Ahueni: Wazazi wachekelea vifaa vya shule vikishuka bei Mwanza
- Vifaa vingi vyaendeea kuuzwa kwa bei iliyokuwepo mwaka jana.
- Wazazi wasema imewasaidia kupata ahueni ya kiuchumi.
Mwanza. Zikiwa zimebaki siku chache kabla ya kuanza kwa muhula mpya wa masomo kwa wanafunzi wa shule za msingi na Sekondari nchini Tanzania kwa mwaka 2025, wazazi mkoani Mwanza wamebanisha kupata ahueni baada ya kutopanda kwa bei ya vifaa vya shule.
Mara nyingi kutokana na kuongezeka kwa wahitaji, wafanyabiashara hupandisha bei ya mahitaji ya wanafunzi jambo linalowalazimu wazazi kutoboa zaidi mifuko yao na wakati mwingine hukwamisha baadhi ya familia kupata mahitaji hayo hususan zinazotoka katika kipato cha chini.
Uchunguzi wa mwanahabari wa Nukta umebaini hali imekuwa tofauti kwa mwaka 2025 ambapo licha ya kuwa tayari wanafunzi wa kidato cha kwanza wameanza kuwasili katika shule mbalimbali mkoani Mwanza, bei ya vifaa vya shule imeendelea kusalia ile ile iiyokuwepo mwaka jana.
Mathalani, bei ya daftari ya ‘msomi’ imeendelea kusalia kuwa Sh700 huku zile kubwa za ‘counter book’Q2 nayo ikisalia kuwa Sh2,000 bei iliyokuwepo mwaka 2024.
Aidha, sare za shule nazo bei imeendelea kubaki vile vile kwa upande wa sare za shule kama shati, sketi na kaptura, bei imebaki kuwa ile ya mwaka jana ambapo kwa bei ya jumla shati zinaanzia Sh1,400 hadi Sh1,800 wakati kwa bei ya reja reja inauzwa Sh2,000 hadi Sh2,500.
Mmoja wa wafanyabiashara Jijini Mwanza, Anitha Samson amesema sare zinauzika kwa wingi na hakuna mabadiliko yoyote yaliyotokea.
Hata hivyo, bei za viatu vya wanafunzi bei imeendelea kuwa juu ambapo vinapatikana kuanzia Sh20,000.
Baadhi ya wazazi Jijini Mwanza wamesema bei ya vifaa hivyo haijapanda kama walivyokuwa wanatarajia badala yake wameenda sokoni na kukuta bei ni ya kawaida.
Elisha Manjala baba wa watoto wanne mkazi wa Nyakato Mwanza, amesema wakati anatoka nyumbani kwenda kununua vifaa hivyo alikuwa na hofu ya kupanda kwa vifaa hivyo, lakini baada ya kufika sokoni amekuta bei ni ya kawaida.
“Bei kwa mwaka huu ni rafiki sana kwa sisi wazazi, mfano daftari ya msomi ni Sh700, kauntabook Sh2, 000 na kalamu 10 Sh1, 000 kwahiyo ni bei rafiki kabisa kwa mzazi yoyote,”amesema Manjala.
Pamoja na vifaa hivyo kuwa rafiki, Johari Hassan mfanyabiashara wa viandikwa pamoja na vifaa vya shule ameiambia Nukta Habari kuwa kuna wasiwasi wa kupanda bei ya karatasi nyeupe maarufu kama ‘rim paper’ kutokana na upatikanaji wake kutotabirika.
“Karatasi nyeupe hasa ‘Double A’ huwa chagamoto misimu yote, mwaka jana (2024) tuliuza mpaka Sh20,000 bunda moja, hatujajua kama itapanda au itabaki bei hii hii, kwa sasa tunauza Sh16,000 mpaka Sh17,000,2 amesema Hassan.
Bunda la karatasi huhitajika hasa kwa wanafunzi wanaosoma shule za sekondari kwa ajili ya kufanyia mitihani ya ndani ya shule.