Pangani ndani ya vita ya kuwaokoa watoto na ulawiti, ubakaji

May 14, 2022 9:54 am · Nuzulack Dausen
Share
Tweet
Copy Link
  • Baadhi ya wazazi wajitoa kuwalinda watoto kwenye maeneo hatarishi yakiwemo ya vigodoro.
  • Wadau wataka wazazi, walezi wafuatilie mienendo ya watoto wao, kuacha kuwadekeza.
  • Serikali yasema itaendelea kuwadhibiti wanaohusika na vitendo hivyo.

Pangani, Tanga. Jioni moja baada ya majukumu yake ya kazi Katibu wa Wilaya ya Pangani, Hassan Nyange alijikuta akishughulikia kisa cha mtoto mmoja aliyekuwa ametoka katika moja ya mapagale yaliyopo mjini hapo.

Mtoto huyo wa darasa la kwanza hakuwa na hali ya kawaida kiasi cha kufanya waliokuwepo hapo kupata mashaka juu ya kilichomtokea.

Baada ya kubanwa mtoto huyo, Nyange anasema alieleza kuwa ameingiliwa (amelawitiwa) na mtu mmoja katika jengo hilo ambalo halijakamilika.

Ni majanga

“Baada ya kupimwa, DMO (Mganga Mkuu wa Wilaya) alishika kichwa…alisema huyu mtoto ameingiliwa…mtoto alipoulizwa alisema ‘amenizowesha kutoka mwaka jana’,” anasema Nyange.

Chanzo cha masahibu kama hayo kwa watoto wa Pangani kwa mujibu wa Nyange ni tabia ya wazazi kuwatuma watoto usiku sehemu yenye umbali mrefu bila kujali usalama wao na kupungua kwa maadili katika jamii hiyo.

Visa vya watoto kulawitiwa na kujihusisha na vitendo viovu vinavyoathiri ukuaji wao ni moja ya masuala yanayoitesa jamii ya wakazi wa Pangani mkoani Tanga.

Wazazi na mamlaka hapa wanahaha kutafuta suluhu zitakazowalinda watoto wao dhidi ya vitendo hivyo hatari katika ukuaji wao na ustawi wa Taifa.

Baadhi ya wakazi wa Pangani wakiwa katika hafla ya uzinduzi wa shughuli za uraghbishi wilayani humo Februari 15, 2022 ambapo wananchi walihimizwa kuibua na kutatua matatizo yanayowakabili katika jamii yakiwemo ubakaji, ulawiti na malezi mabovu. Picha| Twaweza. 

Watoto wajitosa kwenye kamali, vigodoro, ngono kwenye umri mdogo

Miongoni mwa vitendo hivyo ni uchezaji wa kamali maarufu kubet, kujiingiza kwenye ngono katika umri mdogo, kushiriki katika matamasha ya watu kama vigodoro na kwenda kwenye vilabu vya pombe usiku.

“Tunakaa kwenye jamii ambayo mwanafunzi mmoja wa kike wa shule ya msingi anataja wanaume karibu kijiji kizima kwamba ametembea nao, ana kumbukumbu ya wanaume 30 na maumbile yao…halafu ‘tunarelax’ (tumejiachia) maisha yanaendelea,” anasema Nyange.

“Lazima kuwe na tatizo katika jamii yao.”

Mkoa wa kipolisi wa Tanga uliongoza kwa kuwa na visa vingi vya ubakaji mwaka 2020 kwa mujibu wa Ripoti ya Takwimu za hali ya uhalifu na matukio ya usalama barabarani Januari – Desemba 2020 baada ya kuripoti visa 431 ukifuatiwa na Kilimanjaro uliokuwa na kesi 418.

Takwimu hizo za Jeshi la Polisi na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) zinabainisha kuwa Tanga ilikuwa ni miongoni mwa mikoa 15 yenye kesi nyingi za ulawiti mwaka 2020 ukiongozwa na mkoa wa kipolisi wa Kinondoni uliokuwa na kesi 150, Dodoma (127) na Kilimanjaro kesi 94.

Wazazi waanza kudhibiti mdogo mdogo

Baadhi ya wazazi wameanza hatua za kudhibiti jambo hilo kwa kuwaelimisha wazazi na kufanya doria katika majumba ya starehe na kuwafurusha watoto wote wanaokuwepo nyakati za usiku.

Bibie Mohammed, mkazi wa Kijiji cha Msaraza wilayani hapa anasema wazazi wa eneo hilo walijisahau kwa kuwapa fursa kubwa watoto kuwa viongozi wa familia kwa kuwategemea kwenye kipato au kuwatumia kwenye kazi zisizoenda na umri wao.

“Baada ya kuligundua hilo tulipita kila kitongoji na kutoa elimu kwa wazazi kuwa si ruhusa kumtumikisha mtoto mwenye umri wa chini ya miaka 18 na haruhusiwi kwenye vigodiro au usiku wa zawadi katika harusi,” anasema Bibie ambaye ni mmoja ya wajumbe 10 wa kamati ya wananchi inayolenga kuchochea kuibua na kutatua matatizo yanayowakabili kijijini kwao.

