Fedha za Benki ya Dunia zitakavyoinua elimu Tanzania

February 22, 2022 5:40 am · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni mkopo wa Sh1.5 trilioni utakaoboresha elimu ya msingi.
  • Pia utatumika kuimarisha usalama wa umiliki wa ardhi nchini.

Dar es Salaam. Huenda elimu ya msingi nchini Tanzania ikapata msukumo mpya ikiwemo wanafunzi kupata elimu bora yenye manufaa, baada ya Benki ya Dunia kutoa fedha kwa ajili ya kuboresha elimu hiyo. 

Tanzania na Benki ya Dunia zimetiliana saini mikataba miwili ya mkopo wenye masharti nafuu wenye thamani ya Dola za Marekani milioni 650 sawa na Sh1.5 trilioni kwa ajili ya kugharamia utekelezaji wa mradi wa kuboresha elimu ya msingi (BOOST) na mradi wa kuimarisha usalama wa umiliki wa ardhi nchini.

Mikataba hiyo imesainiwa Februari 21,2022 Jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu na Mlipaji Mkuu wa Serikali kutoka Wizara ya Fedha na Mipango, Emmanuel Tutuba kwa niaba ya Serikali na Mkurugenzi wa Benki ya Dunia nchini Tanzania, Mara Warwick.

Tutuba amesema kuwa fedha hizo zimetolewa na Benki ya Dunia kupitia mgao wa masharti nafuu wa mzunguko wa IDA 19, ambapo Dola za Marekani milioni 500 zitatumika kuboresha elimu ya msingi na kiasi kingine cha Dola za Marekani milioni 150 kitatumika kuimarisha usalama wa milki za ardhi hapa nchini.

Miradi iliyo chini ya mikataba iliyosainiwa inatekeleza Mpango wa Tatu wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2021/22–2025/26) na ni sehemu ya ajenda kuu ya Serikali inayolenga kujenga uchumi shindani wa viwanda kwa maendeleo ya watu kupitia mikakati mbalimbali.

Katika sekta ya elimu ya msingi, fedha hizo zitatumika kuboresha na kusimamia mazingira shirikishi ya kufundishia na kujifunzia, kuboresha uwezo wa walimu, kukuza na kuhamasisha matumizi ya Tehama katika shule za awali na msingi.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Emmanuel Tutuba (kulia) na Mkurugenzi wa Benki ya Dunia nchini Tanzania  Mara Warwick , wakibadilishana hati za mikataba miwili ya mkopo wenye masharti nafuu wenye thamani ya Dola za Marekani milioni 650 sawa na Sh1.5 trilioni kwa ajili ya kugharamia utekelezaji wa mradi wa kuboresha elimu ya msingi (BOOST) na mradi wa kuimarisha usalama wa umiliki wa ardhi nchini. jijini Dar es Salaam. Picha| Wizara ya Fedha na Mipango.

Mradi wa BOOST unakusudia kuboresha usawa katika upatikanaji wa elimu bora ya awali na msingi kwa upande wa Tanzania Bara ukiwemo ujenzi wa vyumba 12,000 vya madarasa pamoja na vifaa vinavyohitajika vya elimu; usimikaji wa mifumo na usambazaji wa vifaa vya Tehama katika shule na vyuo vya ualimu 800 kwa pamoja; na kuongeza uandikishaji wa wanafunzi kwa shule za awali na msingi.  

Tutuba amesema kuwa katika sekta ya ardhi, kazi zitakazofanyika ni kukuza na kuwezesha upangaji, upimaji na utoaji hatimiliki za ardhi kwa ajili ya uwekezaji na usalama wa makazi ya watu, kuboresha na kuongeza mfumo unganishi wa taarifa za usimamizi wa ardhi na kukuza matumizi ya Tehama katika upimaji na uandaaji wa hatimiliki ya ardhi.

“Mradi huu unatarajia kunufaisha nchi kupitia ongezeko la usalama wa umiliki katika wilaya 40 zilizochaguliwa, kwa kutoa hati za Kimila ya Kumiliki Ardhi Vijijini (CCROs), hati za Kumiliki Ardhi Mijini (CROs) na Leseni za Makazi,” amesema Tutuba.

Aidha, mradi utaongeza ufanisi wa usimamizi wa taarifa za ardhi kupitia uboreshaji wa Mfumo wa Kidijitali wa Taarifa za Ardhi (ILMIS) na utengenezaji wa ramani za msingi (Base Maps). 

Amewaagiza Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dk Allan Kijazi na Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Eliamani Sedoyeka wakasimamie ukamilishaji kwa masharti yote ya awali (conditions of effectiveness) kwa wakati ili kuwezesha kuanza rasmi kwa utekelezaji wa miradi hiyo miwili.

Benki ya Dunia imekuwa mshirika muhimu katika kufanikisha miradi mbalimbali ya kijamii nchini kwa kutoa misaada na mikopo yenye masharti nafuu ili kuboresha maisha ya Watanzania.


Soma zaidi:


Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Dunia nchini Tanzania, Mara Warwick amesema kuwa Tanzania imepiga hatua kubwa katika kuboresha elimu na kwamba fedha zilizotolewa na benki hiyo kama mkopo nafuu zitawanufaisha zaidi ya wanafunzi 12,000 wanaosoma masomo ya awali na elimu ya msingi.

Amesema mkopo wa dola za Marekani milioni 150 utawanufaisha zaidi ya wananchi milioni 2 hususan waishio vijiji kwa kupatiwa hatimiliki za kimila zaidi ya 500,000 kwenye mikoa 14 yenye wilaya 40.

Kusainiwa kwa mikataba hiyo miwili kumefanya kiwango fedha kilichowekezwa na Benki ya Dunia hapa nchini kufikia Dola za Marekani bilioni 6.15 (Sh14.3 trilioni) kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika sekta mbalimbali.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW