Benki ya Dunia yatoa mkopo wa Sh1.2 trilioni kwa Tanzania
- Utasaidia kuboresha sekta ya elimu hasa sekondari
- Kipaumbele kitakuwa kuboresha mazingira ya kujifunzia kwa watoto wa kike hasa waliopata mimba.
- Serikali yasema ni uamuzi wa kihistoria.
Dar es Salaam. Hatimaye Benki ya Dunia imepitisha mkopo wa elimu wa Dola za Marekani milioni 500 kwa Tanzania baada ya kuahirisha kufanya hivyo kwa mara kadhaa kutokana na suala la kuwarudisha shule watoto wa kike waliopata ujauzito baada ya kujifungua.
Mkopo huo wa Sh1.2 trilioni unakusudia kuongeza ubora wa elimu kwa kujenga vyumba vya madarasa, maabara, mabweni na nyumba za watumishi na vifaa vya kufundishia.
Taarifa ya benki hiyo iliyotolewa jana (Machi 31, 2020) imeeleza kuwa mkopo huo utasaidia watoto wa Tanzania kupata elimu na kumaliza elimu ya sekondari katika mazingira salama na bora ya kujifunzia.
Mkopo huo ambao utakuwa chini ya mradi wa uboresha wa elimu ya sekondari (SEQUIP) utawafaidisha takriban wanafunzi milioni 6.5 wa shule za sekondari kwa kuimarisha utoaji elimu na kuanzisha mfumo mzuri wa kuwasaidia wanafunzi wanaoacha shule wakiwemo wasichana wanaopata mimba.
“Kila mtoto wa Tanzania anastahili elimu bora, lakini maelfu wao wanakosa fursa hiyo ya kubadilisha maisha kila mwaka. Huu mradi unawaweka vijana wadogo wa nchi hiyo katika mstari wa mbele.
“Na unaelekeza theluthi mbili ya rasilimali zake katika kuweka mazingira salama na bora ya kujifunzia kwa wasichana,” amesema Mkurugenzi Mkaazi wa benki hiyo nchini Tanzania, Mara Warwick.
Katika taarifa yake, benki hiyo imebainisha kuwa kwa miaka miwili iliyopita, takriban watoto 300,000 nusu yao wakiwa ni wasichana wameshindwa kuendelea na masomo ya sekondari kutokana na uhaba vya vyumba vya madarasa katika shule za Serikali.
“Kwa kuongezea inakadiriwa wasichana 5,500 wa Tanzania wanapata mimba kila mwaka na kuacha masomo. Mradi wa SEQUIP umebuniwa kuwawezesha wasichana na wavulana kuwawezesha kusoma mpaka kitado cha tano na sita,” inasomeka sehemu ya taarifa ya benki hiyo.
Zinazohusiana:
- Benki ya Dunia yaeleza sababu za kuipatia Tanzania mkopo wa Sh1 trilioni
- AfDB yaipatia Serikali mkopo wa zaidi ya Sh589 bilioni
- Mkopo wa Benki ya Dunia waibua utata ujenzi maabara za sekondari Tanzania
Benki ya Dunia imeahirisha kupitisha mkopo huo muhimu mara kadhaa kutokana na kutoridhishwa kwake na sera ya Serikali kuwazuia wanafunzi wajawazito kwenda shule.
Shinikizo zaidi liliwekwa na Wanasiasa na wanaharakati wa Tanzania na wa kimataifa walioshinikiza benki hiyo isitoe mkopo huo kwa Serikali kutokana na kile walichokiita kuwa ni sera na sheria ya elimu ya kibaguzi kwa wasichana wanaotapata mimba wakiwa shuleni.
Serikali, wadau watoa maoni
Msemaji Mkuu wa Serikali ya Tanzania Dk Hassan Abbas amesema Benki ya Dunia imefanya uamuzi wa kihistoria kuidhinisha mkopo huo ili kuendelea kuinua elimu nchini Tanzania.
— Msemaji Mkuu wa Serikali (@TZMsemajiMkuu) April 1, 2020
Mbunge wa Kigoma Mjini Zitto Kabwe akizungumzia mkopo huo amesema “natoa mkono wa pongezi kwa watu wote ambao walishiriki kupaza sauti kuhakikisha mkopo mpya wa Benki ya Dunia unahakikisha watoto wa kike wanaopata uja uzito shuleni wanaendelea na masomo kwenye shule rasmi. Nawashukuru Benki ya Dunia kwa kusikiliza maoni ya wananchi.”
Naye, mwanaharakati wa haki za binadamu na mwanasheria maarufu Tanzania, Fatma Karume amesema kupitia mkopo huo ni dhahiri kuwa Serikali imeridhia kumrudisha kila mtoto shule wakiwemo wasichana wanaopata mimba.
Hata hivyo, akitoa maoni yake katika mtandao wa Twitter amesema wataendelea kufuatilia kwa karibu kama Serikali itatekeleza suala hilo ili kuhakikisha fedha zilizotolewa zinatumika kama zilivyokusudiwa.
Latest
