“Panya Road” walivyoacha maumivu kwa wakazi wa Dar mwaka 2022

December 29, 2022 11:23 am · admin
Share
Tweet
Copy Link
  • Baadhi wajeruhiwa na baadhi wapoteza maisha 
  • Swali ni je, huu ndo mwisho au wanajipanga?

Dar es salaam. ‘Panya road’ sio jambo geni masikioni mwa Watanzania na wale wanaofuatilia yanayojiri Tanzania hivi sasa. Pale mtu asikiapo ni ama kuna tukio limefanywa na kikundi hicho cha uhalifu au ni taarifa ya Polisi ikielezea kukamatwa kwao. 

Hata hivyo, tukiwa tumakaribia mwisho wa mwaka 2022, matukio ya kundi hilo kwa sehemu kubwa yamedhibitiwa hayasikiki kama ilivyokuwa miezi minne iliyopita. 

Kundi hili la uhalifu wa kutumia silaha lilianza kupata umaarufu kutokana na aina ya utekelezaji wa matukio yake ambapo vijana wenye umri kuanzia miaka 14 hutembea katika makundi makubwa yenye wastani wa watu 10 hadi 30 na kufanya uhalifu.

Wakiwa na silaha za jadi kama mapanga, visu, nondo, nyundo, marungu, wamekuwa wakipora watu mali zao barabarani kabla ya kuanza kuvamia nyumba za watu majira ya usiku kwa kuvunja milango, kujeruhi  na kupora mali.

Mwaka 2022 umekuwa wa machungu kwa baadhi ya wakazi wa jiji la Dar es salaam  kutokana na kuporwa mali zao, kusababishiwa majeraha na wengine kupoteza ndugu zao ambao waliuawa na vijana hao. 

Haya ni miongoni mwa baadhi ya matukio ambayo hayatasahaulika kwa wakazi wa jiji hilo:

Mmmoja wa wakazi wa Nguvu Mpya, Zingiziwa jijini Dar es salaam, akionesha majeraha aliyopata baada ya kujeruhiwa na panya road. Picha l The Chanzo

1. Aprili 24, Chanika

Usiku wa kuamkia Jumapili ya Aprili 24 mwaka huu, Mtaa wa Nguvu Mpya uliopo Kata ya Zingiziwa uligubikwa na vilio mara baada ya kundi hilo kuvamia mtaa huo na kupora mali na kujeruhi watu wapatao 23 kwa kuwakata sehemu mbalimbali za miili yao.

Jeshi la Polisi nchini lilitoka hadharani na kutangaza kuwakamata vijana 10 wenye umri kati ya miaka 13 hadi 21 waliotuhumiwa kuhusika na uhalifu huo.

Tukio hilo lilimuibua pia Waziri wa Mambo ya Ndani Hamad Masauni aliyetoa siku saba kwa jeshi hilo kuhakikisha limewakamata wote waliohusika na uhalifu huo huku aliyekuwa Inspekta Jenerali wa Jeshi la Polisi (IGP) Simon Sirro akiahidi kulivalia njuga suala hilo.

2. Septemba 6, Kinyerezi

Maumivu ya Panya Road yalihamia kwa wakazi wa mtaa wa Kabaga uliopo Kinyerezi ambapo nyumba 24 zilivamiwa na kundi hilo. Watu wanne walikimbizwa katika hospitali ya Amana mara baada ya kupata majeraha katika purukushani hizo.

Watu waliibiwa mali zao na wengine kuachwa na majeraha mbalimbali katika miili yao. Tukio hili nalo liliacha taharuki kubwa kwa wakazi wa jiji hilo linalokuwa kwa kasi Afrika Mashariki. 


Soma zaidi


3.  Septemba 11,  Majengo Vingunguti

Vilio vitokavyo na uvamizi wa kundi hili la vilihamia tena kwenye familia ya Kinahe Baraka anayedaiwa kuvamiwa na Panya Road Septemba 11, 2022.

Kwa mujibu wa mahojiano yaliyofanywa na Mwananchi Digital baba mzazi wa binti huyo Baraka Swedy alikiri kutokea kwa tukio hilo majira ya saa mbili usiku ambapo mtu mmoja aliuawa.

4. Septemba 14, Kawe Mzimuni

Wakazi wa Kawe Mzimuni Manispaa ya Kinondoni  sio tu waligubikwa na simanzi kwa kuporwa mali zao bali uvamizi huo uliondoka na maisha ya Mariam Baso (24) na kujeruhi wengine wawili.

Aidha siku hiyo hiyo yaani alfajiri ya Septemba 14 wakazi wa Buguruni kisiwani nao walikumbwa na kadhia hiyo ya kuporwa na kujeruhiwa na silaha za jadi kama mapanga na visu.

Mfululizo wa matukio hayo,  Mbunge wa Viti Maalumu kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kumuomba Spika wa Bunge la Tanzania kuahirisha kikao cha bunge kilichokuwa kikiendelea Septemba 15 na kujadili suala la Panya Road kama jambo la dharura.

Hata hivyo, Spika Dk Tulia Ackson hakuridhia ombi hilo na badala yake akaiagiza Serikali kushughulikia tatizo hilo kwa haraka.

“Kwa sababu wananchi wanapata athari Serikali ichukue hatua za haraka kudhibiti jambo hili,” alisema Spika Tulia.

