Bandari ya Dar es Salaam kubeba mizigo tani milioni 25 ifikapo 2021

September 17, 2019 1:48 pm · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link
  • Hiyo ni baada ya kukamilika kwa ukarabati wa magati nane kati ya 12. 
  • Gati namba moja na gati namba mbili yamekamilika na yanatumiwa na meli kutoa huduma kama kawaida.
  • Kwa sasa ukarabati wa gati namba sifuri ambayo ni maalum kwa meli za mizigo ya magari uko katika hatua za mwisho.

Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imesema ukarabati wa magati nane ya bandari ya Dar es Salaam utakapomilika utaiongezea bandari hiyo ufanisi zaidi na kuiwezesha kubeba mizigo ya tani milioni 25 kwa mwaka ifikapo 2021. 

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe aliyekuwa akizungumza wakati alipotembelea na kuona meli kubwa ya mizigo ya magari ya kampuni ya Meli ya Mv Grand Duke iliyotua bandarini hapo, amesema kwa sasa bandari hiyo inabeba mizigo tani milioni 17 kwa mwaka. 

“Malengo yetu ni kufikia tani milioni 25 kwa mwaka 2021 tofauti na tani za sasa milioni 17, kwa hiyo nchi wanachama wa SADC, bandari hii sasa inafanya kazi vizuri, kwa hiyo majirani zetu kutoka DRC, Malawi, Zambia na nchi zingine za ukanda huu wa Kusini mwa Afrika  wanakaribishwa sana kutumia Bandari ya Dar es Salaam,” amesema Kamwelwe.

Gati namba moja na gati namba mbili zimekamilika na zinatumiwa na meli kutoa huduma kama kawaida na sasa ukarabati wa gati namba sifuri ambalo ni maalum kwa meli za mizigo ya magari nao umekamilika.

Tayari gati namba sifuri limeanza kupokea meli ambapo mwishoni mwa wiki iliyopita meli kubwa ya mizigo ya magari ya kampuni ya Meli ya Mv Grand Duke iliyotua bandarini hapo jana.

Meli hiyo yenye urefu wa mita 200 na uwezo wa kubeba magari 6,000  ilitia nanga, jambo ambalo Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) inasema bandari hiyo sasa ipo tayari kupokea mizigo mikubwa.

Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Mhandisi Deusdedit Kakoko amesema kuwa gati  jipya namba sifuri lina uwezo wa kubeba  magari 10,000 kwa wakati mmoja kutoka uwezo wa kubeba magari 2,500 ambao ulikuwa nao hapo awali.  Kiwango hicho ni mara nne zaidi ya uwezo wake wa awali. 

Gati hilo ambalo ni la kisasa litakuwa na taa ambazo zitawezesha kufanyika kazi usiku na mchana hapo bandarini. 


Zinazohusiana:


Bandari hiyo, iliyopo katika mwambao wa Bahari ya Hindi, ina gati 12 za kuhudumia shehena za aina mbalimbali za mizigo, ikiwa ni pamoja na shehena ya mizigo mchanganyiko, makasha na mafuta.

Nchi za Jamhuri ya Demokrasi ya Kongo (DRC), Zambia, Rwanda, Burundi, Malawi, Uganda, Zimbabwe, Comoro hutumia bandari hiyo kuingiza na kuuza bidhaa zao nje ya nchi. 

Katika kuongeza ushindani wa bandari katika nchi za kusini mwa Afrika, uongozi wa bandari hiyo unaendelea na upanuzi wa lango ambalo meli zinaingilia kutoka mita 150 za sasa hadi mita 170. 

Pia kina cha maji cha kati ya mita 10.5 hadi 11 kinaongezwa hadi kufikia mita 15 huku usalama wa mizigo ukiimarishwa. 

Enable Notifications OK No thanks