Namna waathirika wa ajali ya Mv Nyerere wanavyoweza kusaidiwa kisaikolojia

September 24, 2018 12:42 pm · Zahara
Share
Tweet
Copy Link
  • Mtu aliyepatwa na janga  kama hilo hupata hofu, kutengwa, kukosa usalama, upweke, sonona, kusalitiwa, kujilaumu, kushindwa kupata umakini na utulivu wa kufikiri.
  • Wataalam wa kisaikolojia washauri jamii kushirikiana na kuwasaidia wahanga kwa hali na mali.
  • Uongozi wa Mkoa wa Mwanza kufungua akaunti maalum kwa ajili ya kukusanya fedha zitakazosaidia walioathirika na ajali

Dar es Salaam. Kutokana na kuzama kwa kivuko cha Mv Nyerere katika Ziwa Victoria Septemba 20 mwaka huu na kugharimu maisha ya watu zaidi ya 200, wataalam wa saikolojia wapendekeza wahanga na ndugu kupatiwa tiba ya kisaikolojia kuwarejesha katika hali ya kawaida.  

Majanga makubwa kama hayo ya ajali, kimbunga, tetemeko la ardhi au mafuriko yanapotokea huja na athari kubwa kwa wahanga wa ajali hizo kuanzia ngazi ya kifamilia, kijamii na taifa.

Kwa mujibu wa taasisi ya Brooken haven retreat inayojihusisha na masuala ya kisaikolojia inaeleza kuwa kwa kawaida mtu ambaye hupatwa na majanga  kama hayo huwa anahisi uoga, hofu, kutengwa, kujirudia rudia kwa tukio lililompata akilini, kukosa usalama, upweke, sonona, kusalitiwa, kujilaumu, kushindwa kupata umakini na utulivu wa kufikiri.

Hali hii huwa ni ya muda mfupi baada ya mtu kupatwa na tukio la kushtua na la kusikitisha na kama litaendelea kutokea kwa muda mrefu zaidi basi mtu huyo atahitaji kupatiwa msaada wa kitaaalam ili kuweza kukabiliana na hali hiyo.

Kazi kubwa ya kuwaepusha wahanga hawa ni kuwafariji na pamoja na kuwa nao karibu na kuwatafutia maeneo ya utulivu ili waweze kurudi katika hali ya kawaida.


Zinazohusiana: 


Kwa upande wa watafiti wa saikolojia kutoka Chuo Kikuu cha New York wanasema msaada ambao anatakiwa apatiwe mtu unaweza kuwa wa hali na mali ili waweze kurudi katika hali ya kawaida au kuwapa moyo na ushauri wa kisaikolojia.

Mtaalam wa saikolojia kutoka kampuni ya DM Saikolojia Limited, Dosi Said Dosi amesema kuna njia mbalimbali za kuwasaidia ndugu, familia na wahanga walionusurika katika ajali ya kivuko cha MV Nyerere.

Wahanga wa ajali

Dosi anasema kwa wahanga wa ajali wanatakiwa waamini katika vipawa vyao kukabiliana na hali.

“Ni kawaida kwa wahanga kuhisi kuvurugwa na kukosa nguvu ila wanatakiwa wakumbuke ya kuwa wana nguvu na uwezo wa kukabiliana na hali hii , kama wameweza kuokoka na ajali hii basi pia wanaweza pia kuishinda hali hii,” amesema Dosi.

Wahanga hukosa hamu ya kujichanganya na jamii ila ili waweze kukikabili kipindi hiki, hivyo wanapaswa kuwa karibu na familia zao na jamii kwa ujumla na ikiwezekana wajitoe katika kazi za kujitolea kama kufanya usafi.

“Watumie muda wao kupumzika na kutulia ambapo wanaweza kufanya meditation, kulala vizuri, kusikiliza muziki uupendao na kuangalia filamu za vichekesho,” amesema Dosi.

Hata hivyo, wahanga wanatakiwa kula chakula kizuri, kwasababu katika kipindi hiki kigumu wengi wanakosa hamu ya kula ila wanatakiwa wajikaze na kujilazimisha kula vizuri ili mwili na akili viweze kufanya kazi kwa ufanisi.

“Mazoezi hasa ya viungo, kukimbia yanasaidia sana kupunguza msongo wa mawazo na kuufanya mwili kuwa na ari nzuri,” amesema.

Wataalam wengine wa saikolojia wanasema kwamba ni vyema kujisahaulisha kwa makusudi, hali ya tukio maana inaweza kuwa inajirudia rudia hivyo inapokutokea jaribu kujisahaulisha na kufanya jambo lingine.

Vilevile ni muhimu kuepuka vilevi, baadhi wanaweza fikiria kutumia vilevi ili kukabiliana na hali hii lakini vilevi vipo kwa ajili ya kulevya akili tu na hivyo vinaweza vikakuletea matatizo zaidi ya kutatua.

Kivuko cha MV Nyerere kikiwa katika shughuli zake za kawaida kabla ya kukutwa na janga la kupata ajali Septemba 20, 2018. Picha|citizentv.co.ke

Msaada wa kisaikolojia kwa ndugu na jamii

Kwa ndugu na jamii walioshuhudia ajali wanatakiwa kuwapa ushirikiano wahanga na familia kwa kuwaonesha mapenzi waathirika waliookolewa kwa kuwa nao karibu na kuwasaidia kadri wawezavyo.

Dosi anabainisha kuwa, “Kutotuma ama kusamabaza picha za marehemu, picha zinaweza kuongeza maumivu kwa jamii na kwa ndugu wa marehemu na hivyo kuchelewesha uwezo wa kukabiliana na hali.”

Katika kipindi kama hiki inashauriwa wananchi na Serikali kuwa wamoja na kushirikiana kuendelea kuokoa na kuwahudumia waathirika na kuacha kulaumiana.

“Jamii inapoanza kulaumu tu inawaweka waathirika njia panda na kuongeza hali ya kuhisi wametengwa,” ameeleza mtaalam huyo wa saikolojia.

Serikali ilivyojipanga kuwasaidia wahanga na ndugu

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Jenista Mhagama amesema uongozi wa Mkoa wa Mwanza utafungua akaunti maalum kwa ajili ya kukusanya fedha zitakazosaidia walioathirika na ajali ya kuzama kwa Kivuko cha MV Nyerere.

“Fedha zitakazopatikana zitawasaidia ndugu na manusura wa ajali,” amesema Mhagama.

Hata hvyo serikali itatoa gharama zote za mazishi kwa watu waliopoteza maisha katika ajali hiyo ikiwa ni moja ya sehemu ya kuwafariji wafiwa na kuwapunguzia gharama.

   

Enable Notifications OK No thanks