Kwa nyakati tofauti viongozi wa Serikali na Jeshi la Polisi wametoa kauli mbalimbali zinazoonyesha hatua walizozichukua kukabiliana na  vikundi vya uhalifu jijini hapa.

Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Godwin Gondwe (Kushoto) akizungumza na baba mzazi wa Mariam Baso aliyeuawa kwa kushambuliwa sehemu mbalimbali za mwili na panya road. Picha l Millard Ayo

Siku moja mara baada ya wahalifu hao kuvamia na kuua mtu mmoja Kawe na Vingunguti, Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla alisema wametoa askari 300, kwa ajili ya kuendesha operesheni ya kuwakamata Panya Road.

Uhalifu huo ukamuibua kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es salaam, Jumanne Muliro, Septemba 18 na kutangaza kuwa Jeshi la Polisi limewaua watu sita wanaohusishwa na vitendo vya uhalifu wa silaha maarufu kama Panya Road.

Tukio hilo lilitokea eneo la Makongo ambapo kwa mujibu wa Muliro watuhumiwa hao walikuwa wanajiandaa kwenda kufanya tukio Goba na walipoteza maisha wakati wakiwahishwa hospitali baada ya kukataa kusalimu amri na kutaka kudhuru askari.

Hata hivyo pamoja na juhudi hizo zinazochukuliwa na Serikali bado vikundi hivi vimekuwa vikiibuka na kupotea na si kutokomea moja kwa moja jambo ambalo linaibua swali la kwanini kikundi hicho hakitokomezwi.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam Jumanne Muliro akiwaonesha waandishi wa habari silaha walizokutwa nazo watuhumiwa wa vitendo vya uhalifu wa kutumia silaha panya road waliouawa eneo la Makongo jijini Dar es Salaam. Picha. Millard Ayo

Nini kifanyike?

Kutokana na suala hili kukaa kijamii zaidi, www.nukta.co.tz imezungumza na viongozi wa dini ambao maoni yao wameyaelekeza kwa jamii kufuata miongozo ya dini ambayo inakataza kujihusisha na vitendo vya kihalifu.

Mchungaji wa Kanisa la  Building the Temple of God, Iman Mwakanyamale amesema uhalifu ni kitu ambacho kipo kwenye jamii nyingi  ila ushiriki wa vijana wadogo ni jambo la hatari kwa Taifa na dini inaweza kuwabadili vijana hao na kuwaleta kwenye tabia na mienendo inayofaa.

“Tunaweza tukawakamata, tunaweza kuwafunga na kuwapiga lakini tujue kwamba kuna kitu cha ndani ambacho huwa ndio kinambadilisha mtu. Mtu habadiliki kwa kupigwa wala kwa kufungwa kuna namna tofauti tunavyotakiwa kushughulika na hawa vijana kwa sababu hawa ndio wamebeba maono ya ulimwengu na ya nchi,” amesema Mchungaji Mwakanyamale.

Kwa upande wake Maalim wa Msikiti wa Meco wa Kunduchi Mtongani jijini Dar es Salaam, Omary Kebula ameiambia www.nukta.co.tz kuwa kuwepo kwa vikundi hivyo vya kihalifu kunatokana na kupungua kwa  mafundisho kwenye jamii huku akitoa wito kwa wazazi kuwa mfano mwema kwa watoto wao.

“Tabia hizi mbaya zinazoenea kwenye jamii yetu ni mafundisho ya kidini kupungua kwa walezi au wazazi wa vijana hawa wanaohusika na masuala ya uhalifu. Dini zote zinakataza kabisa maovu, kama tukiwa wasikivu na watekelezaji wa amri za kidini basi duniani pangekuwa mahali pa kustarehe,” anasema Maalim Kebula.

Juni mwaka huu wakati Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan alipokuwa akitoa hotuba wakati wa uzinduzi wa Taasisi ya Mwanamke Initiatives Foundation (MIF) visiwani Zanzibar aliwasihi wazazi kuwalea vizuri watoto wao kwa kufuata misingi ya maadili ili kuepusha kuibuka kwa makundi ya kihalifu yanayoisumbua jamii pamoja na Serikali.

“Ulezi wa kulea mwana sio wa mzazi peke yake, ni mzazi, taasisi, Serikali na jamii, wote tulee watoto wetu kwa sababu tusipowalea vizuri tunazalisha panya road, na mnajua wanavyosumbua, kwa wale ambao hamjawaona mnasikia kwenye taarifa za habari, ” alisema Rais.

Inaendeshwa na Nukta AI

Follow us on TikTok

Nukta Habari

FOLLOW NOW
Subscribe to our channel

Nukta TV

SUBSCRIBE NOW
Wabunge waliokwenda Morocco bila kibali kikaangoni , utoro ukiibuliwa bungeni

Wabunge waliokwenda Morocco bila kibali kikaangoni , utoro ukiibuliwa bungeni

Nukta TV

Mfahamu Leonard Mususa Alama ya Ungozi iliyoacha majonzi kwa 'MACEOs' Tanzania

Mfahamu Leonard Mususa Alama ya Ungozi iliyoacha majonzi kwa 'MACEOs' Tanzania

Nukta TV

Bei za mafuta mwezi Juni hizi hapa, dizeli ikipaa kwa Sh85

Bei za mafuta mwezi Juni hizi hapa, dizeli ikipaa kwa Sh85

Nukta TV