Viazi vitamu, ndizi mbichi, njegere kavu vyapaisha mfumuko wa bei
- Kasi ya mfumuko wa bei kwa mwaka ulioishia mwezi Septemba, 2026 imeongezeka hadi asilimia 3.9.
- Viazi vitamu, unga wa muhogo, ndizi mbichi, njegere kavu na nyingine zisizo za vyakula zimechangia kupanda kwa bei za vyakula.
Dar es Salaam. Kasi ya mfumuko wa bei za bidhaa za vyakula na vinywaji baridi kwa mwaka ulioishia mwezi Septemba, 2026 umeongezeka hadi asilimia 3.9 kutoka asilimia 3.7 kwa mwaka ulioishia mwezi Agosti, 2026 ikichochewa zaidi na kupanda kwa baadhi ya bei za bidhaa za vyakula ikiwemo viazi vitamu.
Mfumuko wa bei ni hali ya kupanda kwa bei za huduma na bidhaa katika uchumi kwa kipindi fulani.
Kwa lugha rahisi, ni hali ambayo fedha ile ile ambayo mwananchi aliweza kununua kiasi fulani cha bidhaa, inanunua bidhaa nyingi au chache zaidi baada ya kipindi fulani kulinganisha na awali.
Kwa mujibu wa taarifa ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) iliyotolewa Oktoba 8, 2026, inabainisha kuwa kiwango cha jumla cha ongezeko la bei za bidhaa na huduma katika mwaka ulioishia Septemba 2026 kilikuwa sawa na kiwango kilichorekodiwa katika mwaka ulioishia Agosti 2026.Â
Kwa mujibu wa Nbs miongoni mwa bidhaa zilizochangia kupaa kwa mfumuko wa bei kwa mwaka unaoishia Septemba 2026 ni viazi vitamu na unga wa muhogo, ambavyo bei zake zimepanda kwa asilimia 3.9 kila moja, ndizi mbichi kwa (asilimia 3.7) na njegere kavu kwa (asilimia 3.1)
Bidhaa nyingine zilizopanda bei ni mihogo mibichi kwa asilimia 2.0, choroko kwa (asilimia 1.8), samaki wabichi kwa (asilimia 1.7), karanga mbichi kwa (asilimia 1.5) na maziwa ya ng’ombe kwa (asilimia 0.8).

Vilevile, bei za maharage zimeongezeka kwa asilimia 0.4, unga wa ngano kwa asilimia 0.3, mafuta ya kupikia kwa (asilimia 0.3), kuku wa kienyeji kwa (asilimia 0.2), mtama kwa (asilimia 0.1) na nyama ya kuku kwa (asilimia 0.1). Vinywaji baridi jamii ya soda navyo vimepanda kwa asilimia 1.4.
Mbali na chakula, bei za baadhi ya bidhaa za matumizi ya nyumbani pia zilipanda, huku saruji ikiwa asilimia 3.9, nauli za pikipiki/bodaboda kwa (asilimia 5.8) na nishati ya kuni (asilimia 4.6 ).