Biashara, sanaa ya uchoraji inavyochukua mkondo mpya Tanzania-2
- Kabla ya kuanza kazi ya uchoraji, hakikisha umefanya mazoezi ya kutosha.
- Bei utakazowatoza wateja ziandane na thamani ya kazi yako.
- Unaweza kuanza ajira hii kwa mtaji mdogo.
Dar es Salaam. Baada ya kuangazia kwa undani sehemu ya kwanza ya mabadiliko yanayotokea katika tasnia ya uchoraji Tanzania na jinsi wabunifu wanavyotakiwa kuendana na kasi ya mabadiliko hayo, sasa tujadili mambo ya kuzingatia kwa watu wanaotaka kuingia katika tasnia hiyo.
Uchoraji wa picha unaweza kuwa kipaji au ujuzi ambao mtu anajifunza kwa ajili ya kujipatia kipato, kujifurahisha na kuwapatia wengine kama zawadi ili kudumisha upendo kwenye jamii.
Picha zinazongumziwa hapa ni zile zinazochorwa kwa kalamu kwenye karatasi au sehemu maalum ambayo itabeba ujumbe fulani kwa mtu au jamii.
Kwa sasa, ni kawaida mtu kumzawadia mpenzi wake picha kubwa ya sura yake ambayo imechorwa kwa umaridadi kabisa. Siyo mpenzi tu, watoto huwapatia wazazi, rafiki huwapatia rafiki zao na orodha inaendelea.
Nyuma ya picha hizo ni vijana Wakitanzania ambao wamewekeza muda, malighafi na ubunifu katika kujiingizia kipato. Mshangao ukiwa ni inawezekanaje kuhamisha muonekano halisi wa mtu katika karatasi kwa kutumia penseli, kifutio na karatasi?
Picha za kuchora hununuliwa na baadhi ya watu na kisha kutolewa kama zawadi. Picha| David Msia (@de_urudraws).
Nini kinahitajika kuingia katika sanaa ya uchoraji?
Furaha Mwakitalu, mkazi wa Dar es Salaam ambaye amekuwa akifanya kazi ya sanaa ya uchoraji kwa miaka mitatu sasa anasema kuwa msanii wa kuchora inahitaji kipaji na muda wa kujifunza na kufanya mazoezi.
Hata hivyo, siyo wachoraji wote wanahitaji kipaji kwani mtu anaweza kujifunza.
Mchoraji huyo ameiambia Nukta Habari kuwa, sanaa ya uchoraji ni kati ya ajira zinazoweza kumnufaisha kijana endapo atawekeza katika fani hiyo.
“Kwa kuanza, unahitaji mtaji wa Sh500,000 ambao utakusaidia kununua malighafi na kisha unaweza anza kufanyia kazi nyumbani wakati unakuza jina lako,” anasema Mwakitalu ambaye anafanya shughuli zake Mlimani City jijini hapa.
Uchoraji ni ajira
Kama zilivyo kazi nyingine halali, uchoraji pia ni kazi halali ambayo mtu akiwekeza muda na rasilimali ana uhakika wa kupata kipato kumuwezesha mtu kupata mahitaji ya msingi.
Mwakitalu amesema, kuifanya sanaa ya uchoraji unahitaji eneo la kufanyia kazi, malighafi ikiwemo brashi za kucholea, kanvasi na rangi kwa ajili ya kutekeleza kazi zako.
“Malighafi unazotumia mfano penseli, brashi na karatasi au kanvasi zinatakiwa kuwa nzuri. Unaweza kuzipata katika maduka ya vifaa vya ofisi na shule (stationeries) au mtandaoni,” ameshauri Mwakitalu ambaye hutumia mtandao wa easybuy kununua baadhi ya vifaa.
Kupitia Uchoraji, Msia amesema amejipatia wateja mbalimbali wakiwemo kutoka mataifa ya nje ikiwemo Marekani. Picha| David Msia (@de_urudraws)
Muda, mazoezi na matangazo ndiyo funguo ya biashara hii
Kabla ya kuanza kufanya uchoraji kama biashara hakikisha unakuwa umefanya mazoezi ya kutosha kuepusha kuharibu soko lako la kuanzia.
Inashauriwa kuwa na muda wa kufanya mazoezi ya kuchora picha za jamaa na rafiki mbazo unaweza kuwauzia kwa bei ya kawaida ua kuwapatia kama zawadi.
Mchoraji kutoka Aruha, David Msia (@de_urudraws) anasema yeye alianza na watu wake wa karibu hasa rafiki zake ambao aliwachora na kuwauzia picha kwa Sh50,000 ambazo fedha hizo alizitumia kununua malighafi nyingine kuendelea na mazoezi.
Msia anasema baada ya kuiva alianza kuchora picha za watu maarufu ambao waliziweka katika mitandao ya kijamii ambapo ilikuwa mwanzo wa kupata wateja wengi zaidi.
“Huwezi ukamchora msanii akatoka vibaya utegee ataiweka picha hiyo mtandaoni. Lazima iwe nzuri, ivutie ndio atafanya hivyo. Kwa hiyo, kabla ya kuanza biashara ya uchoraji, fanya mazoezi kwanza,” ameshauri Msia ambaye kwa sasa unauza picha moja hadi Sh100,000.
Unavyoweza kutafuta soko la kazi zako
Waswahili wanasema “biashara ni matangazo” na kama zilivyo biashara nyingine, biashara ya uchoraji pia inahitaji kuwafikia wateja ili waifahamu zaidi.
Endapo hauna msingi mkubwa wa wateja, inashauriwa kutafuta majukwaa kwa ajili ya kuonyesha kazi zako ili watu waweze kukuona.
Mwakitalu anasema, hiki ndiyo kipindi cha kufanya maonyesho ya kuchora mubashara, kufanya kampeni za mitandao ya kijamii na kama alivyofanya Msia, kuchora picha za watu mashuhuri.
“Nilianza na wateja wa Tanzania lakini kupitia maonyesho, mitandao ya kijamii nimeweza kuwafikia wateja wa kimataifa wakiwemo wa Marekani na Uingereza,” anasema Msia ambaye anachora picha kwa penseli, rangi za kawaida na rangi za mafuta.
Kwa mchoraji yeyote, masoko yanapatikana kwa kufanya maonyesho ya kazi zako ili wadau wa sanaa wakutambue. Picha| Undarey Mtaki.
Kupangilia bei zako
Bei zako pia ni sehemu ya kuvutia wateja na kuwafukuza. Inashauriwa wakati wa kuanza, usiwe na bei kubwa sana ilimradi zinalipia muda wako na gharama za malighafi.
Msia anasema, kwa kuanzia, kuuza picha kwa Sh50,000 ambayo unaweza ukawa umetumia muda mrefu kuchora siyo kitu kibaya.
“Mara nyingi unapoanza inashauriwa uweke bei ambayo inakurudishia malighafi uliyotumia na kukupatia fedha kidogo ya faida. Usianze na bei “kuuuubwa” utakosa wateja,” amesema Msia ambaye kwa sasa anauza picha moja hadi kwa Sh800,000.
Makala ijayo tutaangalia kwa undani kazi ya ubunifu wa grafiki (graphic designing). Endelea kusoma habari za Nukta Habari (www.nukta.co.tz).
Latest