Baada ya darasa la saba, Mara imeshindwa tena kutoboa kidato cha nne
- Ni miongoni mwa mikoa 10 iliyofanya vibaya katika matokeo ya kidato cha nne mwaka 2018.
- Katika matokeo ya darasa la saba mwaka jana ilikuwa ya mwisho kitaifa.
Kwa mara nyingine tena mkoa wa Mara haujafanikiwa kutoka kwenye kundi la mikoa 10 iliyofanya vibaya katika mtihani wa kidato cha nne mwaka 2018, jambo linaloacha maswali juu ya mstakabali wa elimu wa watoto wa mkoa huo.
Hilo limedhihirika juzi (Desemba 24, 2018) baada ya Baraza la Mitihani la Tanzania (Necta) kutangaza matokeo ya mtihani wa kidato cha nne ambapo katika mpangilio wa ufaulu kimkoa, Mara imeshika nafasi ya 22 kati ya mikoa 31 ya Tanzania.
Katika kundi hilo la mikoa iliyofanya vibaya imeungana na mikoa ya Katavi, Tanga, Mtwara, Mjini Magharibi, Lindi, Kusini Pemba, Kaskazini Pemba, Kusini Unguja na Kaskazini Unguja ambao imekuwa ya mwisho kitaifa.
Matokeo ya Mara ambayo ilikuwa na vituo 194 vya mitihani hayatofautiani na ya mwaka uliotangulia wa 2017 ambapo ilishika nafasi ya 23 kitaifa lakini mwaka jana ilipanda nafasi moja. Hata hivyo, haikutoka kwenye kundi la shule 10 za mwisho Tanzania.
Matokeo mabovu ya mkoa huo yanajidhihirisha zaidi katika madaraja waliyopata watahiniwa wake takribani 13,765 waliofanya mtihani huo ambapo siyo ya kuridhisha.
Uchambuzi uliofanywa na www.nukta.co.tz umebaini kuwa asilimia 25.4 ya watahiniwa wa mkoa huo wamepata daraja sifuri. Hiyo ni sawa na kusema robo ya watahiniwa hao wamefeli na hawawezi kuendelea na masomo ya kidato cha nne.
Licha ya matokeo hayo kuonyesha kuwa asilimia 74.52 ya watahiniwa wamefaulu kwa kupata daraja la I hadi IV, bado yanaacha maswali mengi kwasababu idadi kubwa ya wanafunzi wameangukia katika daraja la nne.
Pamoja na matokeo mabovu, hakuna Wilaya hata moja mkoa huo iliyoingia miongoni mwa halmashauri zilizofanya vibaya nchini.
Anguko la elimu mkoani humo linashuka hadi katika ngazi ya elimu ya msingi ambapo haifanyi vizuri. Katika mtihani wa darasa la saba mwaka jana, Mara ilishika mkia kitaifa na kuzua gumzo kwa wadau wa elimu.
Mpangilio wa mikoa kwa ubora wa ufaulu katika Mtihani wa Kumaliza Elimu ya Msingi (PSLE) 2018 unaonyesha kuwa Mara ilishika nafasi ya mwisho kati ya mikoa 26 ya Tanzania Bara ikiporomoka kwa kasi kutoka nafasi ya 13 iliyorekodiwa mwaka 2017.
Wakati Mara ikijikongoja mkiani, baadhi ya halmashauri zake vilifanya vibaya pia na kuchangia mkoa huo kufanya vibaya kitaifa licha ya juhudi mbalimbali zinazofanyika na Serikali kutoa elimu bila malipo.
Mara iliingiza wilaya mbili za Butiama na Musoma Vijijini katika halmashauri 10 zilizofanya vibaya katika matokeo ya mtihani huo.
Zinazohusiana:
Kushuka kwa ufaulu katika mkoa huo kunaibua maswali mengi ambayo yanahitaji majibu ili kuwanusuru wanafunzi ambao wanahitaji mazingira mazuri ya kusomea ili kufanya vizuri katika mitihani ya kitaifa.
Ukilinganisha na mikoa mingine ya Kanda ya Ziwa, mkoa huo umeachwa nyuma sana katika ufaulu huku mikoa ya Simiyu, Shinyanga, Mwanza na Kagera ikionekana kufanya vizuri hasa katika kuingiza shule kwenye 10 bora kitaifa.
Mikoa hiyo inaipa changamoto Mara ambayo kwa kiasi kikubwa mazingira yao yanafanana.
Latest