Mbali na kutoa elimu wakazi hao, Bibie anasema waliushawishi uongozi wa kijiji kuchukua hatua ambapo walikubali kuweka kwenye utaratibu wa kufanya doria na kupiga faini wanaokiuka.


Tangazo:


Wapanga zamu ya kuwasaka watoto kwenye vigodoro

Kutekeleza jitihada hizo, wanakamati hao 10 walikuwa wanagawana kufanya doria kwenye vigodoro, baa, na maeneo mengine ya starehe ambapo waliwabaini watoto waliokuwa wakienda mara kwa mara na kuwaita wazazi wao kwa hatua zaidi.

“Hatukutaka kuwapa adhabu wazazi wao ila tuliwapa elimu juu ya madhara ya kuwacha watoto wao kwenye mazingira yale na kwamba iwapo watarudia tutawapiga faini ya Sh50,000 kila mmoja,” anasema Bibie.

“Sasa watoto wale ufaulu umekuwa mzuri na wana maendeleo mazuri shuleni tofauti na awali,” anaongeza.

Mraghbishi kutoka Kijiji cha Mwera nje kidogo ya mji wa Pangani, Hamis Mavumila anasema wao moja ya mafanikio makubwa wanayojivunia katika kuimarisha malezi na makuzi ya watoto ni kudhibiti utoro katika shule za msingi na sekondari.

Matunda yaanza kuonekana

Katika kijiji hicho anasema wazazi walihamasishana kupitia waraghbishi kiasi cha kusaidia watoto wengi kuhudhuria shule siku zote jambo lililosaidia kuongeza ufaulu kwenye masomo.

“Safari hii wanafunzi 16 tu katika Shule ya Sekondari Mwera ndiyo wamefeli,” anasema Mavumila.

Tabia ovu walizonazo baadhi ya watoto wa Pangani na maeneo mengine nchini ni matokeo ya udhaifu wa wazazi na walezi katika malezi, watalaamu wanaeleza.

Rukia Masanyika, mkufunzi wa uraghbishi anasema wazazi wanapaswa kuwa mstari wa mbele kuhakikisha wanafuatilia kikamilifu mwenendo wa ukuaji wa mtoto badala ya kuwaacha wajiongoze.

Miaka ya nyuma, anasema, wazazi na jamii kwa ujumla ilikuwa ikijishughulisha zaidi na malezi ya watoto kwa sasa hali ni tofauti.

“Wazazi wamekuwa busy sana kutafuta maisha na wanawasahau watoto wao. Ni vema sasa wakarudi na kuwa karibu nao,” anasema Rukia.

Mbali na ufuatiliaji wa watoto, baadhi ya wadau wa kuwalinda watoto wanaeleza kuwa wazazi wanatakiwa waachane na tabia ya kuwadekeza watoto kiasi cha kuwafanya wajiamulie kila kitu jambo ambalo ni hatari kwa ukuaji wao.

‘Acheni kudekeza watoto’

Mkurugenzi wa Shirika la Pangani’s Coastal Paralegal (Pacopa) Bakari Kishada anasema wazazi hawatakiwi kuwapa watoto wao uhuru uliopitiliza unaofanya kila anachotaka anapewa kutokana na kudekezwa.

“Mtoto anaweza kukuambia baba leo siendi shule nataka unipe Sh5000, anaweza asiende kweli mpaka umpe hiyo fedha…tunawadekeza watoto kupita kiasi…unaweza kumpa mtoto kitu ambacho hata hukutegemea, hii haifai,” anasema Kishada.

Wazazi kama Bibie wanaeleza kuwa wakati umefika kwa kila mzazi kuwa mlinzi wa mtoto wake na wa mwenzie kwa kuwa uzungu wa sasa umefanya iwe ngumu kudhibiti baadhi ya tabia za watoto mtaani.

“Kama wazazi tubadilike ili tuzisimamie kikamilifu ndoto za watoto wetu ili baadaye zitusaidie na sisi ziku za mbeleni. Muda wao utafika ila siyo sasa, tuwalinde na kuwaonya ili waweze kufikia ndoto za kielimu,” anasema Bibie.

Serikali yaahidi kuwadhibiti waovu

Katika wilaya Pangani, uongozi wa Halmashauri unasema wanaendelea kutoa elimu na kuwachukulia hatua kali wanaohusika na vitendo viovu kama vya ulawiti na ubakaji licha ya kuwepo tabia ya wanafamilia kulindana kwa kuwaficha waovu au kuharibu ushahidi.

Nyange aliwaambia wakazi waliokuwa wameshiriki mkutano wa uzinduzi wa masuala ya uraghbishi wilayani Pangani kuwa si vema kumtuma mtoto usiku ili kuwanusuru na madhira hayo.

“Watoto wa kike wasizururezurure,” anasema kiongozi huyo wa wilaya.

“Tunaendelea kutafakari tunatengenezaje sheria ndogo. Nawaomba madiwani kipindi kijacho tutafakari hili…mfikirie hapa katikati tunatengenezaje sheria ngumu kudhibiti hali hii,” anaongeza Nyange.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW