Acha masihara, corona ipo: Chukua tahadhari

April 26, 2020 12:35 pm · Dk Felician
Share
Tweet
Copy Link
  • Kupitia maombi yetu ya kila siku kwa Mwenyezi Mungu aliye mponyaji wa kweli, naamini tutaweza kuishinda corona mpaka jamii duniani ishangae kulikoni Tanzania.
  • Niwaombe Watanzania wenzangu kwamba wakati wa kuchukua hatua kujinusuru na COVID-19 ni sasa

Sisi tunaoendelea kuishi hatuna budi kumshukuru Mwenyezi Mungu maana ni yeye pekee mwenye uwezo wa kutujalia uzima wakati huu wa janga la virusi Corona (COVID-19).

Licha ya ukweli kuwa COVID-19 ilianzia nchini China na hatimaye kusambaa dunia nzima kwa kasi kubwa, taarifa zinazotolewa mara kwa mara na viongozi wetu: Rais, Waziri Mkuu; Waziri wa Afya wengi tumeelewa hali ilivyo kuhusiana na janga la corona duniani na nchini mwetu.

Hata hivyo, kupitia maombi yetu ya kila siku kwa Mwenyezi Mungu aliye mponyaji wa kweli, naamini tutaweza kuishinda corona mpaka jamii duniani ishangae kulikoni Tanzania.

Nichukue fursa hii kuipongeza Serikali kwa kuchukua hatua za makusudi kuzuia corona isisambae sana zikiwemo kuhakikisha kila mgeni au raia anayetoka nje ya nchi anakaa karantini kwa muda wa siku 14 asichanganyike na jamii na kutoa elimu kwa umma kuhusu janga la corona kwa kututaka tunawe mikono wa maji yanayotiririka na sabuni kwa muda wa takribani sekunde 20.

Lakini pamoja na kututaka tutumie vitakasa mikoni (sanitizer) kuweka mikono yetu katika hali ya usafi na salama; baadhi ya wafanyabiashara wakaona hiyo ni fursa nzuri kuweza kupata fedha zaidi kwa kipindi kifupi na kupandisha bei bidhaa hizo.

Serikali ilipoona hali imekuwa hivyo, ikaamuliwa sanitizer ziuzwe kupitia Bohari ya Dawa nchini (MSD) hususani katika Jiji la Dar-Es-Salaam. Tunashukuru sana kwa uamuzi huo na tuombe kuwa sanitizers zipatikane muda wote na bila kikwazo chochote.  

Vilevile, Serikali iliamua kisitisha shughuli zenye kusababisha misongamano kama michezo ya aina yote; kufunga shule na vyuo; kututaka wananchi wasitembee bila sababu za msingi; kuacha utamaduni wa kukumbatiana na kushikana mikono wakati wa kusalimiana; kuacha shughuli za Ibada ziendelee kufanyika kwa misingi ya kumwabudu na kumwomba Mwenyezi Mungu atusaidie na kutunusuru na janga la corona.


Soma zaidi: 


Lakini tunatakiwa kuyafanya hayo yote, ikiwemo shughuli za kutafuta riziki zetu za kila siku kwa tahadhali kubwa sana. Vilevile, waumini wa dini na madhehebu mbalimbali walitahadharishwa kuachana na tabia ya kufanya Ibada kimazoea na pia kutakiwa kunawa mikono kabla na baada ya kutoka kwenye sehemu za Ibada.

Vilevile, navishukuru vyombo vyote vya habari kwa jitihada za kuhamasisha na kuelimisha umma namna ya kujikinga na kuepuka kuambukizwa COVID-19, hakika mnafanya kazi nzuri na Mungu awasaidie na kuwajalia afya njema muda wote wa mapambano.

Kutokana na juhudi za Serikali na za vyombo vya habari hakuna atakayejitetea kuwa amekosa taarifa sahihi. Kazi kubwa inafanyika sana kwenye maeneo ya Majiji, Manispaa, Miji na viunga vyake.

Hata hivyo, Vijijini wanapata taarifa lakini siyo kwa kiwango kama mijini. Ni vizuri tukaongeza nguvu huko vijijini kwa kusudio la kuinua uelewa wao wajue corona ni nini na wafanye nini kujikinga wasiambukizwe na ugonjwa huo.

