa mashaka’ anayeiweka Tanzania njia panda

Rodgers George 0243Hrs   Julai 22, 2020 Ripoti Maalum
  • Njia panda hiyo ni uamuzi wa kutokomeza matumizi ya tumbaku utakavyoondoa mabilioni ya fedha yanayoingizwa na bidhaa hiyo kila mwaka. 
  • Takwimu zaonyesha kuwa zaidi ya robo tatu ya mapato yatokanayo na tumbaku yanatumika kutibu kansa itakanayo na matumizi ya zao hilo. 
  • Makusanyo ya Serikali yanayotokana na tumbaku yameendelea kuongezeka.
  • Takriban watu 7,000 hatarini kukosa ajira iwapo viwanda vya tumbaku vitasitishwa.

Dar es Salaam. Licha ya tumbaku kubainishwa na wataalamu kuwa na madhara lukuki kwa afya ya binadamu, zao hilo limeendelea kuwa chanzo cha ajira kwa wengi na mapato kwa Serikali kiasi cha kuwaweka wadau njia panda katika kupunguza matumizi yake. 

Tumbaku imeendelea kuchangia mapato ya Serikali kwa kodi na kuingiza fedha za kigeni kutokana na mauzo nje ya nchi. 

Ripoti ya Utafiti wa Tumbaku kwa Watu Wazima Duniani (GATS) wa mwaka 2018 iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Shirika la Afya Duniani (WHO) na Ofisi Mtakwimu Mkuu wa Serikali Zanziabar (OCGS) imeeleza kuwa, zao la tumbaku linachangia zaidi ya Sh92.5 bilioni kila mwaka katika pato la Taifa.

Sehemu kubwa ya mapato hayo ni kutokana na mauzo ya zao hilo nje ya nchi ambapo hadi kufikia mwaka 2019, Tanzania ilizalisha tani 68,147 za tumbaku kama ilivyoelezwa katika Uchambuzi wa Takwimu muhimu (Tanzania in figures 2019).

Mchango wa zao hilo katika kuingiza fedha za kigeni unaonekana kuongezeka baada ya takwimu hizo mpya kubainisha kuwa mwaka 2019, mauzo ya tumbaku nje ya nchi yaliipatia Tanzania Sh335.3 bilioni.

Zaidi ya asilimia 90 ya zao hilo, kwa mujibu wa ripoti ya GATS, huuzwa nje ya nchi kwa mataifa mbalimbali duniani zikiwemo Afrika Kusini, Uingereza na Marekani na kiwango kidogo kilichosalia ama moja ya 10 hutumika kwa matumizi ya ndani.

Ukiachana na mauzo nje ya nchi, hata ndani tumbaku imezidi kuchangia kiwango kikubwa cha kodi kupitia ushuru wa bidhaa na kodi ya ongezeko la thamani (VAT). 

Ripoti ya Takwimu za Kodi za mwaka 2017/18 iliyotolewa na NBS inaonyesha kuwa, sigara ni bidhaa ya tatu kwa kuchangia kiwango kikubwa cha ushuru wa bidhaa (Domestic excise taxes) baada ya bia na simu za mkononi.

Kiwango cha juu cha mchango wa sigara katika VAT kuwahi kurekodiwa ndani ya kipindi cha miaka 12 tangu mwaka 2006/07 kilikuwa Sh48.7  bilioni mwaka 2015/16, kikizizidi baadhi ya bidhaa anazotumia mwanadamu takriban kila siku kama sukari na vinywaji laini. Picha| The Irish Times.

Katika kipindi cha kati ya mwaka 2006/07 na mwaka 2017/18, sigara imeingiza jumla ya Sh1.1 trilioni kama ushuru wa bidhaa na kiwango chake kimekuwa kikiongezeka kwa kasi mwaka hadi mwaka. 

Mfano, kiwango cha juu cha ushuru wa bidhaa uliokusanywa kutoka kwenye sigara kuwahi kurekodiwa ni mwaka 2017/18 ambapo Serikali iliweka kibindoni Sh157.3 bilioni, takriban mara tatu ya kile kilichokusanywa kutoka kwenye bidhaa hiyo mwaka 2009/10. Mwaka 2009/10 Serikali ilikusanya ushuru wa bidhaa katika sigara wa Sh55.2 bilioni. 

Mapato ya ushuru wa bidhaa kutoka kwenye sigara mwaka 2017/18 yalitosha kabisa kugharamia miradi ya maendeleo na matumizi ya kawaida ya wizara tatu za Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Wizara ya Habari, Utamaduni, Michezo na Sanaa na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi. 

Wizara hizo tatu kwa pamoja katika mwaka huo wa fedha wa 2017/18 zilikadiriwa kutumia Sh116.7 bilioni pekee maana yake kuwa chenji ya ushuru wa bidhaa kutoka kwenye sigara ungeweza kugharamia pia huduma nyingine zaidi ikiwemo kujenga vituo vya afya kwa Sh40 bilioni zilizosalia. 

