‘Betting’, vinywaji baridi kuchangia bima ya afya kwa wote Tanzania
- Vyanzo hivyo ni pamoja na ushuru wa michezo ya kubashiri (betting) na vinywaji baridi.
- Watanzania milioni 15.8 wasio na uwezo kunufaika.
Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imebainisha vyanzo vya mapato vitakavyoiwezesha kugharamia bima ya afya kwa Watanzania milioni 15.8 wasiokuwa na uwezo vikiwemo ushuru unaotokana na vinywaji baridi na michezo ya kubahatisha(betting).
Wananchi hao ni wale wanaotoka kaya maskini zisizo na uwezo ambazo takwimu za Utafiti wa Mapato na Matumizi ya Kaya Binafsi (Household Budget Survey – HBS) wa mwaka 2017/18 unawaainisha kuwa ni asilimia 26.4.
Kwa mujibu wa takwimu za Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 idadi hiyo ni sawa na watu milioni 15.8 huku milioni 4.4 kati yao wakiishi kwenye umaskini uliokithiri.
Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu aliyekuwa akiwasilisha muswada wa bima ya afya kwa wote kwa mara ya pili bungeni Dodoma leo Novemba 1, 2023 amesema vyanzo hivyo vya mapato vilianishwa na Wizara ya Fedha.
Hii ni mara ya pili kwa muswada huo kusomwa bungeni, mara ya kwanza ulisomwa Septemba 22, 2023 ambapo ulipingwa na kukosolewa vikali na wabunge.
Miongoni mwa hoja za muswada huo zilizopingwa ni pamoja na kufutwa kwa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (CHF) jambo ambalo lingefanya baadhi ya wananchi maskini kushindwa kujiunga na mifuko mingine yenye gharama za juu.
Pia, kuweka zuio la kupata baadhi ya huduma pasipo kuwa na bima ya afya ikiwemo leseni ya udereva, pasi ya kusafiria, kitambulisho cha Taifa.
“Vyanzo vya mfuko huu kutokana na maamuzi ya Wizara ya Fedha ni kama ifuatavyo, sehemu ya mapato yatokanayo na ushuru wa bidhaa kwenye vinywaji vyenye kaboni (carbonated drinks), Vinywaji vikali (Liquor) pamoja na bidhaa za vipodozi…
…Ada ya bima za vyombo vya moto na mapato yatokanayo na ushuru wa miamala ya kielektroniki kwa kadri itakavyopendekezwa na waziri mwenye dhamana ya masuala ya fedha,” amesema Waziri Ummy.
Vyanzo vingine ni pamoja na fedha zitakazotengwa na Bunge, mapato yatokanayo na uwekezaji wa mfuko na zawadi na misaada kutoka kwa wadau mbalimbali.
“Hapa kwenye misaada tayari tuna wadau wetu wanaolipia bima za wajawazito kwa mikoa ya Mtwara,Tanga na Mbeya, tunaamini wadau wa maendeleo watatuunga mkono kulipa bima kwa wasio na uwezo,” amesema Ummy.
Sambamba na kugharamia wasio na uwezo mfuko huo pia utagharamia matibabu ya magonjwa sugu yasiyoambukiza ikiwemo magonjwa ya figo na kisukari.
Soma zaidi:
Wafanyakazi sekta binafsi wapewa uhuru
Muswada huo unaobeba mustakabali wa huduma za afya kwa Watanzania umependekeza kuondolewa kwa ulazima wa wafanyakazi wa sekta binafsi kuchangia asilimia sita ya mishahara yao katika mfuko huo.
“Sekta binafsi hawalazimishwi kujisajili waajiriwa wao katika mfuko wa umma, wanaweza wakasajili katika mifuko binafsi watazingatia sheria zinazosimamimia vitita vya sekta binafsi,” amesema.
Wabunge watoa maoni mchanganyiko
Mbunge Viti Maalum (CCM), Bernadeta Mushashu ametoa ameitaka Serikali kuweka vigezo vitakavyobainisha kaya maskini zinazotakiwa kunufaika na mfuko huo, huku akiitaka Serikali kubainisha watu wenye ulemavu kama sehemu ya wanufaika wa mfuko huo.
Hata hivyo, Mbunge wa jimbo la Kawe (CCM), Josephat Gwajima ameiomba Serikali kuharakisha ujenzi wa vituo vya afya vijijini ili kuwezesha utolewaji wa huduma bora za afya wakati bima hizo zitakapoanza kutumika.
“Ninaiomba Serikali ijitahidi maeneo ya vijijini ambayo hakuna zahanati wapeleke zahanati ili wananchi walipe bima na wapate mahali pa kutibiwa,” amesema Gwajima.