Fahamu vipimo vya afya unavyotakiwa kupima kabla ya ndoa

January 9, 2025 2:52 pm · Fatuma Hussein
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni pamoja na  kupima VVU, kundi la damu pamoja na hali ya ngozi.
  • Husaidia  kila mshirika, kugundua magonjwa ya kuambukiza, na kuandaa wenza kwa afya bora ya uzazi.

Dar es Salaam. Kupata mwenzi na kufunga nae ndoa ni ndoto ya walio wengi, kwa kuwa ni hatua chanya inayoashiria mwanzo mpya wa maisha ya mtu husika kijamii.

Pamoja na kwamba mahusiano na ndoa hutajwa kama jambo la baraka, wakati fulani inaweza kuwa chanzo cha huzuni, majuto, pamoja na simanzi kwa wahusika ikiwa hawakufuata baadhi ya mambo muhimu yanayoshauriwa na wataalamu ikiwemo kupima afya.

Wataalamu wa afya wanashauri ni muhimu kwa watu waliopo kwenye mahusiano wakitarajia kufunga ndoa kufanya baadhi ya vipimo ili kutathmini hali ya afya ya kila mshirika, kugundua magonjwa ya kuambukiza, na kuandaa wenza kwa afya bora ya uzazi.

Wakati msukumo mkubwa ukiwekwa kwenye kupima maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU) pekee inashauriwa kupima vipimo vingine ambavyo  husaidia kutambua hatari za magonjwa ya kijenetiki ambayo yanaweza kurithiwa na watoto wa baadaye.

Tovuti ya Tirta Medical center  inaeleza kuwa kuwa vipimo hivyo vina faida nyingi ikiwa ni pamoja na kugundua magonjwa ya kuambukiza, magonjwa ya kurithi, na kujiandaa kwa uzazi wenye afya.

Kwa mujibu wa Dk Lilian Benjamin, Mkurugenzi wa Shirika la DARE, vipimo vinavyopaswa kufanyika kabla ya ndoa vinajumuisha kundi la damu, hali ya maambukizi ya virusi vya Ukimwi, magonjwa yanayoambukizwa kwa njia ya ngono, na magonjwa ya kijenetiki.

Kundi la Damu na ‘Rhesus  factor’ (Rh factor)

Kupima kundi la damu na Rh factor ni muhimu ili kuzuia matatizo ya ujauzito, hasa ikiwa mama na kijusi wanakuwa na Rh tofauti.

 Rhesus factor ni Protini inayopatikana kwenye chembe nyekundu za damu ambayo hufanya makundi ya damu kuwa na makundi tofauti kama vile A+, A-, B+, B-, O+, O-, AB+, na AB-

Kugundua ufanano wa damu husaidia kuepuka matatizo ya ujauzito. Picha / Stanford blood center.

“Mmoja akiwa na Rhesus hasi (Rh-) na mwingine Rhesus chanya (Rh+), inaweza kusababisha changamoto za ujauzito wa baadaye, ikiwa ni pamoja na kuharibika kwa mimba,” amesema Dk Benjamin.

Dk Benjamin ameongeza kuwa njia za kinga kama sindano za kinga wakati wa ujauzito zinaweza kutumika kuhakikisha usalama wa mama na mtoto.

Kupima VVU

Dk Benjamin amesisitiza kuwa wenza wanapaswa kupima hali yao ya maambukizi ya VVU mara kwa mara, kabla na hata baada ya ndoa.

“Haimanishi haumuamini mwenza wako, lakini kupima mara kwa mara, kama kila miezi mitatu au sita, ni muhimu kwa afya ya wote,” amebainisha Dk Benjamini.

Ameonya dhidi ya kuchelewesha vipimo hadi ‘window period,’ kipindi ambacho maambukizi hayawezi kugundulika.

Dk Benjamini amesisitiza kuwa haijalishi uaminifu uliopo kati ya wenza hakuna mwenye kujua akili ya mtu pale wanapopeana migongo hivyo kupima ni muhimu.

Kupima afya mara kwa mara ni muhimu kwa afya ya wenza wote. Picha / Canva.

Hata hivyo, kupima VVU ni muhimu kwa sababu kunaathiri maisha yako na ya wengine kwa njia tofauti lakini pia kuna kupa muelekeo wa kufanya maamuzi sahihi juu ya maisha yako.

