Usiyoyajua kuhusu biashara ya Forex

January 9, 2025 5:42 pm · Kelvin Makwinya
Share
Tweet
Copy Link
  • Neno Forex limetokana na kufupishwa kwa maneno Foreign Exchange Trading yenye maana biashara ya kubadili fedha za kigeni.
  •  Inatajwa kuwa ndio soko kubwa zaidi la kifedha duniani, likifanya kazi saa 24 na siku saba za wiki.

Dar es Salaam. Huenda umewahi kusikia neno ‘Forex’, na huenda kila mmoja akawa na tafsiri yake anapoliona ama kulisikia, kwa baadhi wa watu neno hilo wanalihusianisha na utapeli kwa kuwa linawakumbusha maumivu ya kupoteza kiasi fulani cha pesa huku kwa watu wengine ni biashara au kazi inayowaendeshea maisha.

Ukosefu wa elimu au taarifa sahihi ya kuhusu ‘Forex’ umeathiri maamuzi ya watu wengi ambao wapo katika kundi la kwanza la waliotapeliwa, kuibiwa, au kupoteza fedha zao.

Kwa kuwatumia wataalamu na vyanzo aminika, makala hii inaangazia maana ya Forex, jinsi inavyofanya kazi, mambo ya kuzingatia pamoja na msimamo wa Serikali kuihusu ili ufanye maamuzi ukiwa na taarifa sahihi tangu umeisoma makala hii.

‘Forex’ ni nini?

Fikiri hivi, unahitaji pesa ya Marekani na wewe una Shilingi ya Tanzania, hivyo ni lazima utakwenda benki au katika maduka ya kubadili fedha kununua Dola ya Marekani kwa kiwango unachotaka, unawapa Shilingi wanakupa Dola hiyo ndio Forex.

Jambo muhimu la kuzingatia ni kuwa neno Forex limetokana na kufupishwa kwa maneno Foreign Exchange Trading yenye maana biashara ya kubadili fedha za kigeni.

Kituo cha mafunzo ya fedha na uwekezaji cha Investopedia kinatafsiri Forex kama mchakato wa kubadilisha sarafu moja na nyingine kwa madhumuni ya biashara na uwekezaji. 

Sasa basi biashara hii hufanyika kwa namna tofauti ikiwemo kupitia benki, maduka ya kubadili fedha (bureau de Change) au mtandaoni ambako ndiko tutajikita kwa leo.

Neno Forex limetokana na kufupishwa kwa maneno Foreign Exchange Trading yenye maana biashara ya kubadili fedha za kigeni. Picha | Bing.com

Forex inatajwa kuwa ndio soko kubwa zaidi la kifedha duniani, likifanya kazi saa 24 na siku saba za wiki  ikihusisha kusimamia kiasi kikubwa cha miamala ya kifedha kila siku.

Investopedia wanaeleza kuwa wafanyabiashara wa Forex hupata faida kwa kununua sarafu wakati thamani yake ikiwa chini na kuuza wakati thamani inapanda, wakitumia tofauti ya viwango vya ubadilishaji wa sarafu ambavyo hubadilika mara kwa mara.

Yaani mfanyabiashara anaweza kununua Dola ya Marekani kwa Sh2,450 kisha akaiuza kwa Sh2,500, hapo atakuwa amepata faida ya Sh50 kwa kila dola aliyouza kutegemeana na namna viwango vilivyo.

Katika jitihada za kujikwamua kiuchumi baadhi ya vijana nchini Tanzania wamejaribu kuitumia Forex kama daraja, hata hivyo si wote wamefanikiwa kutokana na aidha kutokuwa na taarifa sahihi tangu awali au kutofuata taratibu na misingi ya Forex.

Unawezaje kutengeneza pesa kupitia Forex?

Investopedia wanaeleza kuwa kutengeneza pesa kupitia biashara ya forex ni zaidi ya kununua na kuuza sarafu, kunahitaji mbinu, mikakati, nidhamu, na usimamizi wa karibu. 

Ingawa kuna uwezekano wa kupata faida, ni muhimu kuelewa kuwa biashara ya forex si mpango wa kupata utajiri wa haraka kama wengi wanavyodhani.

Njia kuu ya wafanyabiashara kupata pesa katika forex ni kwa kutabiri kwa usahihi mwelekeo wa bei za sarafu ambao hubadilika mara kwa mara.

Forex inatajwa kuwa ndio soko kubwa zaidi la kifedha duniani, likifanya kazi saa 24 na siku saba za wiki  ikihusisha kusimamia kiasi kikubwa cha miamala ya kifedha kila siku. Picha | Forexinvesting.org

Njia nyingine ya kupata faida ni kupitia ‘carry trading,’ ambapo unapata faida kutokana na tofauti za viwango vya riba kati ya sarafu mbili. Kwa kununua sarafu yenye kiwango cha juu cha riba huku ukiuza ile yenye kiwango cha chini, unaweza kupata tofauti ya viwango hivyo.

Kwa mfano, ukinunua Dola za Australia (zikiwa na kiwango cha riba cha 4%) ukitumia Yen za Japani (zikiwa na kiwango cha riba cha 0.1%), unaweza kupata karibu 4% kila mwaka, pamoja na mabadiliko yoyote mazuri ya kiwango cha ubadilishanaji.

Hii ni sehemu ya kwanza, usikose kusoma sehemu ya pili itakayoangazia hatua za kufanya biashara ya Forex kwa mafanikio.

Je wewe umewahi kujihusisha na Forex? Tuandikie maoni kwenye namba yetu ya WhatsApp 0750881888

1 thought on “Usiyoyajua kuhusu biashara ya Forex

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks