Baada ya wafanyabiashara, Magufuli kukutana na wafugaji wa Tanzania
- Amesema anataka azungumze nao ili ajue na kuzitatua changamoto zinazowakabili.
- Amesema sekta ya mifugo ina mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi, ni lazima iangaliwe.
Dar es Salaam. Rais John Magufuli amesema ana mpango wa kukutana na wafugaji wote wa Tanzania ili wazungumze na kumueleza changamoto zao ikiwemo maeneo ya kuchungia mifugo yao, jambo litakalowezesha sekta hiyo kuchangia katika ukuaji wa uchumi wa Taifa.
Mpaka sasa Rais Magufuli ameshakutana na wawikilishi wa wafanyabiasha, wachimbaji wa madini na viongozi wa dini kwa nyakati tofauti Ikulu jijini Dar es Salaam.
Amesema sekta ya mifugo inatoa mchango mkubwa katika maendeleo ya Taifa na haiwezi ikaachwa bila kutatua changamoto zake.
“Nataka nipange kikao in a future (hapo baadaye) nizungumze na wafugaji wote kwa sababu hatuwezi tuka ignore (tukaziacha) changomoto zao wanazozipata na hasa katika kushughulikia maeneo wanayochungia kwa sababu ng’ombe tunao wengi,” amesema Rais Magufuli leo (Julai 22, 2019) Ikulu jijini Dar es Salaam wakati akiwaapisha mawaziri wawili George Simbachawene na Hussein Bashe.
Simbachawene ameteuliwa kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, akichukua nafasi ya mtangulizi wake, January Makamba ambaye uteuzi wake umetenguliwa huku Bashe akiteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Kilimo.
Zinazohusiana:
- Flyover ya Tazara ilivyoleta maumivu, faida kwa wafanyabiashara ndogondogo
- Serikali kuwalipa wafanyabiashara marejesho ya VAT
- Rais Magufuli atoa vitambulisho kwa wafanyabiashara wadogo.
Amesema Tanzania ina rasilimali ya kutosha ya mifugo ambayo inapasa kuendelezwa ili ilete matokeo kwa wananchi na katika ukuaji wa uchumi wa Taifa.
“Mpaka sasa tuna ng’ombe zaidi ya milioni 3.5 lakini nitakaa nao niwasikilize watoe ushauri wao niweze kuwasaidia wafugaji wa Tanzania ili kusudi suala la ufugaji liweze kuleta impact (matokeo) katika uchumi wetu,” amesema Rais.