Afya bora: Silaha namba moja ya kupata pesa za uhakika
- Ijali afya yako kabla ya kuweka maslahi ya pesa mbele.
- Fanya uchunguzi wa afya mara kwa mara.
- Kata bima ya afya, kula vizuri na pata muda wa kupumzika.
Sikatai, pesa ni sabuni ya roho. Lakini kwa jinsi tunavyozitafuta, huenda tukaishia kuona sabuni hiyo ikiosha roho za wengine baada ya roho zetu kuharibika katika utafutaji.
Katika karne hii, pesa ni kila kitu, kujali afya katika majukumu yetu ya kila siku ni changamoto.
Iwe mapenzi, heshima na hata kupata mishe mjini, unahitaji pesa. Huenda ndiyo sababu ya wengi kuwa tayari kufanya lolote ili waipate shilingi.
Hata hivyo, katika utafutaji huo, inashauriwa kuendelea kuiweka afya yako mbele kwani endapo afya yako haitokuwa sawa, hautoweza kuisaka chapa hiyo.
Ufanye nini ili kubaki na afya njema wakati ukiendelea kutafuta?
Weka ratiba ya “Check Up” kila mwaka
Hapa kila mtu ana mapendekezo yake. Uchunguzi huo unategemea hali yako ya afya pamoja na umri.
Tovuti ya masuala ya afya, Healthline inashauri kujua hali ya afya ya mwili wako wote walau mara moja kwa mwaka kwa watu wenye umri chini ya miaka 50.
Kwa watu wenye magonjwa sugu ikiwemo kisukari, inashauriwa kufuata maelekekezo ya dakatari wako juu ya muda wako wa kufanyiwa uchunguzi.
Kata bima ya afya
Mara nyingi nimewasikia rafiki zangu wakisema “bima ya nini?” kwa kuwa hawaumwi mara kwa mara. Kwa baadhi yao, ni kupoteza fedha.
Tovuti ya masuala ya afya ya nchini Marekani, HealthCare.gov imeandika kuwa, bima ya afya itakuepushia gharama kubwa za matibabu usizozitegemea.
Zaidi, bima ya afya itakupatia sababu ya kupata check up yako ya mara kwa mara.
Bima ni muhimu kwani hakuna mtu anayejua lini atapatwa na changamoto za kiafya na hali ya uchumi atakayokuwa nayo kipindi hicho.
Soma zaidi:
- Namna waathirika wa ajali ya Mv Nyerere wanavyoweza kusaidiwa kisaikolojia.
- Jinsi unavyoweza kuishinda sonona isiharibu maisha binafsi, kazi.
Kumbuka kupumzika
Kuwa na pesa muda wote ni furaha kwa wengi hivyo kutafuta pesa hizo pia ni shughuli ya kila siku. Baadhi wanasahau kuwa miili yao ni ya nyama.
Kazi zipo, hazitokuja kuisha. Hakikisha unapata muda wa kutosha kulala ili kuupumzisha mwili wako.
Healthline imeandika, usipopata usingizi na mapumziko ya kutosha, unaweza kuumwa, kuongeza hatari ya wewe kupata saratani na uwezo wako wa kufukiria pia unaweza kushuka hivyo kuathiri ubunifu wako.
Zingatia zana za tahadhari
Katika kukamilisha majukumu yako huenda unatumia baadhi ya teknolojia ikiwemo vitu vizito, kompyuta, vitu vyenye ncha kali na hata kufanya kazi kwenye mazingira ya vumbi.
Unatakiwa kuzifahamu zana zako za tahadhari ikiwemo “gloves”, miwani ya kupunguza makali ya mionzi na hata barakoa kwa mazingira ya vumbi.
Siku zote fahamu kuwa usipoweka kipaumbele kwenye afya yako mwenyewe, hakuna mtu atakayekukumbusha. Labda imi niliyeandika makala haya.