Bado kidogo: Ukosefu wa ruzuku wakwamisha juhudi kuimarisha elimu Geita

July 16, 2021 1:40 pm · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni shule ya Sekondari ya Isebya ambayo imejengwa kwa nguvu za wananchi.
  • Inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo upungufu wa vifaa vya kujifunzia.
  • Serikali yasema itaipiga jeki kwa kuipatia fedha.

Mbogwe. Huenda wanafunzi walioanza kusoma katika Shule ya Sekondari ya Isebya mkoani Geita wakasubiri zaidi kuboreshewa huduma za elimu baada ya kuandamwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ukosefu wa ruzuku ya Serikali.

Shule hiyo iliyopo Kata ya Isebya, umbali wa kilomita 100 au mwendo wa saa mbili kwa gari binafsi kutoka katika mji mdogo wa Masumbwe wilayani Mbogwe, ilijengwa kwa nguvu ya wananchi.

Hii shule ni ya kwanza kujengwa katika kata hiyo na ilianza kuandikisha wanafunzi mwaka 2020 kwa kudahili wanafunzi kutoka katika shule nne za msingi zilizopo kwenye kata hiyo za Kiseke, Isebya, Ngerere na Lindi. 

Kujengwa na kuanza kufanya kazi kwa shule hiyo ambayo ni mkombozi kwa watoto wa Isebya kumetokana na nguvu za wananchi kuchanga fedha na kujitoa kujenga madarasa matano ambayo wanafunzi wa kidato cha I na II wanayatumia.

Baadhi ya wanafunzi wanaosoma katika shule hiyo, wanasema wana matumaini makubwa ya kutimiza ndoto zao za elimu kutokana na kusogezewa shule karibu. 

“Ilikamilishwa pale ambapo sisi tulihitimu (mwaka 2019), tunafurahi sana kuja kusomea hapa kwa sababu ni mazingira mazuri pale ambapo tunakua karibu na wazazi wanazidi kutupa ushauri mbalimbali,” anasema mwanafunzi wa kidato cha pili katika shule hiyo, Japheth Charles.

Japhet (17) ambaye ndoto yake ni kuwa daktari wa meno anasema shule hiyo iko eneo zuri ambalo “hakuna hata magari yanapiga kelele, mwalimu anapoanza kufundisha wanafunzi wengi tunakua tayari kwa ajili ya kusikiliza anachofundisha.”

Hata hivyo, huenda ndoto ya Japhet na wanafunzi wengine zikakatizwa na changamoto mbalimbali ambazo zinaikabili shule hiyo ambayo ina vyumba vya madarasa vitano ikiwemo kukosa walimu wabobezi wa masomo ya sayansi na hisabati.

Licha ya kuwa wazazi tayari wamekamilisha ujenzi wa chumba kimoja cha maabara ya sayansi, mpaka sasa Serikali haijapeleka vifaa na mtaalam wa maabara katika shule hiyo.

Changamoto hiyo inaweza kuwakwamisha wanafunzi kama Japhet wenye ndoto ya kubobea kwenye masomo ya sayansi kwa sababu wanakosa muda na mahali pa kufanyia mazoezi kwa vitendo.

Sehemu ya shule ya Isebya ambayo imejengwa kwa nguvu za wananchi. Picha Gift Mijoe.

Pia Isebya ambayo ni miongoni mwa shule 16 za sekondari za Wilaya ya Mbogwe bado haijaanza kupokea ruzuku kutoka serikalini, jambo linalofanya kukosekana kwa huduma mbalimbali ikiwemo vifaa vya kufundishia na kujifunzia. 

“Changamoto ni vifaa vya kufundishia, shule yetu bado ni changa haipati ruzuku kutoka serikalini, inajiendesha kwa mfumo wa wazazi na wadau mbalimbali wanaoipenda elimu,” anasema Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Isebya, Wambura Bhoke.

Wakati shule hiyo haipati ruzuku, ni tofauti katika shule 13 za Mbogwe ambazo zinapata fedha kutoka serikalini kwa ajili ya kuendesha shughuli zake. 

Miongoni mwa shule hizo ni Masumbwe ambayo kwa mujibu wa ripoti ya ruzuku kwa shule za sekondari kwa mwaka 2019/2020, iliongoza kwa kupata kiasi kikubwa cha ruzuku ambapo ilipokea Sh18.5 milioni katika kipindi hicho.

Kibarua kingine kilichopo ni ongezeko la wanafunzi lisiloendana na kasi ya ujenzi wa madarasa, hali inayoweza kuathiri masomo kwa wanafunzi watakaoandikishwa kidato cha kwanza mapema mwakani. 

