Afrika kutumia zaidi hati fungani kupata mikopo ya maendeleo

May 30, 2023 5:26 am · admin
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni kutokana na kuongezeka kwa  gharama ya mikopo ya nje ambayo utoaji wake ni mgumu na wenye shinikizo
  • Inatarajiwa itachochea kasi ya maendeleo kwa kufanikisha bajeti ya Serikali zao.

Dar es Salaam. Nchi za Kusini mwa Afrika ikiwemo Tanzania zinatazamia kuchukua muelekeo mpya katika sekta ya mikopo kwa kuendeleza soko la ndani la mitaji kwa kutumia hati fungani ili kupata fedha za kutekeleza miradi ya maendeleo.

Hatua hiyo itasaidia kupunguza gharama na riba za mikopo ya kibiashara inayotolewa na taasisi za fedha za kimataifa.

Kamishna wa Idara ya Usimamizi wa Madeni wa Wizara ya Fedha na Mipango,  Japhet Justine amesema mikopo ya ndani inatoa nafuu kubwa kwa nchi za Afrika kwa kuwa haihusishi Dola ya Marekani na haina shinikizo.

“Duniani mikopo ya kibiashara inapatikana kwa gharama kubwa, hivyo mikopo ya ndani itakuwa sehemu ya hatua muhimu ya kuzisaidia nchi za Afrika kufanikisha ufadhili wa bajeti kwa ajili ya maendeleo yao” amesema Justine.

Justine alikuwa akizungumza katika mkutano wa wataalamu wa uchumi na  fedha  wanaosimamia madeni ya nchi zao kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Dk Natu El- Maamry jijini Arusha Mei 30, 2023. 

Justine ameongeza kuwa kuliendeleza soko la ndani la hati fungani kunatoa fursa kwa nchi za Afrika kufanya vizuri zaidi, ambapo  Tanzania kwa sasa inapata mikopo ya zaidi ya Sh7 trilioni kutoka soko la ndani ambayo husaidia kufanikisha bajeti Kuu ya Serikali.

Mkutano huo wa wataalamu wa uchumi na fedha wanaosimamia madeni ya nchi zao umewakutanisha wawakilishi kutoka nchi 16 za kusini mwa Afrika.

Mkutano huo umejadili na kuchambua aina ya hati fungani za ndani zinazotolewa na manufaa yake katika kukuza uchumi wakati ambao mikopo kutoka kwa wakopeshaji wa kimataifa inapungua.


Soma zaidi


Kutokana na janga la Uviko-19 na vita inayoendelea kati ya Ukraine na Urusi, mashirika mengi ya kimataifa ya fedha kama Benki ya Dunia (WB) na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) yamepunguza kasi ya utoaji mikopo kutokana na kiasi kikubwa cha fedha kutumika katika kufadhili na kutoa misaada nchini Ukraine.

Kwa mujibu wa Justine, Namibia ni miongoni mwa nchi ambazo zinafanya vizuri katika bajeti zao kwa kutumia fursa ya soko hilo ambapo zaidi ya asilimia 80 ya bajeti yake inatokana na mikopo ya ndani kupitia hati fungani zake.

Mkutano huo umezishirikisha nchi za kusini mwa Afrika ikiwemo Tanzania ambaye ni mwenyeji wageni Namibia, Zambia, Zimbabwe, Malawi, Afrika Kusini, Uganda, Kenya, Sudani Kusini na Ethiopia.

Hati fungani ni nini

Kwa mujibu wa benki ya NMB, hati fungani ni aina ya uwekezaji ambapo mwekezaji anawekeza katika chombo (haswa shirika la kibiashara au serikali) kitakachokopesha fedha/mfuko huo katika muda maalum na kwa riba inayoweza kubadilika au riba isiyobadilika. 

Hivyo unaponunua hati fungani unakuwa umewekeza au umekopesha fedha zako kwa kwa taasisi hiyo ambapo utapata faida kulingana na muda uliowekeza ambayo inatokana na riba ya mkopo husika.

Tofauti na hisa, hati fungani hazikupi umiliki na huwezi kupiga kura za maamuzi katika benki.

Follow us on TikTok

Nukta Habari

FOLLOW NOW
Subscribe to our channel

Nukta TV

SUBSCRIBE NOW
PART 2: Yafahamu magari 10 yanayotumia kiwango kidogo cha mafuta.

PART 2: Yafahamu magari 10 yanayotumia kiwango kidogo cha mafuta.

Nukta TV

🔴LIVE: LIVE:WABUNGE WAKIWACHAPA MASWALI MAWAZIRI | Bunge la 13 | Kikao cha 28

🔴LIVE: LIVE:WABUNGE WAKIWACHAPA MASWALI MAWAZIRI | Bunge la 13 | Kikao cha 28

Nukta TV

PART 1: Yafahamu magari 10 yanayotumia kiwango kidogo cha mafuta

PART 1: Yafahamu magari 10 yanayotumia kiwango kidogo cha mafuta

Nukta TV