AfDB yaipatia Serikali mkopo wa zaidi ya Sh589 bilioni
- Ni baada ya Serikali kusaini mkopo wenye thamani ya takriban bilioni 589.3 ili kujenga barabara ya Kabingo-Kasulu-Manyovu yenye Kilomita 260 kwa kiwango cha lami na kuboresha miundumbinu ya huduma za jamii.
- Itapunguza gharama zingine za usafirishaji na uboreshaji wa upatikanaji wa miundombinu ya huduma za kijamii na kiuchumi kwenye maeneo ya mradi mkoani Kigoma.
Dar es Salaam. Huenda adha ya barabara inayowakabili wakazi wa Kabingo, Kasulu na Manyovu mkoani Kigoma ikatoweka hivi karibuni baada ya Serikali kusaini mikataba miwili ya mkopo wenye masharti nafuu yenye thamani ya Dola za Marekani 256.2 milioni (Sh589.3) bilioni na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB).
Mkopo huo, utakaotolewa na benki hiyo kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya Kabingo-Kasulu-Manyovu (Kilomita 260) kwa kiwango cha lami na uboreshaji wa miundombinu ya huduma za jamii.
Akizungumza baada ya kusaini mikataba hiyo, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Doto James amesema benki hiyo imekuwa ni mshirika wa muda mrefu wa Serikali katika maendeleo ya miundombinu na uwekezaji wake umekuwa wenye ufanisi na matokeo ya kuridhisha.
Hadi sasa, kwa mujibu wa wizara hiyo, AfDB imeshaikopesha Tanzania zaidi ya Dola za Marekani 1.9 bilioni (Sh4.37 trilioni), kwa ajili ya kutekeleza ujenzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo miundombinu ya barabara, maji, nishati ya umeme, elimu, na ujenzi wa masoko ya kisasa.
“Barabara ya Kabingo-Kasulu-Manyovu ni kiunganishi muhimu katika maendeleo na uboreshaji wa biashara ndani na nje ya nchi. Mradi wa ujenzi wa barabara hii utakwenda sambamba na ujenzi wa barabara ya Rumonge – Gitaza (Kilomita 45) nchini Burundi ili kuboresha mtandao wa barabara za Afrika Mashariki,” amesema James katika taarifa iliyotumwa na Wizara ya Fedha na Mipango.
Makabidhiano ya mkataba kwa ajili ya ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami kati ya benki ya AFDB na serikali ujenzi wa barabara ya Kabingo-Kasulu-Manyovu (Kilomita 260) kwa kiwango cha lami na uboreshaji wa miundombinu ya huduma za jamii.
Utekelezaji wa mradi wa Barabara wa Kabingo – Kasulu – Manyovu ni sehemu ya mkakati wa Serikali ambao unalenga kuimarisha miundombinu ya usafiri ili kuchochea kasi ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii, kupunguza umasikini na kuimarisha ushirikiano wa kikanda.
James, ambaye ni Mlipaji Mkuu wa Serikali, amesema ujenzi wa barabara hiyo utakapokamilika utaunganisha Bandari ya Dar es Salaam na mikoa ya magharibi mwa Tanzania na kufungua masoko ya kikanda nchini Burundi, Rwanda, Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Amesema mradi huo utachangia katika kupunguza gharama za uendeshaji magari, kuboresha usalama wa barabara, kupunguza gharama zingine za usafirishaji na uboreshaji wa upatikanaji wa miundombinu ya huduma za kijamii na kiuchumi kwenye maeneo ya mradi mkoani Kigoma.
Inayohusiana: Usafiri, ubora wa bidhaa: Vizuizi ukuaji biashara mtandaoni Tanzania
Sehemu nyingine ya mkopo huo itatumika katika uboreshaji wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) ili kifikie hadhi ya kituo cha umahili wa usalama barabarani katika Kanda ya Afrika Mashariki na Ujenzi wa Kituo cha Pamoja cha Forodha katika Mpaka wa Manyovu (Tanzania) / Mugina (Burundi).
Pia, fedha hizo zitatumika kuboresha miundombinu ya huduma za kijamii ikiwa ni pamoja na ukarabati wa masoko na usambazaji wa maji na usafi wa mazingira.
Mwakilishi Mkazi wa AfDB Dk Alex Mubiru ameishukuru Serikali Tanzania kwa kutekeleza kikamilifu miradi inayofadhiliwa na benki hiyo na kuongeza kuwa mradi wa ujenzi wa barabara hiyo utaipa fursa za kiuchumi Kigoma na nchi jirani ya Burundi.
Dk Mubiru amesema itaendelea kushirikiana na Serikali ya ili kutekeleza miradi mbalimbali ya kimaendeleo kwa faida ya benki hiyo na wananchi kwa ujumla.