Biashara, sanaa ya uchoraji inavyochukua mkondo mpya Tanzania- 3
- Ni pamoja na uhalisia wa kuwa kazi hii inaambatana na matumizi ya kompyuta kwa muda mrefu.
- Pia, inahitaji uwe na ujuzi zaidi ya ubunifu tu ikiwemo biashara na lugha nzuri.
- Kwa anayehitaji kuanza, anahitaji kompyuta kama mtaji mkuu.
Dar es Salaam. “Graphic designing” kama zilivyo fani zingine ikiwemo udaktari, uandishi wa habari na Uanasheria ni fani ambayo imetoa ajira kwa vijana waliochagua kuendana na teknolojia ya tehama na mawasiliano (Tehama).
Fani hiyo ambayo imekuwepo tangu kuanza kwa mawasiliano ya njia ya picha imepitia mabadiliko mengi kufikia sasa. Zamani watu walitengeneza mabango na matangazo kwa kuyachora lakini kwa sasa, inahitaji kompyuta na mashine kubwa za kuchapisha matangazo hayo.
Kwa yeyote anayetazamia kuingia katika fani hii anahitaji kufahamu kinaga ubaga kuhusu undani wa fani hii ili aweze kufanya vizuri na kuwa katika nafasi nzuri ya kushindana kwani wadau wa fani hiyo wanazidi kumiminika sokoni kila mwaka.
Mratibu wa Maudhui kutoka kampuni ya Empower Limited, Mayur Nayi ameiambia Nukta Habari (www.nukta.co.tz) kuwa mtengeneza grafiki ni mbunifu wa mawasiliano ya picha ambaye hutumia kompyuta kubuni nembo ya biashara, vipeperushi na matangazo ya kuchapishwa au ya kielektroniki.
“Kuwa Graphic Designer ni rahisi na ngumu. Ni rahisi kwa sababu mtu yeyote anaweza kufanya kazi hiyo na akiwa na umri wowote,” anasema Nayi.
Ugumu wa kazi hiyo huanza na ulazima wa kutenga muda wa kujifunza na utayari wa kufanya kazi mbele ya kompyuta kwa muda mrefu.

Unapoamua kuvalia njuga kazi hii unahitaji nini?
Kwa wengine hufanya kazi hii kama kitu wanachokipenda lakini itafika wakati ambapo utahitaji kujua jinsi ya kuifanya kama biashara.
Kwa mujibu wa Nayi, mbunifu wa grafiki anahitaji vipaji vya nyongeza ikiwemo ubunifu, biashara, kuchangamana na watu (networking), ujuzi wa kutumia kompyuta na lugha.
“Endapo unasomea, usiogope kwani unaweza kuifanya hiyo kazi japo inahitaji uwe na shauku ya kujifunza na kufanya mazoezi,” anasema Nayi.
Pia, unahitaji ujuzi wa programu zikiwemo apps za Adobe (Photoshop na Illustrator) na programu za mtandaoni ambazo ni bure kwa wale wanaotaka kufanya kwa haraka kama canva.com.
TANGAZO
Mbinu za kupata masoko ya kitaifa na kimataifa
Kitakachokusaidia kupata masoko katika biashara hii ni ubora wa kazi yako kwani kila mtu anapenda kazi bora. Mbali na hayo, unahitaji kuwa na kurasa za mitandao ya kijamii kwa ajili ya kutangaza kazi zako.
Mbunifu binafsi, Evon Evans ameiambia Nukta Habari kuwa masoko yanapatikana kwa kufanya kazi nzuri.
Amesema, endapo utafanya kazi za kiwango cha juu zitakazotambulika na wengi, ni lazima utapata masoko yawe ya kitaifa na hata ya kimataifa.