Flyover ya Tazara ilivyoleta fursa, maumivu kwa wafanyabiashara ndogondogo
Oscar Erasto kulia akiwa na Ramadhan Moshi wakiwa mawindoni kusubiri wateja mara baada ya ufunguzi wa Daraja la Juu la Mfugale. Picha| Zahara Tunda.
- Bodaboda, bajaji wanaona ni neema kwao katika kuwawahisha wateja wao.
- Wafanyabiashara wa kutembeza bidhaa barabara walia kupungua kwa wateja wajipanga kuhamia kwingine.
- Watumiaji wa barabara hiyo washukuru kwa kupunguziwa foleni katika eneo la Tazara kuelekea mjini.
Dar es Salaam. Wakati waendesha biashara ya usafiri jijini Dar es Salaam wakifurahia ujenzi wa daraja la juu Mfugale (Mfugale flyover) kutokana na kupunguza foleni, wafanyabiashara wa bidhaa ndogondogo ambao hutembeza katika makutano ya Barabara ya Mandela na Nyerere waeleza kuwa kwa sasa “biashara imekuwa ngumu sana.”
Baadhi ya waendesha bodaboda, bajaji na daladala wameiambia Nukta wakati wa uzinduzi wa flyover hiyo leo (Septemba 27, 2018) kuwa kwa sasa wanatumia muda mfupi kusafirisha abiria kwa kuwa foleni imepungua jambo linalosaidia kuongeza idadi ya safari na mapato.
“Sasa unapita kwa uhuru na muda muafaka, dakika tano tu unamuwahisha abiria mjini, hakuna tena kuzuiwa na trafiki katika mataa,” anasema Oscar Erasto, dereva wa bodaboda wa kituo cha Tazara.
Yasin Iddy (37), mkazi wa Gongo la Mboto Viwege huuza simu Kariakoo, amesema foleni ilikuwa inawakera na kuwachelewesha katika kufungua biashara zao jambo lililokuwa likichochea kushuka kwa mauzo na faida.
Hata wakati baadhi wakifurahia ufanisi katika biashara zao, wafanyabiashara waliokuwa wanatembeza bidhaa zao katika foleni kwenye makutano hayo ya Tazara wameeleza kuwa japo flyover hiyo ni jambo jema lakini imeathiri mwenendo wa biashara zao.
“Nimepokea kwa shangwe, ila nimeboreka kidogo, inabidi nitafute sehemu nyingine ya kufanya biashara kwa sababu kwa sasa hapa hakuna kitu,” amesema Grace Ngaraza (28), mfanyabiashara ya kutembeza mihogo na nazi katika eneo la Tazara.
Kilio hiki cha Grace kinatokana na mazoea ya kufanya biashara ya kutembeza mihogo katika foleni kabla ya kuwepo kwa flyover lakini sasa inamlazimu kuhama eneo na kutafuta lingine kwa sababu wateja wake kwa sasa wamepungua kwa kiwango kikubwa.
Grace hajaathirika pekee yake katika ufanyaji wa biashara zake.
Hussein Hamis, muuza ‘Ice cream’ eneo la Tazara aliyekuwa akipata wateja wake wengi kipindi cha foleni, amesema flyover itakuwa na faida kwa wenye magari lakini siyo kwa wao kwa kuwa walikuwa wakiuza bidhaa nyingi kwa watu waliokuwa katika foleni.
Awali kabla ya flyover hiyo, iliyopewa jina la Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) Patrick Mfugale, Hamis alikuwa anapata kuanzia Sh15,000 hadi Sh20,000 kipindi cha foleni lakini kwa sasa magari hayasimami hivyo inamuwia vigumu kupata wateja ukizingatia ndio daraja limefunguliwa rasmi.
“Sasa nahamia Ubungo ingawa ni mbali tutajitahidi twende kule kwa sababu bado kuna foleni,” Hamis ameiambia Nukta.
Zinazohusiana: Mfahamu mhandisi Patrick Mfugale ‘kichwa’ nyuma ya flyover ya Tazara
Rais Magufuli akosoa mapendekezo ya ripoti ya mazingira Stiegler’s Gorge
Daraja hilo la Mfugale limezinduliwa rasmi na Rais John Magufuli mbele ya maelfu ya wakazi wa Dar es Salaam ikiwa ni wiki chache tu tangu Serikali iruhusu vyombo vya moto kulitumia.
Licha ya maumivu ya wafanyabiashara wa kutembeza vitu katika foleni, wakazi wa jiji hilo wameeleza kuwa kuna ahueni kubwa ya foleni kuliko awali.
Wakazi wa maeneo ya Gongo la Mboto, Kiwalani, Machimbo na sehemu nyingine wamesema muda unaotumika katika kusafiri kwa sasa umepungua tangu kuanza kutumika kwa flyover hiyo ya kwanza kujengwa nchini.
“Imetusaidia kupunguza foleni na imebadilisha sura ya mji wetu,” amesema Erick Sylvanus (39) mkazi wa Kiwalani, Minazi Mirefu.
Wanafunzi wameelza kuwa ujenzi wa flyover hiyo na nyingine zitakazokuja utawasaidia kuwahi shuleni na kuwafanya wasome kwa makini zaidi.
“Zamani kulikuwa na foleni sasa hivi itakuwa rahisi kuwahi shule kwa sababu magari yanapita juu na chini,” amesema Abdul Mwalami, mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Kibasila.