Pamoja na jitihada zinazofanyika bado kuna sintofahamu miongoni mwetu. Nimeona hali ilivyokuwa kwenye Soko Kuu la Dodoma; baadhi walionyesha kutojali kunawa mikono yao. Sehemu za kunawa mikono pia zilionekana kuwa chache ingawa waliohojiwa wengi walikiri kufahamu corona ni nini lakini mwamko wa kujikinga ulikuwa bado wa chini.

Hali ilionekana hivyo kwenye Soko Kuu la Samaki eneo la Feri Jijini Dar-Es-Salaam; Soko la Ndizi eneo la Mabibo, Manisapaa ya Ubungo pia kwenye Stendi ya Daladala iliyoko Makumbusho japo wengi walionekana kuchukua hatua ikiwemo Daladala kutobeba abiria waliosimama.

Ila kizungumkuti kilionekana kwenye kupanda daladala ambako walisukumana kupanda basi wengine kupitia kwenye madirisha. Kwa nini hatupangi mistari na kuweza kuingia kwenye magari kwa usitaarabu?

Kwenye mabasi ya mwendo kasi huko hali siyo shwari hata kidogo maana kila wakati msongamano ni mkubwa na mabasi ni machache. Ipo haja kuchukua hatua za haraka kuongeza mabasi ikiwa ni pamoja na kuruhusu daladala zipeleke abiria Posta na Kariakoo kutoka Kimara na Mbezi.

Kwa hali ilivyo tusizembee hali siyo shwari maana corona inaenea kwa kasi kubwa duniani. Ikitokea hali ikawa mbaya tukafungiwa ndani bila kutoka nje ndipo tutakapoonja machungu maana wengi wetu kula yetu inatokana na kutoka nje kubangaiza hapa na pale.

Wenzetu nchi zilizoendelea wanaouwezo kiuchumi kuzuia watu wasitoke na wakawapa riziki ya kila siku angalau kwa muda fulani lakini sisi uwezo huo ni mdogo na tayari tumeishaathirika na mafuriko pamoja na miundombinu mingi kuharibika. Fedha nyingi zinaelekezwa huko tukiongeza na janga la corona hali itakuwa mbaya zaidi.

Kadhalika, tuachane na mtazamo wa “Serikali ifanye” bila kuchukua hatua stahiki. Serikali ndiyo inafanya lakini sisi tufanye zaidi tutimize wajibu wetu, tuchukue tahadhali ipasavyo; tuache kubeza na wakati mwingine kusita kuchukua hatua eti “hali ya maisha ngumu”. Kuendelea kufanya hivyo na kuwa na mtazamo hasi kweli hali ya maisha itazidi kuwa ngumu.

Niwaombe Watanzania wenzangu kwamba wakati wa kuchukua hatua kujinusuru na COVID-19 ni sasa.

Usisubiri mtu mwingine aje kukunusuru anza wewe kuchukua tahadhari ukianzia nyumbani kwako na hatimaye popote utakapokuwa chukua tahadhari nawa mikono mara kwa mara; epuka misongamano; jihadhari kushika macho, pua na midomo au usoni kwa ujumla; funika midomo na pua wakati wa kupiga chafya au kukohoa na sikiliza mara kwa mara ushauri unaotolewa na Wataalamu wa afya na Viongozi wetu.

Vilevile, matumizi ya mitandao ya kijamii yawe kwa nia ya kuelimishana na kutoa ushauri nasaha na wala siyo kubeza au kufanya utani na mizaha. Ukijisikia hali siyo nzuri kimbilia kwenye Vituo vya afya kupata msaada.

Niombe MSD sanitizer zipatikane kwa urahisi na kwa bei mafuu mijini na vijijini ili wote tupate kujikinga na COVID-19.

Zaidi tuendelee kumcha Mungu tumuombe pia atusamehe dhambi zetu na hatimaye atunusuru na COVID-19. Hakuna lisilowezekana kwa Mungu, yeye ni mwema sana na Watanzania tutasalimika.                                                                                            

Dk Kilahama ni Mwenyekiti wa Chama cha Uhifadhi wa Mazingira na Wanyamapori nchini (WCST). Maoni haya ni yake binafsi na wala si msimamo wa Nukta Habari. Tuma maoni yako kupitia maoni@nukta.co.tz au WhatsApp: +255 677 088 088.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW