Unavyoweza kupata huduma Jeshi la Polisi bila kufika kituoni
- Ni kupitia Jukwaa la Huduma za Kielektroniki (e-Services)
- Unaweza kupata huduma kupitia tovuti au programu tumishi inayopatikana katika majukwaa ya programu
- Ni muhimu kwenda kituoni hata baada ya kuhudumiwa kupitia jukwaa hilo
Dar es salaam, ‘Kutoa taarifa polisi’, huwa ni wazo la kwanza watu wengi hufikiria pale wanapopatwa na changamoto inayohitaji msaada wa jeshi la polisi, inaweza kuwa shida ya kiusalama, kupotelewa au kuibiwa mali au pale unaposhuhudia tukio la kihalifu.
Changamoto ni pale ambapo unakuwa huna uwezo wa kufika kituoni muda huo ili kupata msaada husika, sasa ondoa shaka, mradi tu uwe una uwezo wa kupata huduma ya intaneti kupitia kifaa chako cha mawasiliano unaweza kuhudumiwa na polisi bila wewe kufika kituoni, kivipi?
Ni kupitia jukwaa la Huduma za Kielektroniki (e-Services) linalomilikiwa na Jeshi la Polisi ambalo huwawawezesha wananchi kuripoti matukio na shughuli zinazotiliwa shaka kwa haraka na kwa urahisi, na kusaidia kuzuia uhalifu.
Jukwaa hutoa huduma mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa ya mali iliyopotea, kuwasilisha malalamiko, kuripoti unyanyasaji kwa watoto, kuripoti vyombo vya moto vilivyoibiwa, kupata leseni ya udereva, kupata kibali cha mikutano, kupata cheti cha idhini, kuripoti ajali, na aina nyinginezo za taarifa.
Jukwaa hili linaweza kutumiwa vyema na wananchi wanaothamini urahisi na kasi ya kuripoti matukio kwani linaruhusu kutoa taarifa ya shughuli zinazoweza kutishia usalama kwa urahisi bila kulazimika kwenda kituoni.
Huduma hii ya kielektroniki pia inasaidia kuboresha mawasiliano kati ya polisi na jamii, jambo ambalo linarahisisha juhudi bora zaidi za kuzuia uhalifu.
Soma zaidi
-
Jinsi ya kuhariri na kuficha meseji zako WhatsApp
-
Twitter yaja na mbinu mpya kulinda meseji za watumiaji wake
Unaipataje huduma hii
Unaweza kuipata huduma hii kupitia tovuti ya Jeshi la Polisi Tanzania au kupitia programu ya simu ambayo inapatikana kwa kupakuliwa kwenye Apple Store kwa watumiaji wa simu iphone au Google Play kwa simu za android.
Jukwaa hili linapatikana masaa 24 siku saba za wiki ili kuruhusu raia kuripoti matukio wakati wowote wa mchana au usiku.
Jukwaa la Huduma za kielektroniki ni sehemu ya juhudi zinazoendelea za serikali ya Tanzania za kulifanya jeshi la polisi liwe la kisasa na kuboresha ufanisi wake katika kupambana na uhalifu.
Hivi karibuni kuliibuka matukio mbalimbali ya kihalifu yaliyowahusisha vijana waliokuwa na umri wa miaka kati ya 13 hadi 19 maarufu kama panya road ambao walikuwa wakifanya vitendo vya kupora na kujeruhi katika maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam.
Licha ya Serikali kufanikiwa kudhibiti vitendo hivyo, miongoni mwa malalamiko yaliyotolewa na wananchi waliodhurika na wahalifu hao ni kuchelewa kufika kwa Jeshi la Polisi katika maeneo ya tukio kiasi cha kukuta wameshaibiwa na kujeruhiwa.
Hata hivyo lichya ya kutoa taarifa na kuhudumiwa kupitia jukwaa hili bado utalazimika kufika katika kituo cha polisi baada ya muda ili kuthibitisha changamoto uliyoripoti hususani hasa kama umepoteza nyaraka kama vitambulisho au vyeti.
Latest