“Changamoto iliyopo ni upungufu wa madarasa, kimsingi vyumba vya madarasa havitoshi lakini kuna hatua zinafanyika za ujenzi wa madarasa mengine,” amesema Bhoke na kubainisha kuwa, “hata hivyo bado ni changamoto vinatakiwa vyumba vingi.”

Wakati suala la madarasa likitafutiwa ufumbuzi, hamasa inahitajika kwa wazazi kuwasaidia wanafunzi kwenda shule na siyo kuwaingiza katika uchungaji wa mifugo na kilimo katika umri mdogo. 

“Walimu waliopo hawatoshi na linaendana na nyumba za walimu ni chache lakini mwamko duni, wazazi wengi bado hawajawa na uelewa wa kutosha kuhusu mambo hayo ya elimu,” anasema Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi ya Isebya, Saidi Nyoni.

Wakazi wa Isebya wameanza kujenga madarasa mengine mawili ili kuhakikisha shule ya sekonari inakidhi mahitaji ya wanafunzi. Picha| Gift Mijoe.

Manufaa ya shule hiyo

Licha ya changamoto zinazoikumba shule hiyo, wakazi wa Isebya wanaamini shule hiyo itakuwa mkombozi kwa elimu ya watoto wao.

Mwenyekiti wa Bodi Shule ya Sekondari Isebya, Sylivester Peter anasema shule hiyo yenye walimu nane wakiwemo wa kike wawili itasaidia kupunguza changamoto ya watoto wao kutembea zaidi ya kilomita tano kwa miguu na baiskeli kwenda kusoma katika Shule ya Sekondari ya Ilolangulu iliyopo kata ya jirani.

“Kusafiri umbali mrefu ndiyo ilikuwa inasababisha watoto wengi kushindwa kuendelea na masomo kwa sababu ya umbali wa shule,” anasema Peter.

Kwa wastani, kwa mujibu wa kiongozi huyo wa shule, watoto 180 waliokuwa wanaandikishwa kidato cha kwanza kwenda shule za jirani, ni takriban 40 ndiyo walikuwa wanahitimu kidato cha nne kutoka kata yake.

Anguko hilo la wanafunzi linatokana na wanafunzi kupata ujauzito na wengine kujiingiza katika makundi hatarishi kutokana na kukosa uangalizi wa wazazi kwa kupanga mitaani.

Kwa mujibu wa takwimu muhimu za elimu (BEST 2020) zilizotolewa na Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, wanafunzi 1,157 waliacha shule mwaka jana katika Halmashauri ya Mbogwe huku zaidi ya nusu wakiwa ni wavulana.

Idadi hiyo ya waliacha shule wilayani humo ni sawa na asilimia 17.3 ya wanafunzi 6,688 walioacha shule katika mkoa wa Geita uliopo Kanda ya Ziwa.

Mkazi wa kijiji cha Isebya, Rehema Gervas anasema sasa hana hofu na watoto wake kupata mimba na kuacha shule kwa sababu elimu itapatikana kwa urahisi kwenye eneo lao.

“Watoto wetu walikuwa wakizipata changamoto nyingi walipokuwa njiani wanaenda  Ilolangulu za ushawishi…binti anaomba lifti na katika kupewa usafiri hawezi kupewa bure wakati mwingine anaingizwa katika vishawishi na kutokea kwa mimba holela,” anasema Rehema.


Serikali iwafanya nini kuokoa jahazi? 

Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri ya Mbogwe, Pastory Mukaruka anasema wanatambua changamoto za shule hiyo, lakini wanaendelea kufanya hamasa kwa wananchi ili waendelee kuchangia kuhakikisha shule hiyo inajiendesha na wanafunzi wasome katika mazingira mazuri. 

“Kama kuna changamoto ya ruzuku hilo tutaliangalia hata kwa kupitia mapato ya ndani (ya Halmashauri) kuhakikisha shule hiyo inapata fedha ili utekelezaji wa shughuli za kila siku bila kukwama na kuwa na changamoto yoyote ile,” anasema Mukaruka.

Anasema Serikali itaendelea kuboresha miundombinu ya shule wilayani humo kadri fedha zinavyopatikana.

Follow us on TikTok

Nukta Habari

FOLLOW NOW
Subscribe to our channel

Nukta TV

SUBSCRIBE NOW
Rais Samia azindua minara 758, aacha maagizo mazito juu ya mkongo wa taifa

Rais Samia azindua minara 758, aacha maagizo mazito juu ya mkongo wa taifa

Nukta TV

JAJI MKUU: Njia za asili ni mojawapo ya njia halali za utatuzi wa migogoro

JAJI MKUU: Njia za asili ni mojawapo ya njia halali za utatuzi wa migogoro

Nukta TV

Hesabu ya bosi, bei ya mafuta pasua kichwa madereva wa daladala

Hesabu ya bosi, bei ya mafuta pasua kichwa madereva wa daladala

Nukta TV