Auwawa kwa kisu kisa ushabiki wa Simba, Yanga Songwe
- Jeshi la Polisi lasema linaendesha msako kumsaka mtuhumiwa.
- Laonya wananchi kutojichukulia sheria mkononi na kuepuka vitendo vya vurugu.
Dar es Salaam. Jeshi la Polisi mkoani Songwe linamtafuta Evacery Mwaweza mkazi wa Kitongoji cha Ululu kiijiji cha Idiwili kata ya Idiwili wilayani Mbozi mkoani Songwe kwa tuhuma za kusababisha kifo cha Zabroni Mwambogolo (28) mkazi wa kitongoji hicho wakati wakiangalia mpira wa Simba na Yanga.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, Augustino Senga aliyekuwa akizungumzia tukio hilo leo Jumatano Septemba 17,2025 amesema limetokea Septemba 16, 2025 saa 12:50 jioni baada ya mabishano ya mpira wa Yanga na Simba.
“Uchunguzi wa tukio hilo umebainika kuwa ni ushabiki wa mpira wa Simba na Yanga kati ya marehemu na mtuhumiwa. Ambapo mtuhumiwa alitumia kisu alichokuwa nacho wakati wa ugomvi huo kumchoma marehemu kifuani na baada ya kutenda kosa hilo alitoroka kusikojulikana,” amesema Kamanda Senga.
Sambamba na msako mkali wa kumtafuta mtuhumiwa Jeshi la Polisi limetoa wito kwa wananchi kuepuka kujichukulia sheria mkononi na kutojihusisha na vitendo vya vurugu vinavyoweza kusababisha madhara.
Katika tukio lingine Kamanda Senga amesema watu watatu wamefariki dunia katika ajali iliyohusisha bajaji na gari katika barabara kuu ya Tunduma – Sumbawanga katika kata ya Chipaka Tarafa ya Tunduma wilayani Momba mkoani Songwe.
Kamanda Senga amesema gari aina ya Canter ikiwa inaendeshwa na dereva ambaye hajafahamika jina lake aligonga bajaji iliyokuwa ikiendeshwa na dereva aliyefahamika kwa jina Silasi Malongo (23) mkazi wa mwaka Tunduma.
Kwa mujibu wa Senga ajali hiyo ilitokea Septemba 15,2025 saa 3:00 asubuhi ambapo watu watatu waliofariki ni Ibrahimu Kibadeni(16) mwanafunzi, Silasi Malongo(23) dereva bajaji na mwanamke mmoja anayekadiriwa kuwa na miaka 30-40 ambaye jina lake halijafahamika ambaye alifariki akiwa anapatiwa matibabu kituo cha afya Tunduma.
Katika ajali hiyo watu wawili wamejeruhiwa akiwamo Venace Jail (34) na Loyce Kandonga (15) wote wakazi wa Tunduma.
“Uchunguzi wa awali unaonyesha ni uzembe wa dereva wa gari ambaye aligonga bajaji kwa uzembe wa kutozingatia sheria za usalama barabarani,” amesema Kamanda Senga.
Latest