Serikali kuwalipa wafanyabiashara marejesho ya VAT
- Marejesho hayo yanazihusu kampuni na wafanyabiashara mbalimbali nchini wakiwemo waagizaji wa sukari za viwandani ambao madai yao yamehakikiwa kuanzia Septemba, 2018.
- Kuchelewa kulipwa kwa madai hayo kunatokana na kuwepo kwa udanganyifu mkubwa kwa baadhi ya wafanyabiashara wasiokuwa waaminifu.
- Wafanyabashara nao walalamikia wingi wa kodi na mazingira yasiyoridhisha ya ufanyaji biashara.
Dar es Salaam. Serikali imeanza kulipa madai ya marejesho ya kodi ya ongezeko la thamani (VAT Refund) kwa kampuni na wafanyabiashara mbalimbali nchini wakiwemo waagizaji wa sukari za viwandani ambao madai yao yamehakikiwa kuanzia Septemba, 2018.
Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango, ametoa kauli hiyo wakati alipokutana na wafanyabiashara mkoani Tanga ambao wameiomba Serikali kuharakisha mchakato wa kuwalipa wafanyabiashara wanaodai kurejeshewa fedha zao zinazotokana na kufanya biashara nje ya nchi pamoja na wazabuni mbalimbali.
Dk Mpango amesema kuchelewa kulipwa kwa madai hayo kunatokana na kuwepo kwa udanganyifu mkubwa kwa baadhi ya wafanyabiashara wasiokuwa waaminifu hivyo kutaka kuingizia Serikali hasara kwa kulipa madai hewa.
“Kuna baadhi ya wafanyabiashara sio waaminifu, mfano tulipofanya uhakiki tuligundua madai hewa ya pembejeo ya zaidi ya Sh87 bilioni,” amesema Dk Mpango.
Akijibu hoja mbalimbali za wafanyabiashara hao, Dk Mpango, amehakikishia kuwa Serikali itazipitia na kuzitolea ufafanuzi kero zote zinazohusu kodi ili kurahisisha biashara na kuweka mahusiano mazuri kati ya wafanyabiashara na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ili kuongeza mapato kwa serikali.
Pia amesema Serikali inalifanyia kazi suala la mazingira ya kufanyia biashara na wingi wa kodi anazolipa mfanyabiashara kwa taasisi mbalimbali za serikali ili kodi hizo ziweze kutozwa sehemu moja na kupunguza adha wanazopata walipa kodi.
Lakini ili Serikali itekeleze wajibu wake, wafanyabiashara wametakiwa kushiriki katika mikutano ya sera za kodi inayondaliwa na Wizara ya Fedha na Mipango ambayo huanza mwezi Disemba hadi Januari kila Mwaka ili kutengeneza mizania ya ulipaji kodi nchini.
Zinazohusiana:
- NALA yaja na teknolojia ya kijanja kutuma, kupokea pesa
- Wabuni huduma za ofisi kuwawezesha wajasiriamali wanawake Dar.
Awali Mwenyekiti wa wafanyabiashara mkoa wa Tanga, Deogratias Ruhinda, amesema kuwa wafanyabiashara hasa wakulima wa zao la mkonge wanakutana na changamoto kubwa kutokana na serikali kutoa msamaha wa baadhi ya kodi kwa wafanyabiashara wanaoingiza kamba za manila hapa nchini, hivyo kulifanya zao hilo kutokuwa na soko la uhakika kutokana na bei ya kamba za nje kuwa chini.
Aidha wafanyabiashara hao waliiomba Serikali kuangalia uwezekano wa kuongeza kina cha Bandari ya Tanga ili meli kubwa ziweze kuja katika bandari hiyo na kurahisisha usafirishaji wa bidhaa mbalimbali kwenda nje ya nchi tofauti na ilivyo sasa ambapo bidhaa nyingi kutoka Tanga zinasafirishwa kwa kutumia Bandari ya Dar es Salaam au Mombasa jambo linalowaongezea gharama kubwa wafanyabiashara wa mkoa huo.
Wafanyabiashara hao wametakiwa kutosita kuishauri serikali njia bora ya kukusanya kodi na kutoa maoni yao jinsi ya tozo mbalimbali zinazotozwa na serikali kwa kuiandikia TRA au Wizara ya Fedha na Mipngo ili Serikali iweze kuboresha maeneo yenye mapungufu kwa faida ya Taifa.
Maafisa wa Wizara ya Fedha na Mipango pamoja na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), (waliokaa mbele) wakiwa katika mkutano wa Waziri wa Fedha na Mipango na wafanyabiashara wa Mkoa wa Tanga.