Benki Kuu yatoa maagizo kwa watoa huduma ndogo za fedha

January 3, 2020 7:56 am · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link
  • Yapiga marufuku mtu au taasisi kutoa huduma ndogo za fedha bila kujisajili.
  • Atakayekiuka kukabiliwa na adhabu kali. 
  • Yaanza kutumia Kanuni za Udhibiti na Usimamizi wa Huduma Ndogo za Fedha kulingana na madaraja tofauti ya watoa huduma hizo.

Dar es Salaam. Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imesema kuwa ni marufuku kwa mtu au taasisi yoyote kufanya biashara ya kutoa huduma ndogo za fedha bila kuwa na leseni au usajili na adhabu kali itatolewa kwa atakayekiuka sheria. 

Katika taarifa iliyotolewa na BoT Januari 2, 2020, inasisitiza kuwa kwa mujibu wa Kifungu cha 16 cha Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha ya Mwaka 2018, ni marufuku kwa mtu au taasisi yoyote kufanya biashara ya kutoa huduma ndogo za fedha bila kuwa na leseni au usajili uliotolewa na BoT au mamlaka zilizokasimishwa.

“Adhabu kali itatolewa kwa mtu au taasisi yoyote itakayokiuka Sheria hii,” inaeleza sehemu ya taarifa iliyotolewa na BoT jana.

Imesema watoa huduma wote katika sekta ya huduma ndogo za fedha wanatakiwa kuwasilisha maombi ya leseni au usajili Benki Kuu ya Tanzania au kwenye Mamlaka zilizokasimishwa katika kipindi cha miezi 12 baada ya Sheria kuanza kutumika, yaani Novemba 1, 2019. 

BoT imeeleza kuwa watoa huduma wanapaswa pia kukidhi matakwa mengine ya Kanuni za Udhibiti na Usimamizi wa Huduma Ndogo za Fedha ambazo kulingana na madaraja tofauti yaliyoainishwa kwenye Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha ya Mwaka 2018. 

“Pamoja na mambo mengine, kanuni hizi zinagusia vigezo vya utoaji wa leseni, mitaji na utawala wa taasisi ndogo za fedha,” inaeleza sehemu ya taarifa hiyo. 


Zinazohusiana:


Watoa huduma ndogo za fedha wanahimizwa kuwasilisha maombi ya leseni ya Benki Kuu katika kipindi kilichotolewa na Sheria kama ifuatavyo: watoa huduma ndogo za fedha walio katika Daraja la 2 wawasilishe maombi yao ya leseni Benki Kuu ya Tanzania Makao Makuu au katika matawi yake. 

Pia watoa huduma ndogo za fedha walio katika daraja la 3 wanatakiwa kuwasilisha maombi yao ya leseni kwenye Ofisi ya Ushirika ya Wilaya au Mrajisi wa Vyama vya Ushirika wa Mkoa, huku wale wa daraja la 4 watawasilisha maombi ya kuandikishwa katika Ofisi ya Serikali ya Mtaa iliyokaribu. 

Sheria hiyo ambayo ilipitishwa bungeni Novemba 16, 2018 inazihusu taasisi kama vile Vyama vya Ushirika wa Akiba na Mikopo (SACCOS), Taasisi za huduma ndogo za fedha zisizopokea na zinazopokea amana na vikundi vya kifedha vya kijamii, wakopeshaji binafsi na asasi za kijamii.

Enable Notifications OK No thanks