Ukiachana na ushuru wa bidhaa, sigara zinachangia pia kiasi kikubwa cha VAT katika kibubu cha Serikali. Kati ya mwaka 2006/07 hadi mwaka 2017/18 sigara zimechangia jumla ya Sh443.5 bilioni ikiwa ni kodi ya VAT ambayo hutozwa kwa mlaji wa mwisho. 


Zinazohusiana


Uchambuzi zaidi wa takwimu hizo rasmi za kodi unaonyesha kuwa kiwango cha juu cha mchango wa sigara katika VAT kuwahi kurekodiwa ndani ya kipindi hicho kilikuwa Sh48.7  bilioni mwaka 2015/16, zikizizidi baadhi ya bidhaa anazotumia mwanadamu takriban kila siku kama sukari na vinywaji laini. 

Umuhimu wa zao hilo na bidhaa zake unaendelea kuwa mkubwa katika uchumi wa Tanzania kwa kuwa Kitabu cha Hali ya Uchumi wa taifa cha mwaka 2018 kilichotolewa na NBS kinaeleza kuwa, uzalishaji wa bidhaa za sigara uliongezeka baada ya kuwepo “mahitaji makubwa katika soko la ndani na nje.” 

Kwa mwaka 2018, uzalishaji wa bidhaa za sigara ulikuwa kwa asilimia 6.9 ukiwa ni juu ya wastani wa ukuaji wa bidhaa za biskuti na tambi zilizokuwa kwa asilimia 2.8, betri (asilimia 5.7), saruji (asilimia 1.4) na nguo ambazo ukuaji wake ulikua kwa asilimia 1.1 pekee.

Mbali na kuchangia mapato ya Serikali, tumbaku ni chanzo cha mkate wa kila siku kwa maelfu ya Watanzania waliopo mashambani na walioajiriwa viwandani. 

Kitabu hicho kimeonyesha kuwa zao la tumbaku na uzalishaji wa sigara umeajiri watu 6,769 viwandani, hivyo kuzuia matumizi ya zao hilo nchini huenda kukawaacha watu hao wanaotegemewa na familia zao kwenye ukata. 

Endapo Tanzania itaungana na moja ya nchi iliyopo kusini mwa bara la Asia ya Bhutan  ambayo ni nchi pekee duniani iliyozuia uuzaji na uzalishaji wa tumbaku, nini kitatokea?

Mchambuzi wa masuala ya uchumi kutoka Kituo cha Maendeleo Endelevu (CSDI) cha Jijini Dar es Salaam William Massawe amesema endapo matumizi ya zao la tumbaku yatadhibitiwa nchini kuna uwezekano wa kutokea athari za uchumi za muda mfupi na manufaa ya muda mrefu.


Athari za kudhibiti matumizi ya tumbaku kiuchumi

Kwa upande wa athari za muda mfupi, mchumi huyo amesema nchi itapoteza mapato ambayo yanatokana na zao hilo baada ya kuuzwa nje ya nchi au kupitia kodi za ndani. 

Hata hivyo, Massawe amesema athari hizo za kikodi siyo kubwa zikilinganishwa na manufaa yatakayopatikana nchini baada ya kupunguza matumizi ya tumbaku.

“Ukaushwaji wa tumbaku unachangia katika ukatwaji wa miti kwa wingi katika maeneo ambapo zao hilo linalimwa. Hali hiyo inasababisha ukame na ongezeko la joto linaloathiri kilimo kwa ujumla,” amesema Massawe.

Zaidi, mchambuzi huyo amesema Serikali inatumia fedha nyingi katika kutibu watu walioathirika kiafya na matumizi ya zao hilo.

Kwa Mujibu wa ripoti ya GATS), kila mwaka asilimia 15 ya ardhi inayofaa kulimwa Tanzania (arable land)  hukatwa miti kwa shughuli za uzalishaji wa zao la tumbaku.

Ripoti hiyo pia imeeleza hata wakati Tanzania ikiingiza fedha nyingi kupitia zao la tumbaku, bado imekuwa ikitumia zaidi ya robo tatu ya mapato yanayopatikana na zao hilo kutibu wagonjwa wenye magonjwa yatokanayo na madhara ya tumbaku.

“Wakati Tanzania ikiingiza takribani Sh115.9 bilioni kwa mwaka kupitia tumbaku, zaidi ya Sh92.75 bilioni inatumia kutibia kansa zinazohusiana na tumbaku pekee,” inasomeka sehemu ya ripoti ya GATS.

Kiwango hicho kilichoanishwa na ripoti hiyo ni kwa ajili ya matibabu ya kansa pekee ukiachana na gharama nyingine ambazo Taifa linaingia katika kukabiliana na uharibifu wa mazingira na changamoto nyingine zitokanazo na zao hilo. 

Usikose sehemu ya mwisho ya makala haya ambayo itakujia hapa hapa Nukta (www.nukta.co.tz) kesho kuliangazia suala hili kwa mapana zaidi. 

Related Post