Madhara utakayopata usipobadili tairi ya gari kwa wakati
- Kila tairi hutengenezwa kulingana na matumizi ya chombo husika.
- Inatakiwa kubadilishwa mara muda wake unapokwisha vinginevyo ni majanga.
Dar es Salaam. Bila shaka umewahi kusifia au kumsikia mtu akikisifu chombo cha moto, kutokana na uwezo wake wa kubeba uzito fulani wa mizigo, kuwa na kasi kubwa au kuwa na mwendo thabiti kiwapo barabarani.
Je umewahi kujiuliza hayo yote yanawezeshwa na nini, jawabu ni ‘gurudumu’ au wengi wamezoea kuita tairi.
Gurudumu ni muunganiko wa raba iliyokatika muundo wa duara pamoja na ringi nzito ya duara ambayo huundwa kwa chuma au alminiamu, na huwekwa katika vyombo vya usafiri vinavyotumia ardhi.
Pamoja na sifa nyingine za chombo husika, kama ubora wa injini, u ghali wa chombo husika, na malighafi zilizotumika kutengeneza chombo hicho tairi ni mhimili muhimu sana katika chombo cha moto ambao unatakiwa kutupiwa jicho la karibu kutokana na umuhimu wake.
Baadhi ya watu wamekuwa wakikumbana na changamoto mbalimbali ikiwemo ajali, kubadili tairi mara kwa mara, au kushindwa kuhimili chombo husika kutokana na kutokuwa na uelewa wa kutosha kuhusiana na tairi.
Makala haya yanaangazia mambo muhimu ambayo mtumiaji wa chombo cha moto anapaswa kuyafahamu kuhusiana na tairi ambapo Nukta habari (www.nukta.co.tz) ilifanya mahojiano na mtaalamu wa tairi za gari Thadei Mpangala aliyepo Mabibo, jijini Dar es Salaam.
Zinahohusiana
Tairi hutengenezwa kulingana na matumizi
Kila tairi hutengenezwa kulingana na matumizi ya chombo husika. Mfano tairi inayotumika kwenye magari ya mizigo si sawa na inayotumika kwenye magari yasiyo ya mizigo. Tairi inayotumika kwenye mazingira ya joto haifanani na ile ya mazingira ya baridi.
Wamiliki wa vyombo vya moto wanashauriwa kuzifanyia uchunguzi tairi zinazokuja na vyombo vyao hususani kutoka nchi zenye baridi ili kujua ubora na aina ya tairi zilizopo ili kama hazioani na matumizi zibadilishwe.
Mpangala anawashauri wamiliki wa vyombo vya moto, kuzingatia ubora wa tairi kwa kufahamu kwanza matumizi ya tairi husika kabla hajanunua kuliko kununua tairi ambayo haiendani na matumizi ya chombo chake.
Muda wa kubadilisha tairi
Kama zilivyo spea nyingine za vyombo vya moto ambavyo huhitaji kubadilishwa baada ya muda fulani, tairi nazo hivyo hivyo.
Kawaida tairi inatakiwa kubadilishwa kila baada ya miaka mitano au sita kutegemeana na ubora wa tairi, matumizi ya chombo husika pamoja na hali ya barabara ambapo chombo hicho hupita.
“Tairi ya gari uwezo wa kukaa ni miaka minne ingawa zipo ambazo zinaweza kukaa miaka sita bila kubadilishwa, inategemea unatumiaje, kama matumizi yako ni ya kila siku inaweza kuisha haraka. Gari ikipita kwenye barabara nzuri nayo inasaidia kuifanya ikae muda mrefu, “ anasema Mpangala.
Unaweza kubaini kuwa muda wa tairi umekwisha kwa kuangalia idadi ya miaka ambayo imetumika ambayo huwa inaandikwa kwenye tairi, lakini pia kupitia kipimo ‘vernier caliper’ ambacho huwekwa kwenye tundu lililopo kwenye tairi na unene wake unatakiwa usiwe chini ya milimita mbili.
Madhara yanayoweza kukupata iwapo hautabadili tairi kwa wakati ni pamoja na kutokuwa na uwezo wa kukiongoza na kudhibiti chombo chako hivyo unaweza kupata ajali, utelezi wa mara kwa mara na breki kushindwa kufanya kazi ipasavyo.
“Kwanza sheria hairuhusu kutumia tairi ambayo imekwisha muda wake, kwa sababu ni hatari, tairi ambayo kashata zake imeisha inaweza kusababisha kufeli kwa breki, au kuteleza,” anasema Mpangala
Haishauriwi kununua tairi ambazo zimetumika kwa ajili ya matumizi ya gari yako. Pichal Esau Ng’umbi/Nukta Africa.
Usijichanganye ukanunua mtumba
Uzuri wa ukakasi ndani kipande cha mti, ndicho ambacho huwa kinawakuta watu wanaopenda kununua tairi za mtumba kwa kuamini zitawafaa matokeo yake wanaingia gharama ya matengenezo au kununua mpya.
Kwa mujibu wa Mpangala tairi ni spea ya utofauti ambayo inahitaji umakini mkubwa kabla ya kununua hivyo wamiliki waepuke kununua tairi ambazo tayari zimeshatumika.
“Kwa uzoefu wangu tairi za mtumba mara nyingi hazina ubora unaotarajiwa, kwa macho zinaonekana zina ubora ila kwenye matumizi ni tofauti, napenda watu wafahamu zile hazina ubora, labda spea nyingine,” amesema Mpangala ambaye ni fundi kwa muda wa miaka 22 sasa.
Namba muhimu za kuzisoma kwenye tairi
Watengenezaji wa tairi huandika namba tofauti tofauti katika gurudumu ambazo huwa na maana fulani, ni jukumu la mnunuaji kuelewa maana ya namba hizo ili zimsaidie katika kufanya maamuzi.
Miongoni mwa namba hizo ni mwaka ambao tairi hiyo imetengenezwa, ukubwa wa mzunguko, namba ya rimu inayotakiwa kuvishwa, uzito ambao inaweza kuhimili pamoja na kiwango cha joto ambacho tairi hiyo inaweza kuhimili.
Tangazo:
Latest



