Simiyu yashika mkia kwa pato la mtu mmoja Tanzania Bara, 2025

- Mkoa huo umekuwa na wastani mdogo zaidi wa pato kwa mtu mmoja kwa miaka mitano mfululizo, licha ya kurekodi ongezeko la asilimia 58.8 kutoka mwaka 2020.
Dar es Salaam. Kwa miaka mitano mfululizo mkoa wa Simiyu umeendelea kushika nafasi ya kwanza kama mkoa wenye watu wenye kipato cha chini zaidi Tanzania Bara.
Ripoti ya Takwimu za Msingi ya mwaka 2025 iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) inabainisha kuwa mkoa huo ulirekodi pato la Sh1,742,809 kwa kila mkazi (GDP per Capita) mwaka 2025.
Pato la Taifa kwa mtu mmoja, (GDP per capita), ni kipimo kinachoonyesha wastani wa thamani ya bidhaa na huduma zote za mwisho zinazozalishwa ndani ya eneo husika kwa kipindi fulani, ikilinganishwa na idadi ya watu wanaoishi katika eneo hilo.
Mtaalamu wa Uchumi kutoka Dar es Salaam, Paul Chengula ameiambia Nukta Habari kuwa kipimo hicho hupimwa kwa kugawanya thamani ya Pato la Taifa la eneo husika kwa idadi ya wakazi wake.
Hata hivyo, kipimo hiki huonyesha wastani wa pato kwa kila mkazi anayeishi na kufanya shughuli za kiuchumi katika mkoa huo na si mapato halisi anayopata kila mtu.
Hivyo, baadhi ya watu wanaweza kuwa na kipato kikubwa zaidi ya kiwango hicho na wengine kuwa na kipato cha chini zaidi.
Pato lililorekodiwa Simiyu mwaka 2025 ni sawa na ongezeko la asilimia 10.6 kutoka wastani wa pato la Sh1,576,143 kwa kila mkazi mwaka 2024.
Uchambuzi uliofanywa na Nukta Habari umebaini kuwa licha ya wastani wa pato la wakazi wa Simiyu ambao idadi yao ni milioni 2.1 kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, kuongezeka kiduchu, bado pato hilo ni dogo ukilinganisha na wastani wa pato la wakazi wote wa Tanzania Bara.
Pato la Simiyu lililorekodiwa mwaka 2025 lilikuwa chini kwa asilimia 50.8 ikilinganishwa na wastani wa pato la Tanzania Bara, lililofikia Sh3.5 milioni.
Aidha, pato hilo liko chini kwa takriban mara nne ya pato la Sh6,776,483 lililorekodiwa kwa mkazi mmoja wa Dar es Salaam, likiwa ndio pato la juu zaidi kwa mtu mmoja mmoja Tanzania Bara.
Sababu zatajwa
Hata hivyo, Chengula anaeleza kuwa sababu za wakazi wa Simiyu kuwa kinara wa pato dogo kwa miaka mingi mfululizo ni uzalishaji mdogo katika uchumi kulinganisha na idadi ya watu waishio eneo hilo.
“Unaweza ukawa na idadi kubwa ya watu lakini uzalishaji wako ukawa mdogo…huwezi kufananisha na miji mikubwa kama Dar es Salaam ambao hata kama una watu wengi uzalishaji wake pia ni mkubwa,” amefafanua Chengula.
Kwa mujibu wa NBS, Simiyu ilirekodi pato la mkoa la Sh4.23 mwaka 2025, nafasi ya pili kutoka mwisho ikitanguliwa na Katavi iliyorekodi pato la Sh3.19 trilioni.
Kwa upande mwingine, Dar es Salaam ndiyo iliyokuwa na wastani mkubwa zaidi wa pato kwa mtu mmoja mwaka 2025, ikiwa na Sh6,776,483, ikifuatiwa na Iringa Sh5,705,463 na Kilimanjaro Sh5,195,767.
Mikoa 10 yenye wastani mdogo zaidi wa pato
Baada ya Simiyu, Mkoa wa Kagera unashika nafasi ya pili kwa mwaka wa tano mfululizo ukiwa na wastani wa Sh1,850,225 kwa mtu mmoja, ukifuatiwa na Singida wenye Sh1,985,754.
Mikoa mingine ni Dodoma wenye wastani wa Sh2,114,849, Pwani Sh2,162,446, Tabora Sh2,295,838, Kigoma Sh2,300,206, Katavi Sh2,458,982, Rukwa Sh2,877,688 na Songwe Sh2,941,703.