BoT yaeleza sababu za kutumia jeshi kukagua maduka ya ubadilishaji fedha Arusha

Daniel Samson 0705Hrs   Novemba 20, 2018 Biashara
  • Imesema iliwatumia askari wa JWTZ katika operesheni hiyo kwa sababu askari wengi wa Jeshi la Polisi walikuwa wakisimamia usalama katika vituo vya mitihani ya kidato cha pili inayoendelea nchini. 
  • Hiyo ni operesheni ya tatu baada mbili za awali kushindwa kutokana na wahusika kuwa na mtandao mpana wa kuratibu biashara haramu ya fedha.
  • Pia imesitisha utoaji wa leseni za biashara ya ubadilishaji fedha na kusimamisha upokeaji wa maombi mapya mpaka taratibu mpya za uendeshaji wa biashara hiyo zitakapokuwa tayari.

Dar es Salaam. Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imesema ililazimika kutumia askari wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) katika oparesheni ya kukagua maduka ya ubadilishaji fedha jijini Arusha Jumatatu hii kutokana na askari wengi wa Jeshi la Polisi kuwa katika usimamiaji wa usalama katika vituo vya mitihani ya kidato cha pili wakati ukaguzi huo ukifanyika. 

Sambamba na hilo BoT imesitisha utoaji wa leseni za biashara ya ubadilishaji fedha kwa takribani miezi mitatu sasa na kusimamisha upokeaji wa maombi mapya mpaka taratibu mpya za uendeshaji wa biashara hiyo zitakapokuwa tayari.

Kauli hiyo inakuja siku moja baada ya kuonekana kwa askari wa JWTZ katika maduka ya kubadilisha fedha Jijini Arusha, jambo lililoibua mjadala na sintofahamu ya jeshi hilo kuhusika katika shughuli ambazo zilipaswa kufanywa na taasisi husika.

Taarifa ya Gavana wa BoT, Prof Florens Luoga iliyotolewa leo (Novemba 20, 2018) kwa wanahabari imeeleza kuwa oparesheni hiyo ya kushtukiza imelenga kukagua maduka ya ubadilishaji fedha na baadhi ya maduka bubu ambayo hayana leseni lakini yalikuwa yakiendesha biashara hiyo kinyume na sheria.

Zoezi hilo, kwa mujibu wa Prof Luoga, liliratibiwa na Kitengo cha Ukaguzi cha Benki Kuu kwa kushirikiana na vyombo vingine vya Dola.

"Baadhi ya washiriki katika zoezi hilo ni askari wa Jeshi la Wananchi Tanzania wakiwa katika sare zao bila silaha. Hii ni kwa sababu siku oparesheni ilipofanyika askari wengi wa Jeshi la Polisi wapo kwenye kusimamia usalama katika vituo vya mitihani ya kidato cha pili inayoendelea," imeeleza sehemu ya taarifa hiyo. 


Soma zaidi:


Prof Luoga amesema oparesheni hiyo ni ya tatu kufanyika ambapo uchunguzi wa kina katika miezi sita iliyopita ulibaini kuongezeka kwa biashara za kubadilisha fedha kinyume cha sheria, na kukua kwa biashara haramu ya fedha za kigeni na utakatishaji fedha ambayo kwa sehemu kubwa inafanyika katika maduka hayo. 

"Baada ya mashauriano na wataalam na kushirikisha vyombo vya upelelezi na usimamizi ilionekana kuwa ili
kufanikisha zoezi lililokusudiwa ni muhimu wahusika wote wadhibitiwe kwa wakati mmoja na kufanyiwa ukaguzi," imeeleza ripoti hiyo.

Prof Luoga ameeleza kuwa juhudi za Kitengo cha Ukaguzi kutoka BoT kuwapata wahusika hazikuzaa matunda katika oparesheni mbili zilizopita, jambo lililowafanya waongeze nguvu ya ziada ikiwemo kuwatumia maafisa wengi kutoka vyombo mbalimbali ili kuhakikisha usalama wa kutosha na wananchi wanaarifiwa kutoingia sehemu husika kwa wakati huo.

"Napenda kuwaarifu Wananchi kuwa oparesheni hii imeisha salama na bila kuathiri mtu yeyote na tunawashukuru Wananchi wa Jiji la Arusha kwa ushirikiano, hasa kwa kuwa watulivu. Taratibu zinazoendelea ni za kisheria. Wale watakaokutwa na tuhuma za ukiukaji sheria watashughulikiwa kufuatana na taratibu za kisheria," amesema Prof Luoga katika taarifa hiyo.

Askari wa JWTZ akiwa katika moja ya duka la kubalisha fedha Jijini Arusha Jumatatu wakati BOT wakiendesha zoezi la ukaguzi wa leseni na kuwabainibi watu wanaofanya biashara haramu ya fedha za kigeni. Picha| JamiiForums.

Hata hivyo, BOT imesema katika kipindi hiki wakati kesi za watuhumiwa wa utakatishaji na fedha haramu zinashughulikiwa leseni zao zinasitishwa na wanatakiwa kuzirudisha benki kuu mpaka kesi zao zitakapokamilika na taratibu mpya zitakapoanza kutumika.

Maelekezo hayo yanawahusu pia wote waliopatikana na tuhuma za ukiukaji sheria katika oparesheni mbili zilizopita na kufikishwa polisi ambao nao wanatakiwa kurejesha leseni zao BoT na kwamba zinasitishwa mpaka kesi zao zitakapokamilika.

"Wale ambao wanaendesha maduka ya kubadilisha fedha bila leseni au kwa kutumia leseni zisizo zao wanatakiwa kufunga maduka hayo mara moja kabla hawajafikiwa na mkono wa sheria," amesema.

Hata hivyo, Prof Luoga hakuweka bayana idadi wala majina ya watuhumiwa waliokamatwa huku akieleza kwenye taarifa hiyo kuwa "kwa vile operesheni hii inaingia katika hatua za kisheria zinazoweza kupelekea baadhi ya watuhumiwa kupelekwa mahakamani, benki kuu haitaendelea kutoa taarifa zinazohusu wahusika kwa sababu kufanya hivyo kunaweza kupelekea kuingilia uhuru wa mahakama."

Related Post