Sio hivyo tu, pia kutakusaidia kuzuia kuwaambukiza wengine, kupata matibabu ya haraka ikiwa umegundulika mapema, kuilinda familia yako, kujua njia bora za kujikinga na VVU na kuwakinga wanaokuzunguka.

Kupima magonjwa yanayoambukizwa kwa njia ya ngono

Dk Benjamin amebainisha kuwa, yapo magonjwa yanayoambukizwa kwa njia ya ngono kama vile kaswende, kisonono, hepatitis B, Hpv (Human Papillomavirus) ni magonjwa ambayo watu wengi huyapuuza bila kujua umuhimu wake katika afya za weza.

“Watu wengi hupuuzia magonjwa haya wakisubiri dalili, jambo linaloweza kusababisha matatizo makubwa ya kiafya,” amesema Dk Benjamin, akisisitiza kuwa vipimo hivi ni muhimu kwa wenza wote wawili.

Kupima magonjwa yanayoambukizwa kwa njia ya ngono inaweza kukusaidia kumchagua mwenza ambaye atafaa kwa familia. Picha / Adobe stock.

Dk Benjamin pia amesisitiza kuwa suala la kupima magonjwa haya ni bora zaidi likawahusisha weza wote na sio mwanamke mwenyewe.

Kutokupima magonjwa haya mapema kunaweza kusababisha wenza kupata matatizo ya ugumba au kansa ya shingo ya uzazi kwa wanawake.

Sanjari na matatizo hayo, athari nyingine ni pamoja na mimba kutoka au kuzaliwa kwa mtoto njiti, maumivu ya muda mrefu sehemu nyeti na kupoteza maisha iwapo hatua stahiki hazitachukuliwa.

Kupima seli mundu (sickle cell)

Vipimo vya magonjwa ya kurithi kama vile seli mundu (Sickle cell) vinahitajika ili kuepuka matatizo kwa watoto watakaozaliwa.

Kwa mujibu wa Dk Deogratias Soka mtaalamu wa afya na mtafiti kutoka Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi za Tiba cha Muhimbili (MUHAS) amebainisha kuwa kipimo cha seli mundu ni kipimo muhimu kupima ili kufahamu muelekeo wa watoto.

“Watu wenye sickle cell wakioana wanaweza kupata mtoto wenye ‘sickle cell disease’ (ugonjwa wa seli mundu) hapo ndipo matatizo makubwa sana yanapoanzia,” ameeleza Dk Soka.

Kupima vipimo vya seli mundu ni njia ya kujenga msingi wa familia yenye afya. Picha / Canva.

Hata hivyo, Dk Soka ameanisha kuwa kuna baadhi ya watu ambao wao wana vimelea vya seli mundu lakini hawajijui kitaalam huitwa ‘carrier’ na hawana dalili za ugonjwa huo, hivyo watu hawa wakioana wana uwezekano mkubwa wa kuzaa mtoto mwenye tatizo hili. 

Shirika la Afya Dunia (WHO) linaeleza kuwa takriban asilimia 5 ya watu duniani hubeba jeni za magonjwa ya haemoglobini, kama seli mundu na Thalassaemia, ambayo husababishwa na urithi wa jeni zilizoharibika kutoka kwa wazazi wote wawili. 

Kwa mujibu wa Dk Soka Tanzania ni nchi ya nne duniani kwa wa watoto wenye Seli mundu ambapo asilimia 15 hadi 20 ya watu wote wa Tanzania wanavinasaba vya ugonjwa wa seli mundu. 

Hali ya ngozi  (Albinism)

Dk Benjamin, anasisitiza kuwa ikiwa mmoja wa wenza ana vimelea vya Albinism, nafasi ya kupata mtoto mwenye hali hiyo inaongezeka zaidi, jambo ambalo linapaswa kufahamika mapema.

“Huyu mwenye Albinism akioa au akiolewa na mtu ambaye ni ‘carrier’ nafasi ya kumpata mtoto mwenye Albinism inaongezeka zaidi,” ameongeza Dk Benjamin

Vipimo vya albinism husaidia kuhakikisha afya ya watoto wa baadaye. Picha / Canva

Kwa kuhitimisha, Dk Benjamin amesisitiza kuwa vipimo vya kabla ya ndoa si dalili ya kutokuaminiana, bali ni njia ya kujenga msingi wa familia yenye afya.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks